2016-04-14 16:33:00

Papa Francisko Kisiwani Lesvos, Ugiriki!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Aprili 2016 anafanya hija yake ya kitume ya kumi na tatu kimataifa kwa kutembelea Kisiwa cha Lesvos, kilichoko nchini Ugiriki, huu ni mwendelezo wa mshikamano wa huruma na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji; maskini na wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na sababu mbali mbali. Huu ni mwendelezo wa hija za kitume ambazo Baba Mtakatifu Francisko amefanya huko Tirana, Albania, Uturuki, Sarayevo, Bosnia na Erzegovina na Jumuiya ya Ulaya.

Baba Mtakatifu anatembelea Kisiwa cha Lesvos ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wakimbizi na wahamiaji walioguswa na kutikiswa katika utu na heshima yao! Ni hija ya kitume inayopania pia kuimarisha mshikamano wa kiekumene katika mchakato wa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji, kwani Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume, ataambatana na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na viongozi wa Makanisa ya Kikristo nchini Ugiriki.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika hija yake ya kitume huko Lesvos. Huu ni ufafanuzi ambao umetolewa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican wakati akifafanua hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kisiwani Lesvos. Hii ni hija ya kiutu na kiekumene, itakayomwezesha Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Makanisa nchini Ugiriki. Atapata nafasi ya kusali. Kwa pamoja watawatembelea wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaoomba hifadhi ya kisiasa, ambao kwa sasa wanafikia jumla ya watu 2500.

Viongozi wa kidini watasalimiana na wakimbizi na wahamiaji hawa mmoja mmoja ili kuonesha na kushuhudia uwepo wa karibu wa Kanisa katika shida na mahangaiko ya watu hawa! Viongozi wa Makanisa wataweka sahihi katika tamko la pamoja linaloyawajibisha Makanisa katika huduma ya kiekumene! Wakimbizi na wahamiaji 14 watapata chakula cha pamoja na viongozi wa Makanisa.

Baba Mtakatifu Francisko atapata pia nafasi ya kuzungumza, kusali na kuwakumbuka wahanga wa uhamiaji, wanaoendelea kufa maji, kunyanyasika na kudhulumiwa, wakati wakiwa njiani kutafuta hifadhi na usalama wa maisha. Hii ni hija ya mshikamano, huruma na upendo kwa watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.