2016-04-09 09:35:00

Rushwa na ufisadi vinadumaza maisha ya wananchi!


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewataka Wajumbe na Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kuhakikisha wanakuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kuwa na Benki ya ardhi ili kuepuka migogoro.  Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa ALAT uliofanyika mjini Dodoma ambapo amewataka Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri wakasimamie upimaji wa ardhi katika maeneo yao na watambue mipaka yao.

Amesema kitendo cha kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo yao ni aibu kwani hali hiyo inaonyesha kuwa hawajajipanga hivyo ameziagiza halmashauri zote nchini zifanye mapitio ya ardhi waliyonayo na kutambua mipaka yao na wakibaini kama kuna matatizo wakutane na wizara husika kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi.

Pia mewataka wataalamu wa sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kusimamia vizuri sekta hizo ili kuleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla kwani kilioni kingine cha wananchi ni uduni wa sekta hizo ambazo ni muhimu kwa uchumi wa taifana ni chanzo kikubwa cha ajira kwani asilimia 75 wanaishi vijijini na wamejiajiri katika sekta hizo.

Pia asilimia 95 ya chakula kinazalishwa na wakulima wadogo, ambao hutumia zana na mbinu duni za kilimo, hivyo wanahitaji miongozo na maelezo kutoka kwa wataalam wa sekta hizo za kilimo, ufugaji na uvuvi ili waweze kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo Ijumaa tarehe 8 Aprili 2016 wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa ALAT uliofanyika…..ambapo amesema wakati wa kampeni za ukaguzi wa mwaka 2015, Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli aliahidi kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa vya mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Majaliwa amesema serikali itahakikisha wananchi wanatayarishwa na kujengewa uwezo wa kuzitumia fursa za kiuchumi, zinazoletwa na uwekezaji mdogo na mkubwa ili kuanzisha viwanda hivyo.

“Nazitaka Halmashauri ziweke mazingira rafiki kwa wawekezaji ili watakapotaka ardhi, waipate bila mizengwe na vibali vya ujenzi vitolewe kwa wakati, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetimiza azma ya serikali ya kujenga viwanda,” amesema.

Aidha, amewataka viongozi wa ALAT kuiongoza jumuiya hiyo kwa kuwaletea wananchi maendeleo hususana wenye kipato cha chini na kubuni mbinu mbalimbali zitakazosaidia halmashauri kuwa na ufanisi zaidi hasa katika kukusanya mapato.

Amesema sifa nzuri ya Halmashauri ni ile ya kukusanya mapato na kuyatumia kwa umakini katika kuwaletea wananchi maendeleo na ALAT wana nafasi kubwa ya kuzisaidia Halmashauri hizo kufanya vizuri zaidi na kwa ufanisi mkubwa.

MWISHO

,Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Khadija Mussa-Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Waziri Mkuu








All the contents on this site are copyrighted ©.