2016-04-16 12:58:00

Sala ya Viongozi wa Makanisa kwa wahamiaji na wakimbizi!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Askofu mkuu Jerome II, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 baada ya kukutana na kusalimiana na wananchi wanaoishi katika Bandari la Lesvos, Ugiriki, walisali kwa pamoja ili kuwaombea wakimbizi na wahamiaji waliofariki dunia wakiwa njiani kutafuta hifadhi na usalama wa maisha! Baba Mtakatifu Francisko amesema, kwa bahati mbaya makaburi ya watu hawa hayana majina wala kumbu kumbu yoyote, lakini ni watu wanaofahamika na kupendwa na Mungu na kwamba, kamwe hatawasahauliwa; wakumbukwe kwa sadaka na matendo yao ya kijasiri na wala si maneno matupu!

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale wote walijitosa katika safari ya kutafuta usalama na maisha bora zaidi, kwa kuvumilia woga, wasi wasi, nyanyaso na dhuluma na hatimaye, wakafika bandari salama. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwasahau watoto wake kama alivyofanya kwa Mtoto Yesu na Familia Takatifu kwa kuwapatia hifadhi salama; kwa sasa awe karibu na kuwalinda watu wanaoteseka, ili kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, Jumuiya ya Kimataifa ijikite zaidi katika kudumisha misingi ya uhuru, utu na amani na kamwe asiwepo mtu anayelazimika kukimbia makazi yake kwa lazima!

Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasaidia watu kuondokana na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, bali waoneshe jicho la upendo na kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tayari kushirikishana karama za zawadi mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama familia moja ya binadamu. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, binadamu wote ni wasafiri kuelekea kwenye makao ya milele ambako, kila chozi litafutwa, amani na usalama vitadumishwa milele!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika sala yake ameombea lishe kwa watoto wadogo, elimu kwa vijana, nguvu kwa watu wazima; ujasiri kwa wale waliokata tamaa, mshikamano kwa wale waliotengana na wenzi wao; na kwamba Mwenyezi Mungu aendelee kusafiri na wasafiri wote; awalinde na kuwasimamia wajane na yatima;  awafungulie wafungwa na kuwaponya wagonjwa.

Amewaombea na kuwakumbuka watu wanaoishi ugenini, katika mazingira magumu na hatarishi; wanaohitaji msaada na wale waliokata tamaa na hasa zaidi wale wanaokimbilia wema na huruma ya Mungu. Wote hawa waweze kumiminiwa huruma na kupata wokovu! Amewaombea wale wote waliolala katika usingizi wa amani wakiwa njiani kutoka katika maeneo ya vita, kuelekea katika nchi ya usalama, amani na maendeleo. Anamwomba Mungu awasaidie wasiokuwa na matumaini, wanaoteseka kutokana na safari ngumu na awe ni tabibu wa wagonjwa na awe yote kwa wote wanaomtumainia kutoka katika maeneo yaliyokumbwa na majanga asilia, vita na mipasuko ya kijamii!

Askofu mkuu Jerome II amemwomba Mwenyezi Mungu aliyeonesha ukuu dhidi ya nguvu ya shetani na kifo, awajalie maisha ya uzima wa milele wale wote waliotangulia kwenye usingizi wa amani; malisho mabichi na utulivu, mbali kabisa na machungu na magumu ya maisha ambayo walikuwa wanayakimbia. Awasamehe dhambi za ona kuwaonesha uzuri na wema wake usiokuwa na mipaka, kwani Mungu ni mwema na sheria yake ni ukweli na kwamba, ni chemchemi ya ufufuko wa wafu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.