2016-04-16 13:33:00

Papa Mstaafu Benedikto XVI atimiza Miaka 89!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Aprili 2016 akiwa njiani kuelekea Kisiwani Lesvos, Ugiriki, amekutana na kuzungumza na waandishi wa habari 50 waliokuwa kwenye msafara wake. Hija hii ya kitume ni tofauti kabisa na hija nyingine zinazofanywa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kusema kwamba, hija hii imesheheni simanzi na huzuni! Ni safari ambayo inawapeleka kuona na kuonja hali tete ya binadamu kuwahi kutokea tangu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Ni safari itakayowawezesha kuona mateso na mahangaiko ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi zao, wakitafuta hifadhi na usalama wa maisha yao Barani Ulaya. Wanakwenda kutembelea kaburi la wakimbizi na wahamiaji wanaomezwa na kufunikwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania ambako hawatakumbukwa kamwe, lakini majina yao yameandikwa mbele ya uso wa huruma wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, huu ndio ujumbe ambao angependa waandishi wa habari waweze kuufikisha kwenye vyombo vyao vya habari.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia nafasi hii kutuma salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 89 tangu alipozaliwa. Anamwombea afya njema ya roho na mwili, ili aendelee kuwa karibu na Kanisa kwa kutoa huduma ya sala kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.