2016-04-15 16:08:00

Jikiteni katika ushuhuda wa imani, ili kuwainjilisha walimwengu!


Familia ya Mungu nchini Poland inaadhimisha Jubilei ya miaka 1050 tangu Sakramenti ya Ubatizo ilipotolewa kwa mara ya kwanza nchini humo. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Kuchota kutoka katika yaliyopita, ili kujenga yajayo”. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya. Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Poland wanatumaini kwamba, maadhimisho haya yatasaidia kuleta mwamko mpya wa zawadi ya imani inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo.

Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, ili kuweza kuwashirikisha Wakristo wote zawadi ya imani, tayari kuiungama na kuishuhudia hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Kardinali Pietro Parolin, akiwa nchini Poland ameitaka familia ya Mungu nchini humo kujikita kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya Barani Ulaya, kutokana na Ulaya kuanza kumezwa mno na malimwengu.

Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland iwe ni fursa kwa Wakristo kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi; matumaini yanayosimikwa katika upya wa maisha ya imani. Ni tukio ambalo linapaswa kuimarisha utambulisho na mchango wa wananchi wa Poland katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu; kama ilivyokuwa kunako tarehe 14 Aprili 966, Poland ilipofungua ukurasa mpya wa Uinjilishaji na tangu wakati huo, imani ya Kikristo imeota mizizi na matunda yake yanaonekana katika maisha na utakatifu wa watu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambayo inapata chimbuko la ujumbe na changamoto zake kutoka kwa watakatifu Faustina Kowalska na Mtakatifu Yohane Paulo II; walioshuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya nyaraka zao, lakini zaidi kwa njia ya maishana utakatifu wao.

Viongozi wa Kanisa nchini Poland wanakaza kusema, maadhimisho haya yawe ni fursa ya kwa familia ya Mungu nchini humo kuendelea kukuza maisha na utume wa familia unaojikita katika ubinadamu na utu wema, chimbuko la tafakari ya kina kuhusu utakatifu wa Mungu unaojionesha katika utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maadhimisho haya yakuze na kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika maisha ya watu, kielelezo cha imani tendaji.

Baba Mtakatifu Francisko alikwisha kupewa mwaliko wa kushiriki maadhimisho haya na viongozi wa Serikali na Kanisa! Papa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, tarehe 28 Julai 2016 anatarajiwa kutembelea na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mjini Czestichowa, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo Poland. Familia ya Mungu nchini Poland inataka kumwilisha kwa vitendo, ile Kanuni ya Imani iliyotamkwa na Mfalme Mieszko wakati ule. Ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Poland yanategemea kwa kiasi kikubwa nguvu na ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake; kanuni maadili na utu wema, tayari kuambata Injili ya Kristo, dira na mwelekeo wa maisha adili na manyofu!

Kwa upande wake, Bwana Piotr Nowina- Konopka, Balozi wa Poland mjini Vatican anakaza kusema, maadhimisho haya ni muhimu sana katika mchakato wa kutafakari na hatimaye kumwilisha kanuni maadili na utu wema; ushirikiano na mshikamano kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Poland. Huu ni mwaliko wa kuendelea kujikita katika Mapokeo na tamaduni njema za watu wa Poland sanjari na kutekeleza changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Hapa, familia ya Mungu nchini Poland iwe ni mfano na kielelezo bora cha tunu msingi za maisha ya Kikristo. Wananchi wajenge na kushuhudia Injili ya upendo na huruma kwa maskini, wakimbizi, wahamiaji, wagonjwa na wenye shida mbali mbali. Waendelee kuchota kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni kisima cha ukweli, haki, wema na utakatifu, tayari kuwashirikisha jirani zao kama huduma ya huruma na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.