2016-04-13 15:50:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kuombea Miito ndani ya Kanisa!


Dominika ya nne ya Pasaka huitwa Donimika ya Kristo Mchungaji mwema. Hili ni adhimimisho ambalo linatupatia nafasi ya kumtafakari Kristo kama Mchungaji mwema ambaye anajiweka tayari na kujitoa katika hali zote kwa ajili ya ustawi wa kundi lake. Kwa namna hiyo Kristo anakuwa kielelezo kwetu cha uwajibikaji wetu katika miito mbalimbali ambayo Mungu ametuitia kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu. Ndiyo maana pia , Dominika hii ni maalum kwa ajili ya miito, pale ambapo Kanisa zima huitwa kwa ajili ya kuiombea miito. Mwenyezi Mungu anamuita kila mmoja wetu katika wito maalum kusudi kila mmoja anapotenda kwa ufanisi jamii nzima inapata fanaka. Nafasi uliyonayo katika jamii si kwa ajili ya ubinafsi wako bali ni kwa ajili ya kuufunua upendo wa Mungu na kumfanya mwanadamu aendelee kuionja huruma yake.

Somo la kwanza katika Dominika hii linatuonesha wito ambao Mungu ametupatia: “Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata miisho ya dunia”. Nuru hiyo tunayopaswa kuiangaza ni Kristo Mfufuka aliye nuru yetu, Yeye ambaye kwa nuru hiyo amelifukuza giza  la dhambi. Tunaitwa kuwa nuru kwa watu wengine na kwa njia hiyo kuwa sababu ya wokovu kwao. Tunapowaangazia wengine ndipo tunapowapa fursa ya kuionja huruma ya Mungu. Kristo anatuambia kwamba: “nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mt 5:16). Tunapoalikwa kushuhudia Ufufuko wa Kristo kwa maisha yetu ndipo tunapoitwa kuwa nuru daima. Huku ni kuendelea kuufanya mshumaa wa Pasaka, Mwanga wa Kristo uendelee kutumulika daima.

Utumishi wetu uliotukuka hudumisha ustawi wa kondoo tunaokabidhiwa na kwa hakika husikia sauti yetu. Injili ya Dominika hii inatufunulia utumishi huo kupitia Mchungaji wetu Mkuu Yesu Kristo. “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu”. Matendo haya ya kusikilizwa, kufahamika na kufuatwa na wale tunaowahudumia huambatana na huduma zetu zinazowauhisha, zinazowalinda na kuwaongoza.

Tunaalikwa kuwahuisha wenzetu kwa kufanya utumishi wetu kuzaa matunda na kuiendeleza jumuiya ya mwanadamu. Tunapaswa kujihoji mara nyingi ni kwa jinsi gani huduma yangu inaneemesha jumuiya inayonitegemea. Hapo ndipo tunaweza kujiona kwamba tunawalinda na kuwaongoza wote. Kila mmoja wetu mahali popote anapokuwa, iwe ni ndani ya maisha ya familia, iwe katika jumuiya ya Kanisa, iwe katika jamii ya kisiasa, iwe katika jamii ya kiuchumi na pengine popote aupokee wajibu anaopewa na kuutenda mithili ya Kristo Mchungaji Mwema.

Mchungaji anayejijali mwenyewe daima atatafuta kwanza maslahi yake. Huu ndiyo utendaji unaoonekana katika nyanja mbalimbali za maisha katika jamii ya mwanadamu wa leo. Tunapewa changamoto leo hii: Ni kwa nini umepokea kwa furaha jukumu lililo mbele yako? Ni ipi iliyo furaha ya mwalimu kama si kumuona mwanafunzi wake anafaulu na kutatua changamoto mbalimbali za maisha? Tabibu kwa upande wake anafurahia nini kama si kumona mgonjwa wake amepata nafuu? Muelekeo huo ndiyo utatuwezesha kuutimiza kiamifu wito tunaopewa na Mungu wa kuwa “nuru ya mataifa upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia”. Dominika iliyopita tulisisitiziwa sana kuweka usikivu wetu kwa Mungu na si kwa mwanadamu.

