2016-04-14 07:58:00

Hali ya wakimbizi na wahamiaji ni tete sana!


Askofu Fragkiskos Papamanolis, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ugiriki anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko Kisiwani Lesvos ni kielelezo na ushuhuda wa ukaribu na mshikamano wa Baba Mtakatifu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kisiwani hapo. Wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani huu ni umati mkubwa watu unaosafiri kutafuta hifadhi na usalama wa maisha.

Wimbi hili lilianza kujiotokeza kunako mwaka 2015, wengi wao wakiwa wanaitwa wahamiaji haramu. Idadi yao ikaendelea kuongezeka maradufu, leo hii kuna umati mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi wasiokuwa na nyaraka za kusafiria, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Tangu mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa upendo kwa kuwapatia hifadhi baadhi ya wahamiaji hao nchini Ugiriki. Lakini, idadi ya wakimbizi na wahamiaji imeongezeka maradufu kiasi hata cha kuwazidi wenyeji wao. Hapa Kanisa na Serikali vikashikamana kuwasaidia watu hawa, lakini idadi yao ilikuwa ni kubwa kulinganisha na uwezo wa Serikali na Kanisa kutoa huduma makini! Katika siku za hivi karibuni, Kanisa limeendelea kutoa msaada kadiri ya uwezo wake anasema Askofu Papamanolis, ili kuwasaidia wakimbizi waliokuwa wanakabiliwa na mazingira magumu na hatarishi.

Takwimu za Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Ugiriki zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 150, 000 ambao wameingia nchini humo tangu mwanzo wa Mwaka 2016. Kati yao asilimia 38% ni watoto wadogo; asilimia 21% ni wanawake na asilimia 41% ni wanaume. Baada ya Jumuiya ya Ulaya kufunga mipaka yake, zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 50, 000 wamejikuta wakiwa wamebaki nchini Ugiriki. Caritas inaendelea kutoa msaada wa chakula na afya! Jitihada hizi zinaungwa mkono na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kitaifa na kimataifa.

Askofu Papamanolis anasema tangu tarehe 18 Machi 2016, Serikali ya Uturuki ilipowekeana mkataba na Jumuiya ya Ulaya, mahusiano kati ya wananchi wa Uturuki na wahamiaji pamoja na wakimbizi yamebadilika sana; kwani hawa si tena wahamiaji haramu bali ni wafungwa ambao amekataa kufukuzwa kutoka Ugiriki na hawataki kurudi nchini Uturuki. Katika mwelekeo huu, hali ya ulinzi na usalama; haki, amani na utulivu ni tete sana. Hali ya uchumi imeendelea kuwa mbaya kwani watalaii wamesusia kutembelea huko Ugiriki. Hali hii pia imelitendea Kanisa kwani limelazimika kufunga baadhi ya huduma za kijamii zinazotolewa na Kanisa kwa kukosa rasilimali fedha!

Kutokana na mwelekeo huu, hata wenyeji wameanza kuwa na wasi wasi wa usalama wa maisha na mali zao; kwa sasa anasema Askofu Papamanolis, baadhi yao wameanza kununua silaha za kujihami; upendo na ukarimu vinaanza kuyeyuka pole pole kutokana na vurugu zinazotishia maisha ya watu Visiwani hapo. Kumbe, hija ya Baba Mtakatifu Kisiwani Lesvos ni muhimu sana katika kujenga mshikamano wa upendo na huruma kwa wakimbizi na wahamiaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.