2016-04-14 16:21:00

Iweni wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 14 Aprili 2016 amewataka Wakristo kuonesha unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kusonga mbele katika mchakato wa Uinjilishaji na wala si uaminifu kwa sheria kama wanavyodhani wengi. Neema ya Roho Mtakatifu itawawezesha wakristo kuwa ni mashuhuda na Wainjilishaji wenye mvuto na mashiko kama ilivyokuwa kwa Filipo aliyemwinjilisha mtu wa Kushi, towashi, aliyekuwa na Mamlaka chini ya Kandake Malkia wa Kushi.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, hapa mhusika mkuu si Filipo wala yule Towashi aliyehubiriwa Neno la Mungu, bali Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kuchipua na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Katika historia, kuna wakati watu walijikuta wakipingana na Roho Mtakatifu kwa kuwa na nyoyo zilizokunjamana na kusinyaa kama kigae, kiasi kwamba, baadhi ya watu wakashindwa kuona miujiza iliyokuwa inatendwa na Mitume wa Yesu; Ushuhuda uliokuwa unatolewa na Shemasi Stefano, Shahidi; yote haya wazee wa Sinagogi waliyafanya kwa kujificha chini ya mwamvuli wa kuwa waaminifu kwa sheria.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii Kanisa linawahamasisha Wakristo kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuliumba na kuliwezesha Kanisa kusonga mbele. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu wahubiri kama Filipo wanaweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, jambo la msingi ni utii kwa Roho Mtakatifu pamoja na Habari Njema ya Wokovu. Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi katika nyoyo za watu kama ilivyokuwa kwa yule Towashi wa Kushi, ambaye hatimaye, aliomba kubatizwa na kuambata imani kwa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu alipandikiza mbegu ya udadisi kwa Towashi wa Kushi, kiasi hata cha kuweza kuambata imani kwa Kristo Yesu, na hatimaye, kubatizwa na hivyo kuonja furaha ya kuwa mnyenyekevu kwa Roho Mtakatifu na kwamba, fadhila hii ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha ya mwamini. Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu ndiye anayeliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini, changamoto kwa waamini kuwa makini kusikiliza sauti ya Mungu anayewaita ili waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Ili kuweza kusikiliza sauti ya Mungu, mwamini anapaswa kuonesha fadhila ya usikivu! Pale waamini wanapokuwa na mashaka katika maisha, wafungue mioyo yao tayari kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu inayozungumza ndani mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.