Leo hii wengi wetu wanashindwa kutimiza sawasawa nyajibu zao sababu tu wamegeuza masikio yao na kumsikiliza mwanadamu na wala si Mungu. Katika mazingira ya jamii ya kisekulari, jamii ambayo ndiyo inatuzunguka leo ni aghalabu kuuona huo upendo wa kimungu. Daima tunagubikwa na furaha za kidunia ambazo hudumu kwa kitambo tu. Tunapaswa kuamka. Tumepewa kipindi cha neema katika mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu katika kuuona huo upendo na huruma ya Mungu. Huruma hiyo na upendo huo asili yake ni Mungu mwenyewe na unafunuliwa kwetu kwa njia ya Kanisa.

Katika ujumbe wake kwa siku hii ya kuitafakari miito yetu mbalimbali, Baba Mtakatifu Francisko anatuambia kwamba “Kanisa ndilo Mama ya miito yote”. Hii inamaanisha kwamba nyajibu zote zinapaswa kuzaliwa ndani ya Kanisa, yaani katika fumbo la Mwili wa Kristo. Baba Mtakatifu anaendelea kusema: “Ni matumaini yangu makubwa kwamba katika kuendelea na mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, wabatizwa wote waionje furaha ya kuwa wanakanisa na kugundua kwamba wito wa kikristo, kama ulivyo wito wowote mahsusi, huzaliwa kutoka ndani ya maisha ya waana wa Mungu na ni zawadi ya huruma ya Mungu. Kanisa ni nyumba ya huruma na udongo ambao miito hupata mizizi, hukomaa na kuzaa matunda ... tendo la huruma la Bwana husamehe dhambi zetu na hutufunulia maisha mapya ambayo hupata maana katika wito wa utume na misioni. Asili ya kila wito ndani ya Kanisa ipo katika jicho la huruma la Yesu”.

Baba Mtakatifu Fransisko namalizia ujumbe wake huo kwa kusema kwamba miito yote huanzia, kukua na kuwezeshwa ndani ya Kanisa. Huu ni mwongozo muhimu sana wa namna ya kuitikia na kuitekeleza miito yetu, yaani kutokea ndani ya Kanisa. Kitabu cha Ufunuo kimetuambia kwamba: “Hao ndiyo wanaotoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo ... wanamtumikia mchana na usiku ... hawataona njaa, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.” Hivyo hatuna sababu ya kukata tama wala kuvunjwa moyo na ukinzani wa kidunia. Tunapaswa kutambua kwamba kile tunachokifanya ni kutoka kwa Mungu na ni kwa ajili ya kuustawisha utawala wake kati yetu.

Ni muhimu kuiona nafasi ya Kanisa katika kutuelekeza kwa njia ya mafundisho yake na miongozo yake namna ya kutimiza nyajibu zetu. Lakini pia tusiusahau umuhimu wa Kanisa kupitia utajiri wake wa matakatifu na uwezo wake wa kutugawia sisi. Hizi ni Sakramenti, kwa namna ya pekee Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu, Sakramenti zinazotuonjesha daima upendo na huruma ya Mungu, lakini pia baraka mbalimbali na maombezi ambayo Kanisa huziadhimisha kwa ajili ya ustawi wa watu wake. Tunapoanza kufikiri kwamba nafasi ya huduma unayopewa imetokana na vipawa vyako an uwezo wako binafsi hapo ndipo utaingia katika janga la kumtenga Mwenyezi Mungu na matokeo yake ni kujifanyika kama unavyoona inafaa wewe na mwishowe ni kuingia katika ubinafsi, chuki, magomvi na maovu mengine yanayotutenga. Katika hali hii ni vigumu kuutimiza wito wetu na hata kuwa nuru na wokovu kwa wenzetu.

Dominika hii ya Kristo Mchungaji mwema iwe chachu kwetu na kwa namna ya pekee katika mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ni kwa huruma yake kuu kwetu Kristo amekuwa Mchungaji wetu mwema. Leo anakualika nawe pia kuwa chombo cha kuieneza hiyo huruma yake kwa watu wote. Amekuweka kuwa nuru ya mataifa ili upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Kumbuka daima kwamba huduma yako ina asili toka kwake na hivyo jishikamanishe naye, jiloweke katika damu yake inayotakasa na kutia nguvu na mwisho muombe yeye akuongoze na kukutia nguvu. Daima tusisahau kuiombea miito ndani ya Kanisa kusudi wote waitikie na kutumikia mithili ya Kristo Mchungaji mwema.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.