2016-04-11 11:58:00

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya!


Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Mtakuwa mashahidi wangu kwa njia ya utakatifu na wokovu kwa watu wote! Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linavyoiandikia familia ya Mungu nchini Kenya, baada ya kuhitimisha mkutano wake wa mwaka, uliowapata nafasi ya kutafakari kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake, linachambua kwa kina na mapana hali ya taifa la Kenya, maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa kuhusu makossa ya jinai; Saratani ya rushwa na ufisadi; wizi wa mitihani; Tume huru ya uchaguzi; Ukabila; Utamaduni tenge miongoni mwa vijana na kwamba, uchu wa mali na madaraka ni chanzo kikuu cha kuyumba kwa kanuni maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya bado linakumbuka hija ya kitume iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini humo mwezi Novemba 2015 pamoja na changamoto mbali mbali alizotoa kwa Familia ya Mungu nchini humo, changamoto ya kushikamana ili kujenga na kuimarisha ujenzi wa Kenya mpya inayojikita katika ushuhuda, utakatifu na wokovu wa wengi! Kenya inapaswa kujengwa katika msingi wa uhuru, usawa, utu na heshima ya binadamu sanjari na kupambana na ujinga, umaskini na maradhi, ili kuleta maendeleo na mafao ya wakenya wote.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kusema kwamba, malengo haya msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na viongozi waasisi wa Kenya yamewekwa kando na matokeo yake viongozi wa Serikali wanataka kujinufaisha wenyewe kwa kutumia migongo ya wakenya! Maaskofu wanakaza kusema, hukumu iliyotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai haina tija wala mashiko kwa wananchi wengi wa Kenya kwani bado kuna umati mkubwa wa wananchi wasiokuwa na makazi, watu wanaosubiri kutendewa haki!

Hapa wananchi walipwe fidia na hatimaye, kuanza mchakato wa msamaha, upatanisho na umoja wa kitaifa, ili watu waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya iwe ni fursa kwa Kenya kuanza mchakato wa maisha mapya! Rushwa na ufisadi ni saratani inayoendelea kuwatumbukiza wananchi wengi wa Kenya katika umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa fursa za ajira hususan miongoni mwa vijana.

Umefika wakati kwa wananchi kusimama kidete kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi nchini Kenya, kwa kukataa kutoa na kupokea rushwa kwani rushwa ni adui wa haki. Kwa viongozi wanaotuhumiwa kwa kashfa ya rushwa, wakae pembeni, ili uchunguzi dhidi yao uweze kufanyika na haki kutendeka! Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na tabia ya kuiba mitihani na kudanganya kwenye mitihani shuleni, jambo ambalo ni hatari kubwa sana katika mchakato wa ujenzi wa elimu bora ndani ya jamii hali ambayo itadumaza utamaduni na Sanaa ya wanafunzi kusoma kwa bidi, juhudi na maarifa. Viongozi wanaohusika na kashfa hii wafukuzwe kazi mara moja na kufikishwa kwenye mkondo wa sheria. Kashfa ya rushwa na ufisadi inaendelea kuvindama vyombo vya sheria, Mahakama na Tume huru ya uchaguzi; vyombo muhimu sana katika kukuza na kudumisha utawala bora, sheria na demokrasia. Kutokana na rushwa na ufisadi, mipaka ya Kenya inakosa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao! Hapa wananchi wanapaswa kukataa kutoa wala kupokea rushwa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kuona kwamba, viongozi wengi wa Serikali na vyama vya kisiasa wananuka harufu ya rushwa na ufisadi! Baadhi yao wamekuwa ni wachochezi wakuu wa vurugu na mipasuko ya kijamii wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu; na matokeo yake ni kuwatumbukiza wananchi wa Kenya katika utamaduni wa kifo! Umefika wakati wa kukazia kanuni maadili, utu wema na utawala wa sheria.

Maaskofu wa Kenya wanasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya viongozi wanaoendelea kuchochea ukabila na kwamba, tabia hii haina tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Kenya. Hapa wananchi wakuze na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Inasikitisha sana kuona vijana wengi nchini Kenya wanamezwa na malimwengu kiasi cha kukosa heshima na adabu!

Vijana wanatumiwa na baadhi ya wanasiasa ili kujijenga na kujiimarisha kisiasa! Hawa ndio vijana wanaotumbukizwa katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, utumwa mamboleo na kwamba, baadhi ya wazazi wametelekeza dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto wao! Matokeo yake ni kizazi cha vijana wasiokuwa na hofu ya Mungu, wachovu wa maadili na utu wema! Hawa ni vijana wanaochungulia kaburi! Kuna haja kwa vijana kuwa na matumaini mapya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima yao; mambo msingi yaliyopewa mkazo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na vijana wa Kenya kule Kasarani.

Uchu wa mali na madaraka ni chanzo cha maovu na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema kunakoendelea kushika kasi ya ajabu nchini Kenya. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaitaka familia ya Mungu nchini Kenya kutokata tamaa, bali kusimama kidete kupinga rushwa na ufisadi pamoja na maovu yote ndani ya jamii, ili haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa viweze kutawala katika akili nan yoyo za watu! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena!

Na Paadre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.