2016-04-14 10:17:00

Serikali ya Tanzania kulipa deni lake la ndani, lakini...!


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) , anafanya uhakiki wa madeni yanayodaiwa serikali na watumishi na kubaini madudu. Amesema madai mengine yameonyesha mashaka ambapo amewataka wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wakuu wa ndani kujiridhisha ukweli wa madai hayo kabla ya kuyafikisha serikalini kwa ajili ya malipo. “Madai mengine yanatia mashaka, sisi hatuhitaji kuletewa madeni ya hovyo hovyo ni vema Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wa ndani wakajiridhisha kabla kuyapeleka serikalini kwa ajili ya malipo. Madeni mengine ya ajabu, mfano unakuta mtumishi mmoja anaidai serikali sh. milioni 30,  jambo ambalo ni gumu hata kama alihamishwa haiwezekani kufikia kiwango hicho, pia kuna baadhi ya majina yamejirudia mara nne,” amesema.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa alipotembelea Hospitali hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukabidhi msaada wa vifaa tiba alivyovitoa kwa ajili ya hospitali hiyo. Amesema kuwa serikali italipa madeni yote inayodaiwa baada ya kumaliza kuyafanyia uhakiki, hivyo aliwaomba watumishi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea zoezi la kuyahakiki ili kuweza kulipa deni sahihi inalodaiwa.

Awali akisoma taarifa ya Idara ya afya kwa Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amesema idara ya afya inakabiliwa na madeni ya watumishi ambayo ni sh. milioni 109,662,483. Amesema madeni hayo yametokana na likizo, matibabu, uhamisho wa ndani na nje ya wilaya, gharama za mizigo kwa watumishi waliostaafu, ambapo  halmashauri imejipangia utaratibu wa kulipa madeni hayo pindi inapotokea fedha kutoka serikali kuu. Hata hivyo kasi ya mtiririko wa fedha ni ndogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya maslahi ya watumishi ambapo Halmashauri inawapongeza watumishi wa Idara ya afya kwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuwahudumia wananchi.

Dk. Simeo amesema halmashauri inawapongeza Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuongeza mapato nchini, ambapo wana matumaini kuwa watumishi wataboreshewa maslahi na stahiki zao ili kuchochea motisha kiutendaji. Katika hatua nyingine Dk. Simeo alizungumzia upatikanaji wa dawa, alisema ambao  umeongezeka kutoka asilimia 30 mwaka jana na kufikia asilimia 80 mwaka huu dawa muhimu katika vituo vyote vya kutolea huduma ambavyo viko 32.

Duka la dawa lajengwa katika ndani ya Hospitali ya wilaya ya Ruangwa

Waziri mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa ambalo  litatoa fursa kwa wilaya nyingine kama Kilwa, Nachingwea na Liwale kufuata dawa katika duka hilo. Ujenzi wa duka hilo la dawa ndani ya wilaya ya Ruangwa umefadhiliwa na Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD)  na unakadiriwa kugharimu sh milioni 55 mpaka kukamilika kwake ambapo kutasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa hospitalini hapo na katika hospitali zingine zilizoko katika wilaya za jirani. Waziri Mkuu, Majaliwa amesema mbali na ujenzi wa duka la dawa pia hospitali hiyo inatarajiwa kujengewa uzio ili kuepusha vitendo vya uhalifu vinavyoweza kutokea kutokana na hospitali hiyo kukosa uzio. Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa katika Hospitali hiyo.

“Nataka hapa ndio iwe bohari ya dawa, watu kutoka Kilwa, Nachingwea na Liwale wawe wanafuata dawa na vifaa tiba katika duka la dawa lililoko ndani ya Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, pia kujengwa kwa duka hili kutasaidia kumaliza tatizo la upungufu wa dawa,” amesema. Amesema mkakati uliokuwepo ni kuhakikisha vifaa tiba na dawa vinapatikana  hospitalini hapo ili kuwawezesha wagonjwa kupata huduma bora. “Kinachoniuma ni kuona akinamama, akinababa, vijana na wazee wangu wanakwenda hospitali na kuambiwa vipimo hakuna, hivyo nitahakikisha vifaa tiba vyote  vinapatikana,”.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amemshukuru Waziri Mkuu kwa juhudi mbalimbali anazozifanya ikiwemo kutafuta wafadhili mbalimbali wanaoendelea kusaidia utoaji wa huduma za afya hospitalini hapa. “Mpaka sasa kuna mradi wa ujenzi wa uzio wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa duka la dawa, ukarabati wa majengo na upanuzi wa hospitali na tunamuomba aendelee kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali yetu ya wilaya,” amesema. Dk. Simeo ameongeza kuwa kwa kupitia Waziri Mkuu, Majaliwa wameweza kupata vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi y ash. Milioni 100 kutoka umoja wa kampuni unaotengeneza vinywaji  baridi nchini ambavyo jana walikabidhiwa na Meneja wa MSD, kanda ya Mtwara, Helman Mng’ong’o.

