2016-04-09 08:36:00

Ninakupenda, imarisha pendo langu kwako!


Ndugu wapendwa, karibuni tena katika tafakari ya Neno la Mungu dominika hii ya tatu ya pasaka. Baada ya kutafakarishwa na wito wa huruma ya Mungu, leo tunaalikwa kutafakari sana mahusiano yetu na Mwenyezi Mungu. Somo la kwanza linatanguliza tafsiri ya kile kilichopo katika somo la injili, ukamilifu wa kilichosemwa na Yesu. Somo la pili laongelea kuhusu ushindi wa mwisho, wale walio wake Mungu wanasherehekea ushindi. Katika sehemu hii ya Injili toka Yohane twaona mara ya tatu na ya mwisho ya tokeo la Yesu kama ilivyorekodiwa naye Yohani. Somo linatuonesha kuwa Yesu hakufufuka tu kwa maana ya maneno bali hakika kimwili pia. Ushuhuda wa mitume uko wazi - tulikula na kunywa pamoja naye baada ya ufufuko wake. Petro anasisitiza hili katika somo la kwanza. Katika Injili, Yesu anaongea na Petro na inafuata kula samaki na mitume. Halafu yanafuata maswali matatu na majibu matatu na hitimisho tatu – lisha kondoo wangu

Kwa neno hili la Yesu yaeleweka kuwa Petro anakabidhiwa rasmi mamlaka ya uongozi. Anamkabidhi uongozi wa kanisa aliomwahidia alipomwambia ‘wewe ni mwamba na juu ya mwamba huu nitajenga kanisa langu’ – Mt. 16:18-19. Yesu anabaki mwaminifu hata kama mwanadamu anakosa uaminifu – Mt. 26:35. Maswali matatu ya Yesu kwa Petro, yanabatilisha majibu matatu ya Petro dhidi ya ufahamu wake kwa Yesu. Watu wengi husema hapa ndo Petro anapata uongofu. Wengine huita ungamo la Petro. Ungamo hili la Petro laweza fananishwa na ungamo la yule  baba mwenye mtoto aliyepagawa na shetani katika Mk. 9:24 - hapo baba wa kijana alilia kwa sauti kubwa, Nasadiki. Saidia kutokuamini kwangu. Anachosema Petro ni kuwa ndiyo Bwana nakupenda, ongeza upendo wangu kwako.

 Daima Mungu humpatia mwanadamu nafasi zaidi ya moja. Changamoto hii inampatia Petro nafasi ya kuanza upya. Tangu hapo anachukua nafasi ya Yesu katika ulimwengu. Anaondoka Galilaya na kwenda ulimwenguni kutangaza habari njema. Mwishoni anathibisha ahadi yake ya uaminifu kwa Kristo kwa kutoa maisha yake kwa Kristo. Ukuu wa Yesu wa kusamehe na kumpa mwanadamu nafasi, unampatia nafasi hata mvovu kuongoka. Mazungumzo kati ya Yesu na Petro, hubadilisha maisha ya kila mmoja wetu. Mt. Agostino akitafakari sehemu hii anasema kuwa kwa kumwuliza Petro maswali, Yesu pia atuuliza kila mmoja wetu swali lile lile – Je, wanipenda?

Ndugu wapendwa, ukristo siyo mkusanyiko wa maandiko mazuri bali ni swala la ufungamano wa ndani. Ni swala la mahusiano na Kristo. Kabla ya ufufuko wake aliwafundisha watu kumwamini na kumsadiki Mungu. Tumeona pia hili dominika ya pili kwamba kiini cha ibada ya huruma kwa Mungu ni kumwamini na kumsadiki zaidi Yesu. Hakuongelea kuhusu kumpenda. Swala la upendo amelisema baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Upendo kwa Kristo huonekana kwa kuwapenda wengine. Hana haja na faida ya upendo huo. Anachotaka yeye ni kondoo wake wafaidike. Sababu na chanzo cha upendo huo ni Mungu Baba. Mama Teresa anasema – tunda la upendo ni huduma na tunda la huduma ni amani. Yesu atualika tumpende na tukifanya hivyo tutawapenda wengine.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso. C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.