2016-04-13 14:57:00

Hata wadhambi wanaweza kula pamoja na Yesu!


Nataka rehema, wala si sadaka ndiyo sehemu ya Neno la Mungu iliyoongoza katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 13 Aprili 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni sehemu ya Injili inayomwonesha Yesu Kristo akitoa mwaliko kwa Mathayo mtoza ushuru, mdhambi machoni pa wengi; anayekubali wito na hatimaye kuamua kumfuasa Yesu na hivyo kuwa ni kati ya mitume wake! Mathayo mtoza ushuru alithubu hata kumwalika Yesu na mitume wake nyumbani kwake ili kujipatia chakula!

Na hapa anasema Baba Mtakatifu zogo likazuka kwa kumshutumu Yesu kwa kula na kushirikiana na wadhambi! Lakini Yesu alilenga mbali zaidi kwa kutoa nafasi kwa mdhambi ili kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza kuandika ukurasa wa maisha mapya kwa kuitia wito kwa moyo wa unyenyekevu na ukweli! Kanisa ni Jumuiya ya wafuasi wa Kristo ambao wako kwenye hija ya kumfuasa Kristo kwa kutambua udhaifu na mapungufu yao na kwamba, wanahitaji kuonjeshwa huruma na msamaha kwani maisha ya Kikristo ni shule ya unyenyekevu inayojikita katika neema!

Baba Mtakatifu anasema, Yesu alichukua fursa ya wito wa Mathayo kufafanua kwa kina na mapana kwamba, amekuja hapa duniani si kwa ajili ya kuwaita wenye haki na watakatifu, bali wadhambi, tayari kutubu na kumwongokea Mungu. Yesu anawaalika wafuasi wake kuketi pamoja naye mezani, ili kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalowatakasa kwa njia ya Neno la Mungu na kuwaunganisha zaidi pamoja na Kristo katika hija ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anataka rehema na wala si sadaka; anataka toba na wongofu wa ndani badala ya maneno na ibada zisizogusa undani wa maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuungama dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, ili kuitikia kwa moyo wa ukarimu mwaliko wa kuweza kukaa pamoja na Yesu mezani pamoja na jirani, ili kuonesha na kushuhudia moyo wa shukrani kwa huruma na upendo wake unaookoa! Waamini waendelee kujifunza kutoka kwa Kristo maana ya rehema, ili kumtambua na hatimaye, kushirikiana na Yesu kama rafiki. Wakristo waache tabia ya kujiona kuwa wao ni wema na watakatifu zaidi na badala yake, watambue kwamba wao bado ni wafuasi wa Kristo na wadhambi wanaopaswa kuguswa na kuponywa na huruma ya Mungu. Iwe ni fursa ya kuwatambua na kuwathamini jirani zao katika hija ya maisha yao ya kiroho.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini, mahujaji na wageni kutoka Poland kwamba, wakati huu Kanisa nchini Poland linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka  elfu moja na hamsini tangu Sakramenti ya Ubatizo ilipotolewa kwa mara ya kwanza nchini Poland. Hili ni tukio la kumshukuru Mungu kwani katika historia ya miaka hii yote, imesaidia mchakato wa kuwafunda watu wa Poland: imani, tasaufi na tamaduni kama Jumuiya ya wakristo sanjari na kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Huu ni wakati muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II kwani wamebatizwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na maji, ili kuboresha ile sura ya Mungu aliye hai kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu nchini Poland kuendelea kua aminifu kwa neema ya Ubatizo kwa kushuhudia upendo kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili Ijayo, tarehe 17 Aprili 2016, maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema, Kanisa linaadhimisha Jumapili ya 53 ya Kuombea Miito Duniani. Iwe ni fursa kwa waamini kumwomba Yesu, Mchungaji mwema, aweze kutuma watendakazi wapya katika shamba lake. Anawaalika waamini kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanatekeleza masharti yote ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ili kujipatia rehema kamili inayotolewa na Mama Kanisa kwa ajili  yao wenyewe, ndugu, jamaa na marafiki!

Mwishoni mwa Katekesi yake Baba Mtakatifu Francisko amesema, Jumamosi tarehe 16 Aprili 2016 anatarajiwa kutembelea Kisiwa cha Lesvos, kilichoko nchini Ugiriki. Akiwa Kisiwani hapo, atajiunga na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Askofu mkuu Jerome II wa Kanisa la Athens na Ugiriki nzima kukutana na kuzungumza na wakimbizi wanaohifadhiwa Kisiwani hapo Serikali ya Ugiriki imeonesha ukarimu wa pekee kwa wakimbizi na wahamiaji! Lengo ni kuonesha mshikamano wa upendo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika hija hii ya kitume kwa sala na sadaka yao, kwa kuomba mwanga na nguvu za Roho Mtakatifu, sala, maombezi na tunza ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.