2016-04-14 09:06:00

Sifa za mchungaji mwema!


Watu hukusanyika palipo na sikukuu, mhadhara, semina, kongamano, msiba, au penye upendeleo mmoja, kwani“Penye mzoga ndipo wanapokusanyika tai.” Linapoisha lengo la mkutano watu wanasambaratika. Kadhalika ukiona mifugo imetulia mahali ujue pana malisho na mchungaji ni mzuri. Kama malisho siyo mazuri na mchungaji mbaya hapo mifugo husambaratika. Dominika ya leo Wakristo wamekusanyika ili kusherekea Sikukuu ya mchungaji mwema. Jina sahihi lingepaswa kuwa dominika ya Mchungaji Mzuri. Mtu mwenye roho nzuri anajali, anaheshimu, anapenda, anakirimu na kusamehe. Yesu ni mchungaji mzuri kwa vile anawaongoza vizuri wale wanaomfuata. Kinachochangia uzuri wa Kristo ni kule kusamehe, kujali na hatimaye kutoa maisha yake kwa ajili ya wanyonge na wadhambi ili waonje huruma na upendo wa Mungu unaokoa na kufariji!

Leo Yesu anazungumza juu ya Mchungaji mzuri akiwa Hekaluni Yerusalemu tena katika sikukuu ya kukumbuka kutabarukiwa kwa Hekalu la Yerusalemu. Siku hiyo ya kutabaruku Hekalu iliitwa Sikukuu ya mwanga kwa lugha ya Kiyahudi ni Hanukkah na inasherekewa kwa muda wa siku nane mfululizo. Siku hiyo Waisraeli walisherekea kutakaswa kwa Hekaluni lao kwa sababu lilikuwa limechafuliwa au kunajisiwa na makafiri walipoiteka nchi yao. Wapagani hao wakaingiza na kuweka hekaluni humo sanamu ya mungu Zeus. Kwa bahati nzuri mwaka mia moja sitini na tano (165) Yuda Makabayo akaikomboa nchi na kuwarudishia tena Waisraeli uhuru wao. Kwa hiyo kabla ya kulitumia ilibidi kulitakasa yaani kulitabaruku upya hekalu. Wakatengeneza vinara nane vya taa kama vinara vya mshumaa tofauti na menora (vinara vitano vya wayaudi). Wakawa wanawasha kila siku kinara kimoja hadi siku nane.

Waisraeli walisherekea sikukuu hiyo ya mwanga ili kukumbuka kurudi kwa mwanga wa uwepo wa Mungu Hekaluni sababu mwanga ulizimika kutokana na kuchafuliwa na makafiri. Kwa hiyo Hanukka ilikuwa ni sikukuu ya mwanga na sikukuu ya kutabaruku hekalu kwa pamoja. Katika siku hizo nane Waisraeli walijichana kwa madiko diko na mapochopocho! kwa vyakula vya kukaangwa-kaangwa kwa mafuta kama vile bagia, maandazi, sambusa, vitumbua, chapati, mikate, nyama za kuku na vikorombwezo mbalimbali bila kusahau divai iliyokuwa inasaidia kulainisha koho na kusaidia vimeng’enya kufanya kazi yake barabara!

Baada ya kumponya mtu aliyezaliwa kipofu Yesu alisema: “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” (Yoh. 8:12). Kumbe, mwanga huo wa Mungu upo sasa katika nafsi ya Yesu aliye mwanga wa kweli wa ulimwengu anayefukuza giza la ubaya na dhambi. Yesu amekuja kutabaruku ulimwengu uliokuwa umenajisiwa na makafiri, waliomweka mungu wao zeus (mkuu wa miungu ya uwongo) watu wasio na huruma. Kwa hiyo leo kwa Wakristo ni dominika ya Hannukkah, yaani sikukuu ya ujio wa mwanga wa Kristo na ya kutabaruku ulimwengu.

Ama kweli Yesu ni mwanga unaomwongoza binadamu kwenye uzuri wa utu kweli, wa utumishi, wa upendo na wa kuhurumia wengine, changamoto kwa waamini kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni! Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kama tunapokea mapendekezo ya Yesu, hapo tutakuwa wazuri kwani tutapendana na kutumikiana kwani matendo ya huruma yanamwilishwa katika huduma ya mapendo, kielelezo cha Kristo mchungaji mzuri, aliyejinyenyekesha hata akathubutu kuwaosha mitume wake miguu, kazi iliyokuwa ikifanywa na watumwa. Wafuasi wa mchungaji mzuri wanatambulika kwa tabia moja wanayokuwa nayo. Tabia ya wafuasi wazuri hudhihirika katika matendo matatu yafuatayo:

