2016-04-09 12:15:00

Mapambano ya maambukizi ya Ukimwi kwa watoto wadogo!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kuanzia tarehe 11- 13 Aprili, 2016 linaendesha mkutano wa kimataifa utakaoibua mbinu mkakati wa kuwasaidia watoto wanaoishi na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi. Shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa UNAIDS katika taarifa yake ya mwaka 2015 linaonesha kwamba, kuna watoto millioni 15 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekwisha ingizwa katika mpango wa kutumia dawa za kurefusha maisha, ART.

Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, ni idadi ndogo sana ya watoto ambao wamefanyiwa uchunguzi na hatimaye kuwekwa kwenye orodha ya watoto wanaosaidiwa kupata dawa ya kurefusha maisha. Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, UNAIDS pamoja na wadau mbali mbali, wanakutana ili kujadili mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika mapambano dhidi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, changamoto zilizoko kwa sasa na kwa siku za usoni na mkakati wa kuchunguza magonjwa nyemelezi na hatimaye kutoa tiba kwa watoto wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.

Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja na Balozi Deborah Birx, mratibu mkuu wa ugonjwa wa Ukimwi na mkurugenzi mtendaji wa PEPFAR ni kati ya wazungumzaji wakuu katika mkutano huu ambayo utawashirikisha wadau mbali mbali kutoka katika mashirika ya kidini yanayojihusisha kwa karibu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.