2016-04-16 07:50:00

Ni kwa ajili ya ustawi na mafao ya familia!


Katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuitia shime Familia ya Mungu nchini Poland na kwamba, ataungana nao kwa karibu zaidi wakati wa maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa nchini Poland mwishoni mwa Mwezi Julai 2017. Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee, umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni umoja unaojikita katika imani, upendo, mafundisho na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake, daima wakihakikisha kwamba, Poland inaendelea kua aminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Huu ni ujumbe uliotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 15 Aprili 2016 wakati alipokuwa anawasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Kwa njia ya umoja, mshikamano na ushuhuda wa imani tendaji, Poland imeweza kuvuka kinzani na magumu yaliyosababishwa na utawala wa Kikomunisti, changamoto kwa Maaskofu kuendelea kusoma alama za nyakati, kwa kushuhudia uwepo endelevu wa Kanisa kati ya watu!

Hiki ni kipindi cha Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko sanjari na uaminifu kwa wito wake! Ni muda wa kujenga na kuimarisha umoja wa kimissionari, ili kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya furaha na huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati zote. Uinjilishaji ni changamoto pevu inayowataka waamini wote kujifunga kibwebwe ili kweli Habari Njema ya Wokovu iweze kuwafikia watu wengi zaidi. Licha ya Poland kupiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini bado kuna makundi makubwa ya maskini, watu wasiokuwa na fursa za ajira, wagonjwa na wazee; hawa wote Kanisa linapaswa kuwa karibu nao ili kuwaonjesha Injili ya upendo, huruma na mshikamano.

Kardinali Parolin anakaza kusema,  familia ni kiini cha maisha ya kijamii, mahali ambapo wanajifunza kuishi kwa amani, utulivu na mshikamano; familia ni mahali muafaka pa wazazi kurithisha imani, matumaini na mapendo kwa watoto wao. Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya Upendo ndani ya familia "Amoris laetitia" ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu kuhusu familia.

Ni wosia unaoichangamotisha familia kufanya tafakari ya kina; kujenga na kudumisha majadiliano katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, hususan utume kwa familia. Wanafamilia wajitahidi kujenga na kusimika maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda wa furaha na amani, changamoto kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya! Wosia huu ulisaidie Kanisa na familia kuwa imara na thabiti; kukua na kukomaa katika fadhila ya upendo, uaminifu na ukarimu; uvumilivu na huruma; msaada na mshikamano kwa wengi!

Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland ni mchakato ambao umewawezesha waamini nchini humo kuwa ni sehemu ya Fumbo la mwili wa Kristo, yaani Kanisa, changamoto ya kutoa huduma bora kwa familia ya Mungu nchini humo, kwa kumshuhudia Kristo Mfufuka. Kanisa nchini Poland lijielekeze katika hija ya kumfuasa Kristo peke yake, kwa kujiaminisha katika mwanga wa Neno la Mungu; Majadiliano pamoja na kugundua uwepo endelevu wa Mungu katika matukio, historia na maisha ya watu! Wawe ni watu wanaokabiliana na changamoto za maisha ka ujasiri na uwazi zaidi.

Wakati huo huo, Kardinali Parolin katika utangulizi wa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Watakatifu Petro na Paulo, Jimboni Poznan, amewapatia waamini salama na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Amewataka waamini kuendelea kushikamana huku wakitembea pamoja na Bikira Maria katika hija ya maisha yao kwani anang’aa duniani kama alama hakika ya matumaini na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri, mpaka Siku ya Bwana itakapowadia.

Bikira Maria ni nyota ang’avu ambayo imeendelea kung’ara katika historia na maisha ya wanchi wa Poland, kamwe hawatelekezi watoto wake hasa wale wenye shida. Bikira Maria ameonesha uwepo wake wa karibu hata pale, wananchi wa Poland waliposhindwa kuwa waaminifu kwa Kristo na Injili yake; ameteseka nao, kama alivyofanya pale chini ya Msalaba, ili kuwaonesha njia sahihi wanayopaswa kufuata!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.