Jumamosi majira ya asubuhi katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko alitoa Katekesi yake kwa mahujaji na wageni kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mafundisho ya Papa yalilenga katika Injili ya Matayo 6,1-4, somo lenye kuhimiza utoaji wa sadaka bila kujionyesha au kutafuta makuu. Papa alionya Mungu hatoi thawabu kwa sadaka zinazotolewa kwa nia za kujionyesha. Na alisisitiza utoaji wa sadaka lazima uwe kisiri siri , kimyakimya tena kwa unyenyekevu na bila mbwembwe, kiasi kwamba hata mkono wa kushoto usijue kiinachotolewa na mkono wa kulia. ”Sadaka na itolewe kwa siri ,na Baba aonaye sirini atajaza kilichopungua”.
Papa aliendelea kufafanua juu ya Somo hilo, akisema huongoza katika kugundua kipengele muhimu katika matendo ya huruma na utoaji wa sadaka. Na alionya kwamba, inaweza onekama kama ni jambo jepesi kutoa sadaka, lakini si hivyo kwa kuwa tunatakiwa kuwa waangalifu, ili sadaka tutoayo isionekana kama tendo la majivuno au kutaka kujionyesha mbele ya wengine au kama tu wema sana. Maelezo ya Papa yalirejea neno hili sadaka katika asili yake ya Kigriki akisema, ina maana ya huruma. Kwa hiyo, kwa maneno mengine, sadaka ni huruma. Na kwamba, huruma huweza onekana kupitia mambo na mifano mingi, inayolenga kupunguza makali ya upungufu kwa wahitaji.
Na kwamba , utoaji wa sadaka si jambo geni lakini limekuwepo nyakati zote tangu wakati wa Agano la Kale, imeandikwa jinsi Mungu, alivyotoa angalisho maalum kwa maskini wasiokuwa na kitu, wageni, yatima na wajane. Pamoja na kukumbusha wajibu huo, pia Mungu anataja kama jambo muhimu kwamba , sadaka ni lazima itolewa kwa ukarimu kama zawadi, bila ya moyo kuhuzunika. (Kumb 15:10). Hii ikiwa na maana kwamba, sadaka ni upendo , upendo wenye kufurahia na kuona fahari katika kusaidia wengine wahitaji . Ni kutoa kwa sababu umeguswa na mahangaiko ya wengine bila ya kuona kama ni mzigo au kutaka kuondokana na kero ya muombaji kwa haraka iwezekanavyo. Papa alieleza na kukikumbuka kisa cha Nabii Tobias , ambaye baada ya kupokea kiasi kikubwa cha fedha, alimwita mwanawe na kumpa maneno ya hekima akisema :kwa wale wote wote wanaotenda haki hutoa sadaka. Na usimpe kisogo maskini yoyote , na hivyo Mungu pia hatakupa kisogo Tb 4,7-8). Papa ameyataja maneno haya kuwa ni maneno ya busara sana yanayoweza kutusaidia kuelewa thamani ya kutoa sadaka.
Na alirejea mafundisho ya Yesu aliyowachia wafuasi wake, ambamo akataza kutoa sadaka kwa kujionyesha na mbwembwe.Sadaka isitolewa kwa nia za kujitafutia sifa kwa watu lakini katika kutambua kwamba kuna watu waliopungukiwa na mahitaji muhimu. Na upande mwigine, haipaswi kuonekana kama ni kosa kwa mtu anayeomba msaada . Na hivyo kumbe ni muhimu kutoa sadaka tukiwa na utambuzi kwamba , kuna watu wanaohitaji msaada wa haraka, bila kutazama nani anaomba au hadhi ya mtu anayeomba. Aidha Papa ametoa wito wa kutofautisha kati ya maskini na aina mbalimbali za ukosefu wa huduma unaowafanya watu kuwa maskini. Papa alieleza na kusema kwa kifupi sadaka ni tendo la upendo kwa mtu anayeomba ambaye tunakutana nae. Na tunapaswa kutoa msaada huo bila mtu mwingine kujua tulichotoa.
Papa alieleza na kutoa mwaliko wa kuyafanya maneno ya Mtume Paulo kuwa maneno yetu : Ni heri kutoa kuliko kupokea " (Matendo 20:35; taz 2Kor 9,7).
All the contents on this site are copyrighted ©. |