2016-04-13 15:14:00

Mshikamano wa huruma na mapendo kwa wakimbizi!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Frabcisko kisiwani Lesvos, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016 ni kutaka kuonesha mshikamano wa huruma na mapendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na mahangaiko ya watu. Hii ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kusutwa na dhamiri nyofu, tayari kushikamana kwa dhati ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji ili kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana.

Baba Mtakatifu Francisko daima amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee kwa shida na mahangaiko ya maskini, wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni watu ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, dhuluma, nyanyaso, ukosefu wa haki msingi za binadamu, umaskini na hata wakati mwingine wanatafuta usalama na hali bora zaidi ya maisha. Watu wana haki ya kubaki katika makazi na nchi zao, ikiwa kama kuna usalama, amani, utulivu na vichocheo vya maendeleo endelevu, vinginevyo, watu wanalazimika kuyakimbia makazi yao.

Ili kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu anasema Kardinali Turkson, kuna haja ya Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa diplomasia ya amani, urafiki, upendo, haki, umoja na udugu; mambo msingi ambayo wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuonjeshwa katika shida na mahangaiko yao ya kila siku! Ugiriki imeonesha ukarimu mkubwa kwa wahamiaji na wakimbizi na kwamba, kwa siku za hivi karibuni imepokea msaada mkubwa wa fedha kutoka katika Jumuiya ya Ulaya!

Jambo la kujiuliza, Je, huu msaada unaotolewa wakati huu ni kwa mafao ya nani zaidi? Kuna haja ya kujenga na kudumisha mchakato wa amani na utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi; haki na amani kati ya watu. Hapa kuna mchezo mchafu unaoendelea huko Mashariki ya Kati, kwani kuna mataifa yanayotaka kufaidika zaidi kutokana na vita, kinzani na migogoro!

Kardinali Turkson anasema, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa ajili ya mafao ya wengi. Ekolojia ya binadamu, ipewe pia kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii, kwa kuheshimu na kuthamini Injili ya uhai inayojikita katika Injili ya familia na huruma ya Mungu kwa binadamu na upendo kwa jirani. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kuguswa na utu wa watu, ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na kwamba, maendeleo endelevu yanafumbata mambo mengi katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.