2016-04-15 15:52:00

Fedha isiwe ni sababu ya utumwa!


Sera endelevu za fedha na utunzaji bora wa mazingira mintarafu Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, Laudato si! Masuala ya fedha kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira, fedha na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 ni kati ya mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati akichangia mada kwenye mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na wadau mbali mbali wa mazingira nchini Italia na Ulaya katika ujumla wake!

Kardinali Turksona amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha, maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, mwanadamu anawajibika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kuwa na sera makini, shirikishi na zinazowajibisha katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ili kuondokana na ulaji usiokuwa na tija wala mashiko! Binadamu alinde na kudumisha mazingira kwa ajili ya mahitaji ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu kuhusu utunzaji bora wa mazingira ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, kumbe, hata sera na mikakati ya shughuli za fedha inapaswa kuwa na mwelekeo wa ujumla unaopania kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, fedha iwe ni kikolezo cha maendeleo na wala isimgeuze mwanadamu kuwa mtumwa wake. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni matokeo ya uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka unaojikita katika faida kubwa, huku mwanadamu na mahitaji yake msingi akisukumizwa pembezoni mwa jamii. Sera na shughuli za fedha zinapaswa kusimamiwa na kuongozwa na kanuni maadili na utu wema, mwanadamu akipewa kipaumbele cha pekee!

Kardinali Turkson anakaza kusema, kuna haja ya kuwa na elimu inayowawajibisha watu katika utunzaji bora wa mazingira; kwa kujikita katika mshikamano, umoja na udugu; daima mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza, ili haki, amani na maridhiano viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu! Vitega uchumi vizingatie amana ya maadili, ili kukuza amani, kulinda na kuendeleza mazingira. Vitega uchumi muafaka ni vile vinavyopania kuwaendeleza maskini, kupunguza hewa ya ukaa angani pamoja na kulinda mazingira.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa utunzaji bora wa mazingira anawataka watu kuwa ni watumishi na wahudumu bora wa mazingira nyumba ya wote; kulinda na kuendeleza Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu, ili kujenga ekeolojia inayobubujisha furaha katika maisha ya binadamu. Wachumi na wadau mbali mbali wa maendeleo wanapaswa kusaidia katika mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, kwa kupambana na umaskini, ili uweze kupewa kisogo; kwa kukuza na kudumisha uhuru, utu na heshima ya binadamu. Watu wajenge utamaduni wa kuwashirikishana bala ya kutengeneza kuta za utengano zenye madhara makubwa katika ustawi na maendeleo ya binadamu! Hii ni changamoto ya kulinda na kuheshimu haki msingi za binadamu kwa kuwapatia watu maisha bora zaidi! Katika mapambano dhidi ya umaskini, kuna haja kwa Makanisa kudumisha uekumene wa huduma na mapendo, ili kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.