2016-04-13 16:13:00

Vijiji 42 Wilayani Ruangwa kupatiwa umeme!


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema vijiji 42 vya wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa umeme katika Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu. Amesema hadi sasa tayari vijiji 48 vya wilaya hiyo vimeunganishiwa umeme na kwamba lengo lake ni kuhakikisha vijiji vyote 90 vinapata huduma hiyo, hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na subira.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo tarehe 12 Aprili 2016 alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Michenga, Chinongwe, Makanjiro na Chinokole katika mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa. “Niliwaahidi kuwatumikia, kuwahudumia na kuwasemea ndani na nje ya nchi, nawahakikishia kuwa sitowaangusha hivyo endeleeni kuwa na subira, nitafanya mambo mengi ya maendeleo kama isemavyo kauli mbiu yangu, Ruangwa kwa maendeleo inawezekana.” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi, Sotco Nombo amesema tarehe 15 mwezi huu wataanza kusambaza vifaa katika kijiji cha Chinongwe na kwamba hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu umeme utakuwa umewaka katika kijiji hicho.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Majaliwa amewasisitiza wananchi kuanza kulima kwa wingi zao la muhogo kwa sababu kuna soko la uhahika la zao hilo baada ya kujitokeza kwa wafanyabiashara kutoka China na Marekani wanaotaka kununua zao la mihogo kutoka nchini Tanzania “Mnataka hela, mnataka hela? ila lazima mfanye kazi…mimi nimewatafutia hela nawaomba mlime mihogo kwa wingi maana kuna wafanyabiashara wanataka kununua mihogo, hela ndiyo hiyo ambayo ni soko la uhakika la mihogo. Nawasihi mchangamkie dili hili,” amesema.

Amesema wafanyabiashara hao wanataka kununua mihogo kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale kwa ajili ya kusaga unga na kutengeneza vyakula vingine vitokanavyo na zao hilo, hivyo amewaomba wananchi hao kuchangamkia fursa hiyo na kulima mashamba makubwa ya mihogo.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kufuatilia maendeleo ya mradi wa umwagiliaji wa Narunyu katika kata ya Kiwalala wilayani Lindi. Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa kata hiyo kusimamisha msafara wa Waziri Mkuu, Majaliwa katika eneo la Kiwalala tarehe 12 Aprili 2016 na kumwomba awasaidie kuhusu hatma ya mradi wao wa umwagiliaji ambao walitakiwa wakabidhiwe tangu mwaka 2014.

Awali mwakilishi wa wananchi hao, Mohammed Bakar alisema kuwa mradi huo uliogarimu shilingi milioni 600 ulitakiwa uwe tayari umekabidhiwa kwa wananchi, lakini hadi sasa bado na hata banio halijakamilika, hivyo wanashindwa kuendelea na kilimo katika eneo hilo. “Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu bado haujaanza ila tulishangaa wakati wa mbio za Mwenge mwaka 2014 ilisomwa taarifa kwamba wakazi wa Kiwalala wananufaika na mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Narunyu jambo ambalo si kweli kwani mradi huu haujawahi kufanya kazi na hata banio hakuna,” amesema.

Waziri Mkuu, Majaliwa amesema malalamiko hayo ya wananchi wa Kiwalala lazima yafanyiwe kazi, hivyo amemuagiza mkuu wa mkoa wa Lindi, Zambi kuhakikisha anakwenda kwenye kata hiyo kulipatia ufumbuzi suala hilo. “Kweli kuna miradi ambayo inaelekezwa na watu kwa viongozi kuwa imekamilika wakati bado, namuagiza mkuu wa mkoa kulifanyia kazi jambo hili,” amesema. Pia amesisitiza kwamba serikali hii si ya kuleana, mtu atakayebainika kukwamisha miradi ya maendeleo watamalizana naye hapo hapo, hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira kwani taarifa yao imepokelewa na inafanyiwa kazi.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo, Zambi amesema tayari ameshapata taarifa za tatizo la mradi huo na kwamba atafanya ziara kwenye eneo hilo na mtu atakayebainika kutafuna fedha za mradi huo atamwajibisha hapo hapo kwa sababu yeye hataki kutumbuliwa kwani Serikali ya Dr. Magufuli haina mchezo wala mzaha katika masuala ya haki, nidhamu na uwajibikaji!

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.