2016-04-16 10:48:00

Katika hali tete kama hii, uwajibikaji na mshikamano ni muhimu sana!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na viongozi wakuu wa Makanisa, majira ya jioni, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016, amekutana na kuzungumza na Jumuiya Waamini wa Kanisa Katoliki katika Bandari ya Lesvos, huko Ugiriki. Amewashukuru viongozi wa Serikali na Kanisa kwa kumwalika kutembelea Kisiwa cha Lesvos. Kwa namna ya pekee kabisa, amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Ugiriki ambao wameonesha mshikamano wa huruma na huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji, licha ya kukabiliwa na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa.

Wananchi hawa wamefungua nyoyo na malango ya nyumba zao kwa ajili ya kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji kwa kuwashirikisha hata kile kidogo walichokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hakika wamekuwa ni msaada mkubwa kwa wahamiaji ambao wamelamizika kuyakimbia makazi yao! Baba Mtakatifu amewashukuru watu wanaojitolea, vyama vya kitume pamoja na taasisi za serikali na kiraia zinaoendelea kuonesha udugu kama kielelezo cha uwepo wao wa karibu!

Katika mazingira tete kama haya, kuna haja ya kukazia uwajibikaji na mshikamano wa dhati, ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji Kisiwani Lesvos na wale wote walioko nchini Ugiriki, kwani wanaishi katika hofu, wasi wasi na hali ya kukata tamaa kwa kukosa huduma msingi na hivyo kutofahamu mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni. Wasi wasi wa wananchi wa Ugiriki na Ulaya katika ujumla wao, unafahamika na ni haki kabisa. Lakini jambo la msingi ni kutambua kwamba, wahamiaji na wakimbizi hawa kabla ya kutajwa kwa namba ni watu wenye utu, historia, nyuso na majina kamili!

Bara la Ulaya linasadikika kuwa ni makazi ya haki msingi za binadamu, changamoto kwa wananchi wa Ulaya kuhakikisha kwamba, wanashuhudia, wanaheshimu na kulinda haki hizi. Inasikitisha kuona kwamba, kuna umati mkubwa wa watu, hasa watoto ambao hawakufanikiwa kuwasili salama salimini, wakafa maji na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Meditterania. Hizi ni safari hatari sana zinazodhibitiwa na watu wakatili.

Wakazi wa Kisiwa cha Lesvos anasema Baba Mtakatifu bado wanaonesha utamaduni wa utu na heshima kwa binadamu na kwamba, wanataka kujenga madaraja ya kukutana na wakimbizi na wahamiaji badala ya ujenzi wa uzio wa chuma, ili kujisikia kuwa huru na salama zaidi! Kuta za utengano zinachochea ubaguzi badala ya kusaidia kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi; kuta hizi kwa sasa au baadaye zitakuwa ni sababu ya watu kukinzana na kupigana!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapa jambo la msingi ni kujenga na kudumisha mshikamano kwa kutafuta suluhu ya kudumu ya vyanzo vya migogoro na kinzani zinazosababisha watu kukimbia makazi yao. Hii ni fursa ya kuibua mbinu mkakati makini utakaosaidia kukuza na kudumisha amani pale ambapo vita imepandikiza utamaduni wa kifo ili kuzuia na kudhibiti saratani hii isiendelee kuenea sehemu nyingine kwa kupiga rufuku ya biashara haramu ya silaha; kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaochochea kinzani, vurugu na vita, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kuna haja ya kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kushirikiana kwa dhati, ili kuwasaidia watu wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha, changamoto kubwa kwa Mkutano wa kwanza wa Ubinadamu Kimataifa utakaofanyika mjini Istanbul, Uturuki, mwezi Mei, 2016. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana ili kutafuta suluhu ya kudumu inayojikita katika hadhi, utu na heshima ya binadamu sanjari na kuwahudumia wahamiaji hawa kwa upendo na ukarimu. Makanisa na Jumuiya za waamini zinapaswa kuchangia kwa hali na mali, ushuhuda unaooneshwa na viongozi wakuu wa Makanisa wanaotembelea Kisiwani Lesvos, wanaotaka kuendeleza mchakato wa ushirikiano ili kukabiliana na changamoto hii ili iweze kuwa ni fursa ya kukuza utamaduni wa upendo badala ya kujenga kinzani na mipasuko ya kijamii.

Waamini wakumbuke daima kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao, ni Baba yao anayewapenda na kuwatakia mema. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, amejifanya kuwa mtumishi wa wote na kwa njia ya huduma ya upendo, ameikomboa dunia na kujenga amani, changamoto ya kuonesha upendo na mshikamano ili kuvuka utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, hali inayochefua akili na mioyo ya watu! Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza wananchi Kisiwani Lesvos kwa kuwa ni walinzi wa ubinadamu, kwa kutunza sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, ndugu zao wanaoteseka kwa njaa na utupu na wao wamewakirimia kwa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.