2016-04-16 12:05:00

Bahari ya Mediterrania lisiwe ni kaburi, bali chemchemi ya matumaini mapya!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox katika hotuba yake kwa wahamiaji na wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye Kambi ya Moria, Lesvos nchini Ugiriki, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 amewahakikishia wakimbizi hawa kwamba viongozi wa Makanisa wamefika kisiwani hapo ili kuwakumbusha kwamba, bado hawajasahaulika na kwamba, wanataka kuonesha mshikamano na ushirikiano kwa wananchi wa Ugiriki walionesha ukarimu na huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji tangu walipowasili visiwani humo!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema Mwenyezi Mungu ni kimbilio, nguvu na msaada wa watu wake na kamwe hawataogopa. Viongozi wa Makanisa wanatambua kwamba, hawa ni watu waliotoka katika maeneo ya vita, njaa na mateso makali na kwamba, wana machungu sana kuhusu familia zao. Hawa ni watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi.

Viongozi wa Makanisa wamehuzunika na kusikitika sana walipoona tumbo la Bahari ya Mediterrania linageuka kuwa ni kaburi la wakimbizi na wahamiaji. Wameshuhudia upendo na ukarimu wa wananchi wa Lesvos na visiwa vya jirani, lakini pia wameshuhudia mioyo migumu ya ndugu zao, wakifunga mipaka na kwenda zao bila kuguswa na mahangaiko ya jirani zao! Hawa ni watu ambao hawakuthubutu kuwaangalia machoni, nyuso wala watoto wao: ni watu ambao wamesahau utu na uhuru na matokeo yake wamemezwa na hofu pamoja na migawanyiko na kusahau kwamba, uhamiaji ni changamoto ya kimataifa!

Patriaki Bartomeo wa kwanza anakaza kusema, walimwengu watahukumiwa kwa jinsi ambavyo wamewatendea wakimbizi na wahamiaji na kwamba, watawajibika kwa jinsi wanavyoshughulikia migogoro, kinzani na vita katika maeneo wanamotoka wakimbizi na wahamiaji hawa. Bahari ya Mediterrania lisiwe ni kaburi ya watu, bali mahali pa maisha panapowakutanisha watu wa tamaduni na  staarabu mbali mbali; mahali pa kukutana na kujadiliana.

Bahari inapaswa kuwa ni mahali pa salama! Migogoro, kinzani na vita huko Mashariki ya Kati ni chanzo kikuu cha wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, amani na usalama vikirejeshwa huko, changamoto hii itakoma. Viongozi wa Makanisa wanasali ili haki za Wakristo na makundi ya watu wachache waendelee kukaa huko Mashariki na wala wasitoweke na kutoweka katika ramani ya dunia. Viongozi wa Makanisa wamewahakikishia wakimbizi na wahamiaji kwamba, kamwe hawatawasahu, wataendelea kuwatetea na kwamba, wataendeleza mchakato wa amani! Bara la Ulaya linapaswa kulitambua hili kuliko Mabara mengine yote, iko siku amani na utulivu vitarejea kati ya watu!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Jerome II, Mkuu wa Kanisa la Athens na Ugiriki nzima amesema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko utasaidia kuvuta hisia za Jumuiya ya Kimataifa ili kuaangalia na hatimaye, kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wakimbizi na wahamiaji. Viongozi wa Makanisa kwa kauli moja wana laani vikali vitendo vyote vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Uwepo wa viongozi hawa Kisiwani Lesvos uwe ni mwanzo wa mageuzi yatakayosaidia amani na usalama kwa wananchi wote. Wahusika wote wanaosababisha mateso haya wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha nyanyaso na dhuluma dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mateso na mahangaiko ya watoto wasiokuwa na hatia ni kielelezo cha kufilisika kwa utu na ubinadamu; mshikamano na upendo kutoka Barani Ulaya.

Askofu mkuu Jerome II anawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Ugiriki kwa kuonesha mshikamano wa huruma na upendo; kwa kusaidia kubeba Msalaba wa matumaini wakimbizi na wahamiaji wanaoelekea kwenye Mlimani Kalvari. Kanisa linaendelea kuwalilia wale wote wanaopoteza maisha kwa kufa maji baharini. Kanisa litaendelea kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kadiri ya uwezo wake na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa iwajibike kikamilifu katika kuwasaidia wahanga wa matukio haya. Ni matumaini ya Askofu mkuu Jerome II kutoona tena maiti za watoto wachanga zikielea kwenye ufuko wa bahari, bali watoto wakiwa na nyuso za furaha, huku wakifurahia zawadi ya maisha ya utotoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.