2016-04-12 11:50:00

Dhuluma ni chakula cha kila siku cha Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 12 Aprili 2016 amesema, madhulumu dhidi ya Kanisa ni chakula cha kila siku, kama ilivyotokea kwa Stefano shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; watoto wadogo waliouwawa na Mfalme Herode kwa hofu ya kuzaliwa  kwa Masiha na kwamba, hata leo hii kuna maelfu ya Wakristo wanaoteswa na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna madhulumu ambayo yanaendelea kusabisha vifo kwa watu wasiokuwa na hatia! Kuna watu wanatumia mabomu ya kujitosa, ili kusababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha, pengine wakati wakiwa wanatoka Kanisani. Dhuluma na nyanyaso zinazofanyika katika hali ya kificho na usiri mkubwa! Kuna dhuluma inayoendeshwa katika tamaduni kwa kuwatenga Wakristo kutoka katika maisha ya hadhara au hata kunyimwa fursa ya ajira, kwa vile tu ni Wakristo!

Baba Mtakatifu anasema, simulizi la kifodini cha Stefano, shahidi kilichotokea takribani miaka elfu mbili iliyopita si dhana ya kufikirika, lakini huu ni ukweli, kama ilivyokuwa kwa Wakristo kutupwa kwenye Magofu ya Colosseo ili kupambana na wanyama wakali! Leo hii Colosseo imekuwa ni eneo maarufu sana la kitalii, lakini hapa kuna Wakristo wa nyakati mbali mbali wameshuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa kuyamimina maisha pasi na utani!

Hivi ndivyo ilivyotokea nchini Pakistan wakati wa Siku kuu ya Pasaka mwaka huu, Wakristo wakaandika ukurasa mpya kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na chuki za kidini! Kifodini cha Stefano kinahusishwa na mtandao wa dhuluma na nyanyaso uliofanywa dhidi ya Wakristo huko Yerusalemu, hali inayoendelea hata leo hii kwani kuna Wakristo ambao hawako huru kuungama na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Lakini pia kuna nyanyaso na dhuluma ambazo zimefishwa katika tamaduni, usasa wa maisha na maendeleo. Hizi ni nyanyaso na dhuluma zisizopiga makelele! Lakini Wakristo wanawajibishwa kwa kumshuhudia Kristo katika maisha yao. Kuna wakuu wa Serikali wanatunga sheria zenye mwelekeo huu. Nchi ambazo hazifuati sheria hii ya jumla, zinashikishwa adabu na mataifa makubwa na yenye nguvu ya kiuchumi. Hii ni nyanyaso na dhuluma inayopoka uhuru na dhamiri nyofu!

Lakini ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu na kumkiria uhuru kamili. Waamini wanahamasishwa kutolea ushuhuda Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kinara wa dhuluma na nyanyaso anasema Baba Mtakatifu ni Shetani anayewasukuma wakuu wa nchi kutengeneza sheria zinazokwenda kinyume cha Mwana pamoja na Mungu mwenyewe! Huu ni ukanimungu, lakini, ikumbukwe kwamba, maisha ya Kikristo yanazidi kusonga mbele hata katika wimbi na dhuluma na nyanyaso kwani Kristo ameahidi kuwa na wafuasi wake hadi utimilufu wa dahali, lakini wanapaswa kuwa macho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.