2016-04-16 16:06:00

Tanzania inataka kucharuka katika viwanda! Ili wengine wasome namba!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda kama mkakati wa kukuza uchumi ili nchi iweze kutoka kwene umaskini na kufikia uchumi wa kati. Waziri Mkuu amesema hayo Alhamisi, Aprili 14, 2016 alipofanya mazungumzo na Waziri wa Biashara wa Oman, Dk. Ali Masoud Al Sunaidy ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam. Amesema mbali na kuimarishwa kwa sekta ya viwanda, pia Serikali imelenga kuboresha sekta za nishati, uchukuzi na kilimo ambazo zitawezesha Taifa kufikia malengo yake ya kufikia uchumi wa kati.

“Sekta ya viwanda ni eneo ambalo tunataka kuliimarisha kwa sababu litatuwezesha kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini jambo ambalo pia litakuza  ajira kwa vijana. Hivyo nawakaribisha mje kuwekeza nchini,” amesema. Pia Waziri Mkuu amemuhakikishia kuwa serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa kutoka Oman kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Dk. Al Sunaidy amefurahishwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kwamba wapo tayari kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo viwanda vya usindikaji, kilimo kinachotumia teknolojia ya kisasa, na mafuta, gesi, na ujenzi wa bandari. Akitoa ufafanuzi, Waziri huyo alisema: “Oman ina bandari ya Salala ambayo ni moja kati ya bandari bora duniani yenye uwezo wa kupakua makontena 45 kwa saa. Lakini pia tunayo bandari ya Sohar maarufu kwa bidhaa za viwandani ambayo ina uwezo wa kupakua makontena 32 kwa saa,” amesema. Dk. Al Sunaidy yuko nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku tatu akiwa ameambatana na wafanyabiashara 80 wa Oman kwa mwaliko wa Kiserikali kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi.

Naye Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amesema anatambua kuwa Oman imepiga hatua katika teknolojia ya gesi asili ya kimiminika (LNG) hivyo ana imani Tanzania itapata ujuzi  kutoka kwao. Amesema wafanyabiashara hao wana fursa ya kuwekeza kweye ujenzi ujenzi wa viwanda vya mbolea katika mikoa ya Lindi na Mtwara lakini pia wanaweza kuwekeza kwenye bandari za Tanga, Bagamoyo, Kilwa, Lindi na Mtwara ambazo Serikali imepanga kuboresha miundombinu yake.

METOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

 








All the contents on this site are copyrighted ©.