Amesema licha ya kupata vifaa hivyo, pia walipokea vifaa tiba kutoka shirika la VSO vyenye thamani ya sh. milioni 32 ambavyo vitatumika katika kusaidia watoto waliozaliwa kabla umri haujatimia. Dk. Simeo alitaja vifaa tiba hivyo kuwa ni ni mashine ya kusaidia kupumua, mashine ya kusaidia kuhifadhi joto la mtoto, mashine nyingine ni za kusafishia watoto waliopaliwa na mashine ya kusaidia kujua kiwango cha hewa ya oxygen ndani ya mishipa ya damu ya watoto hao.

Mke wa Waziri Mkuu  atoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua

Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua. Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba  waendelee kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao. Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati alipotembelea wodi ya akinamama waliotoka kujifungua na kufurahishwa na hali ya utoaji huduma hospitalini hapo, ambapo  aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu wao ndio wamebeba dhamana ya afya za wananchi. “Nimefurahi kukuta wazazi wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba huduma zinazotolewa hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea kusikia wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia, hongereni sana” amesema.

Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye amelazwa katika wodi hiyo  amesema alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili zilizopita akiwa katika hali mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa anakaribia kutoka. “Mimi nilikuwa sijitambui, siwezi kufanya kitu chochote lakini baada ya kuletwa hospitalini hapa madaktari kwa kushirikiana na wauguzi wamenihudumia vizuri na sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe na bila msaada wao mimi ningekuwa nimepoteza maisha kutokana na hali yangu ilivyokuwa,” amesema Hamisa. Mbali na kutoa msaada huo wa mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya wanawake wawili walemavu lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli zao za kijamii kwa urahisi. Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke wa Waziri Mkuu kwa msaada huo, ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa awawezeshe kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na walemavu ikiwemo michezo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji kazi wa mazoea kwa sababu umepitwa na wakati. Pia amesema amefurahishwa  na kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa wanahudumiwa vizuri tofauti na hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari hiyo ya kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.

Ruangwa yatwaa ubingwa ligi mkoa wa Lindi: Majaliwa akabidhiwa kombe

Waziri mkuu  Kassim Majaliwa ameipongeza timu ya mpira wa miguu ya Namungo FC na kuikabidhi zawadi ya sh. milioni tano baada ya kuibuka mabingwa wa ligi daraja la tatu mkoa wa Lindi. Ubingwa huo wa mkoa ulionyakuliwa na timu ya wilaya ya Ruangwa, umeiwezesha kupanda daraja la pili taifa, hivyo kupata tiketi ya kushiriki  mashindano ya ligi daraja la pili mechi zitakazochezwa nyumbani na ugenini. Timu hiyo iliyoanzishwa na wafanyakazi wa mgodi wa Green Ganet uliopo Namungo, kijiji cha Chingumbwa wilayani Ruangwa  mwaka huu imekuwa mabingwa wa ligi daraja la tatu mkoa wa Lindi hivyo kupata tiketi ya kucheza ligi daraja la pili ngazi ya taifa.

Akipokea kombe hilo, Waziri Mkuu, Majaliwa amesema amefurahishwa na ubingwa huo, ambapo amewataka wadau wa soka wilayani hapa kuiunga mkono timu hiyo na kuhakikisha inapanda daraja na kucheza ligu kuu ya Tanzania bara. Pia amesema atafanya mazungumzo na halmashauri kuona kama wanaeneo kwa ajili ya kujenga kiwanja cha mpira wa miguu na litakapopatikana wananchi wanaweza kuanza kujenga mabanda ya biashara kuzunguka kiwanja hicho na kisha kutafuta mfadhili kwa ajili ya ujenzi wa eneo la kuchezea.

Kwa upande wake Shanel Nchimbi ambaye ni mmoja wa viongozi wa timu hiyo alimwomba Waziri Mkuu, Majaliwa kuisaidia timu hiyo katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya ukosefu wa kiwanja, vifaa vya michezo na vya huduma ya kwanza, usafiri na daktari. Nchimbi amesema changamoto ya ukosefu wa uwanja ilisababisha kuutumia uwanja wa michezo wa Sokoine wa wilaya ya Nachingwea kuwa wa nyumbani hivyo kusababisha timu hiyo kutumia gharama kubwa kufika eneo la michezo.

MWISHO

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu. 








All the contents on this site are copyrighted ©.