2016-04-13 09:35:00

Kisiki cha tambiko kimeng'oka; Babu Isuja kapumzika kwa amani!


Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma, imepigwa na simanzi kubwa kutokana na msiba wa Askofu mstaafu Mathias Isuja Joseph wa Jimbo Kuu la Dodoma uliotokea alfajiri ya tarehe 13 Aprili 2016 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Itigi, Singida, Tanzania alikokuwa amelazwa kwa matibabu zaidi. Askofu mstaafu Isuja, wengi walizoea kumwita “Babu”, “Mnyakaya” “Mng’atuka” amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86 ya kuzaliwa; miaka 55 ya huduma ya Upadre na miaka 43 ya Uaskofu kwa kubahatika kuona Jimbo Katoliki Dodoma lizaa Jimbo Katoliki la Kondoa na hatimaye, kupandishwa hadhi kuwa Jimbo kuu la Dodoma! Si haba, kweli “Mnyakaya amelala katika usingizi wa amani! marehemu Askofu Mathias Isuja Josefu anatarajiwa kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma, Jumatano tarehe 20 Aprili 2016.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mstaafu Mathias Isuja Joseph alizaliwa kunako tarehe 14 Agosti 1929, Parokiani Haubi, Kondoa, Jimbo Katoliki la Kondoa kwa sasa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kunako tarehe 24 Desemba 1960 akapewa Daraja Takatifu la Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Dodoma. Tarehe 26 Juni 1972 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Dodoma na kuwekwa wakfu tarehe 17 Septemba 1972 na Kardinali Laurian Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, akisaidiwa na Askofu mkuu Marko Mihayo wa Jimbo kuu la Tabora pamoja na Askofu Adrian Mkoba wa Jimbo Katoliki Morogoro. Tarehe 15 Januari 2005 akang’atuka kutoka madarakani! Na tarehe 13 Aprili 2016 amefariki dunia huko Itigi, Singida, Tanzania.

Taarifa rasmi kutoka kwa Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu la Dodoma inasema, Askofu mstaafu Isuja alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ta Mtakatifu Gaspari, Itigi kwa muda wa juma moja baada ya hali yake kudhohofu kutokana na ugonjwa wa Saratani ya utumbo. Hayati Askofu Isuja atakumbukwa na wengi kutokana na moyo wake wa huruma kwa yatima, walemavu na wagonjwa. Pengine, Jimbo kuu la Dodoma ni kati ya Majimbo Katoliki yenye vituo vingi vya huduma kwa ajili ya watoto yatima, walemavu na wagonjwa nchini Tanzania. Askofu Isuja alionesha moyo wa upendo na ubaba kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Dodoma. Hata katika uzee wake, bado aliendelea kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Dodoma. Aliendelea kutoa huduma Parokiani na Vigangoni kama Kuhani, kielelezo cha sadaka na majitoleo kwa Mungu na jirani hadi dakika ya mwisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.