Tendo la kwanza ni kusikia: Mchungaji mzuri anasema: “Kondoo wangu waisikia sauti yangu.” Katika biblia, neno kuu linalomanisha kusikia ni shema. “Sikiliza ee Israeli” (Kumb. 4:1). Kadhalika mzaburi anasema: “Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, masikio yangu umeyazibua” (Zab. 40:6). Hivi tabia ya kwanza ya kuwa katika kundi la kondoo ni kuzibua masikio na kusikia sauti ya mchungaji. Kuwa mfuasi wa Yesu hakutegemei kuwa kabila moja wala fikra moja, bali ni kuunganika pamoja na kusikia sauti ya mchungaji mzuri.

Kuna sauti nyingi potoshi, kama vile sauti za televisheni, za filamu, sauti za biashara, sauti za wote wenye maoni tofauti ya maisha nk, Kumbe sauti ya ukweli ya Mungu ni ile sauti ya upendo wa mchungaji mzuri. Hapa wafuasi wa Kristo wanahamasishwa kuachana na tabia ya kuchafua mazingira kwa makelele yasiyokuwa na tija wala mashiko! Lakini ikumbukwe kwamba, kusikiliza ni sanaa ambayo mtu anapaswa kujifunza ni utamaduni wa kuwa na moyo wa unyenyekevu, ili kuwa tayari kupokea kutoka kwa wengine! Pasi na sanaa ya kusikiliza, utakuwa ni mtu wa majungu!

Tendo la pili, ni kujua. Mchungaji mzuri anasema: “nami nawajua.” Katika Biblia kujua kunamaanisha ule umwandani wa watu wa ndoa, lakini siyo wa kujua kwa vionjo, bali ni ule wa kufahamu na kugundua uzuri wa mwingine na kuwa na mlengo mmoja, yaani wote tunamfuata kwa dhati Yesu mchungaji mzuri ili kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ushuhuda unaobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwamini baada ya kukutana na kuonja uwepo endelevu wa Yesu katika maisha yake!

Tendo la tatu, ni kufuata. Mchungaji mzuri anasema:“nao wanifuata” kama ilivyoandikwa: “naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” (Mdo 10:38).Kumfuata Yesu maana yake kumwiga Yesu katika mizunguko yake alipokuwa hapa duniani. Yatubidi tumwenzi kwa kuzunguka naye kutenda mema. Baada matendo haya matatu Yesu anawaambia wafuasi wake kuwa: “Wanaosikia sauti yangu wataokolewa. Hawatapotea kamwe.” Kukombolewa huko si kwa maisha ya hapa duniani, bali ni kuwa na maisha ya utu uliofanikiwa kama wa Yesu, yaani kuwa mtu huru aliyejikomboa.

Yesu mwenyewe anawaahidia wafuasi wanaofuata mambo yafuatayo: Mosi, Yesu mchungaji mzuri anaahidi: “Nami nitawapa uzima wa milele.” Siyo uzima wa kimwili bali atakuwa amefanikiwa na kujikomboa kwa milele, kwa kigiriki ni Zoen aionion - maisha yanayodumu yaani uzima wa Mungu. Kwa hiyo mchungaji mzuri anatoa maisha hayo kwa wanaochagua kufuata maisha yake kwa sababu Mungu  anataka furaha ya daima kwa kondoo wake wanaosikia na kufuata sauti yake.

Pili, Yesu mchugaji mzuri anaahidi na kusema: “Wala hawatapotea kamwe” Wapendanao hawawezi kuachana. Kwa hiyo mfuasi anayefuata sauti yake yuko katika mikono salama na hawezi kumpokonya. Katika kuhitimisha Yesu anarejea kwa Baba yake na kusema: “Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.” Mchungaji mzuri anawahakikishia kondoo waliokuwa mikononi mwake kwamba, wako pia mikononi mwa Baba yake. Yesu mchungaji mzuri anawachunga na kuwatetea kondoo wasiibiwe na sasa wako mikononi mwa baba. Aidha ili kuonesha uzito wa mshikamano wa utatu mtakatifu Yesu anahitimisha kwamba yeye na baba yake wanao mradi mmoja tu:“Mimi na Baba tu umoja.

Leo Yesu ametuomba ushirikiano wa kuishi kama yeye hapa duniani ili tujikomboa na kuishi kama watu huru ili kushiriki katika mchakato wa kuwakomboa wengine kwa kuwatendea matendo ya huruma, changamoto kubwa sana wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.