2016-04-16 09:59:00

Msikate tamaa wala kupoteza matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wakimbizi na wahamiaji walioko kwenye kambi ya Moria, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 amesema kwamba, anataka kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote ambao wanateseka kutokana na hamu ya kutaka kupata maisha bora zaidi, baada ya kulazimishwa kuhama makazi yao kutokana vita, kinzani na dhuluma; wengi wao wanataka kusalimisha maisha ya watoto wao wadogo. Watu hawa wameacha mambo mengi mazuri na kwa sasa wanaishi katika hali ngumu zaidi na wala hawafahamu mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni na kwamba, kuna umati mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi wanaotamani kujenga maisha mapya Barani Ulaya!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, viongozi wa Makanisa wameamua kwenda kuwatembelea, ili kuwasikiliza sanjari na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee ili hatimaye, kupata suluhu ya kudumu kwa hali hii tete ya ubinadamu. Wanataka kuzungumza nao katika ukweli na uwazi. Ni matumaini yao kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa makini zaidi kuhusiana na hali hii ya kukatisha tamaa, ili hatimaye, kutoa jibu muafaka mintarafu Jumuiya ya binadamu inayounda familia moja inayowajibika na kutaabikiana.

Inasikitika kuona kwamba, kuna baadhi ya watu hawaguswi hata kidogo na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao, kiasi hata cha kuthubutu kuwanyonya! Hata katika mazingira tete kama haya, bado kuna watu wenye moyo wa ukarimu na upendo wanaweza kujitokeza ili kusikiliza kilio cha ndugu zao wanaoteseka na kusumbuka. Huu ndio ushuhuda unaooneshwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofika Kisiwani hapo ili kuwahudumia! Ni kweli bado kuna mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa, lakini Baba Mtakatifu anapenda kumshukuru Mungu kwamba hata katika mahangaiko yao, bado hajawaacha pweke, kwani kuna watu ambao wanaendelea kuwa ni Wasamaria wema kwa hali na mali!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ujumbe wake kwao ni kushinda kishawishi cha kukosa matumaini, zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kwamba, zawadi hii inafumbatwa katika upendo; uso wa huruma, hali ya kusikilizana, kuelewana na kutiana moyo! Matumaini ni sala ambayo wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kushirikishana katika hija ya maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani yake. Msamaria mwema ni kielelezo cha huruma ya Mungu inayowaambata watu wote, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, changamoto kwa watu kuonjeshana huruma, hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Ni matumaini ya baba Mtakatifu kwamba, wananchi wa Bara la Ulaya watajitahidi kuwa ni Wasamaria wema kwa kujitokeza kutoa msaada wa hali na mali kwa wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha; kwa kujikita katika ari na moyo wa udugu, mshikamano, utu na heshima ya binadamu; mambo msingi yanayopambanua historia ya Bara la Ulaya! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko alitoa baraka yake kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa Barani Ulaya! Anawatakia nguvu na amani itokayo kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.