2016-04-15 16:24:00

Wajumbe wa Kanisa Anglikani wako Lusaka, Zambia kwa mkutano maalum!


Wawakilishi wa Baraza la Ushauri la Kanisa Anglikani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wameridhishwa na mchakato wa Kanisa Anglikani kwa katika mkutano wa kumi na sita wa Baraza la Ushauri la Kanisa Anglikani unaoendelea mjini Lusaka, huko Zambia. Wajumbe wanalipongeza Kanisa Anglikani kwa kujikita katika mchakato wa kuimarisha na kudumisha haki jamii miongoni mwa wanawake.

Haya yamesemwa na Padre Anthony T. Currer, afisa kutoka Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo anayeshughulikia mahusiano na Kanisa Anglikani. Mkutano huu ulizinduliwa rasmi tarehe 8 Aprili na utafungwa rasmi tarehe 19 Aprili 2016. Unahudhuriwa na Maaskofu, Mapadre na waamini walei kutoka Kanisa Anglikani. Wajumbe wamezungumzia masuala nyeti na tete katika maisha na utume wa Kanisa Anglikani, kwa kuwataka wajumbe kuwa na sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kabla ya kutoa maamuzi. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuendeleza majadiliano ya kiekumene hususan katika masuala ya haki jamii miongoni mwa wanawake.

Padre Currer anakaza kusema, mwaliko wa kushiriki na kuchangia mawazo katika mkutano huu, imekuwa ni fursa muhimu sana ya kuendelea kujenga na kuimarisha majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika moyo na huduma ya upendo na ukarimu. Wajumbe wanaendelea kujadili kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira na umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Majadiliano ya kiekumene kati ya Waanglikani na Waorthodox, mwaliko kwa waamini wa Makanisa haya kuwa mitume katika ulimwengu mamboleo na kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mkutano huu unaangalia pia maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri, yatakayofikia kilele chake kunako mwaka 2017. Wajumbe wanasikiliza pia taarifa ya Kanisa Anglikani, baada ya mkutano uliofanyika mwezi Januari kwenye Kanisa kuu la Canterbury, nchini Uingereza. Wajumbe wa Kanisa Anglikani kutoka Afrika wanajadili kuhusu kumfuasa Kristo Yes una kumtangaza katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.