2016-04-09 14:12:00

Mahali pa sala na tafakari!


Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano wa mtoza ushuru na mfarisayo waliosali hekaluni. Alionyesha maana ya mahali maalum kwa ajili ya sala. Nami leo ninapenda nigusie kidogo nafasi ya mahali pa sala, mahali kwa ajili ya sala katika maisha yetu ya sala. Jinsi muda tuliotenga kwa kusudi maalum la kusali, kukutana na Mungu, unatusaidia sana kupanga kwa busara mambo yote ya kutwa nzima, juma, mwezi na mwaka, vivyo hivyo kujitafutia mahali panapofaa kwa ajili ya sala kunasaidia kuleta utaratibu, mpangilio bora na uwiano mzuri wa mambo yote katika maisha yetu yote na katika mazingira yetu.

Kusudi tuweze kuwa watu wazima kiroho na kiakili na kimwili, tunahitaji uwiano bora na utaratibu bora, mpangilio bora katika maisha yetu na mazingira yetu. Hatuwezi kuwa watu wazima endapo nyumbani kuna vurugu, vitu vimezagaa hovyo. Tunapopata mahali kwa ajili ya kusali, mahali hapo panaanza kuvumisha amani na kuleta utaratibu na mpangilio mzuri katika maisha yetu na mazingira yetu. Kwanza tutaona jinsi nyumbani tunavyoanza kupanga vizuri mambo, baadaye katika shughuli zetu, kazi zetu n.k.

Mahali pa kwanza pa sala palikuwa ni Bustani ya Edeni, mahali patakatifu. Katika bustani hiyo binadamu aliishi katika uhusiano kamili na Mungu, Muumba wake. Aliishi pamoja na Mungu. Binadamu alipotenda dhambi, alijifukuza pale na ilimbidi ajitafutie mahali pengine, mahali ambapo hapakuwa tena patakatifu. Ndiyo maana binadamu alianza kujificha mbele ye Mungu. Dhambi ilipoenea ulimwenguni, Mungu aliamua kujitafutia sehemu mbalimbali, kama visiwa katika bahari ya uovu na dhambi, ambapo angeweza kukutana na binadamu huyo. Tunaposoma Maandiko Matakatifu, Agano la Kale, tunaona jinsi Mungu alivyokuwa anakutana na watu katika sehemu mbalimbali. Na watu hao walioguswa sana na matukio hayo ya kukutana na Mungu, waliaanza kuziita sehemu hizo walipokutania na Mungu kama sehemu au mahali patakatifu.

Mfano: Yakobo alipokuwa anamkimbia Esau, alikutana na Mungu Aliye Hai sehemu ambayo baadaye aliita kwa jina la Betheli. Akasema: „Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni” (Mwa 28, 16-17). Hivyo Yakobo akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake (taz. Mwa 28,18) kusudi watu wote wajue kuwa hapo ni mahali patakatifu ambapo binadamu alikutana na Mungu Aliye Hai.

Musa alipopanda mlima mtakatifu wa Bwana, aliambiwa na Bwana: „Musa! Musa! (...) Usikaribie hapa! Vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu” (Kut 3,4-5). Mungu alidai Musa awe na heshima kubwa na uchaji mahali pale. Lakini amri hii ya Mungu ya kuvua viatu ina maana nyingine tena. Kwa sababu mahali pale ni patakatifu, basi, kwa kuvua viatu, miguu ya Musa iliweza kugusa mahali patakatifu na hivyo mwili wake mzima, nafsi yake nzima ilipata kutakatifuzwa. Utakatifu wa mahali ulienea hadi ndani ya nafsi ya Musa. Mahali hapo baadaye pametengwa katika Hekalu la Mungu Yerusalemu kama Patakatifu Patakatifu ambapo kuhani mkuu aliruhusiwa kuingia mara moja tu kwa mwaka.

Katika dini zote za ulimwengu daima tunakuta mahali patakatifu, mahali pa sala panapoheshimiwa sana. Hakuna dini ambayo haithamini mahali patakatifu kuanzia dini za jadi. Hata katika jumba la makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, kuna chumba cha sala, mahali maalum palipotengwa kwa ajili ya sala na tafakari.

Binadamu anahitaji mahali patakatifu, kusudi utakatifu wake uenee ndani mwake na katika maisha yake na shughuli zake zote. Mahali patakatifu panang’aa maishani mwetu, pakileta uwiano bora wa mawazo yetu, hisia, maamuzi na kazi. Mahali patakatifu panatusaidia sana kutumia vema na kwa busara maisha yetu na muda wa maisha yetu. Ndiyo maana kila mahali panapaswa kuwa na sehemu hizo takatifu – hospitalini (katika hospitali nyingi Ulaya na Marekani kuna vikanisa vidogo ambapo wagonjwa na wauguzi wanasali na kuomba msaada kutoka kwa Mungu), katika viwanja vya ndege, hata gerezani. Binadamu aweze kukutana na Mungu Aliye Hai mahali ambapo ni patakatifu, mahali pa kukutania na Mungu Aliye Hai.

Tunajua kuwa kila kanisa lililowekwa wakfu ama kwa baraka au kwa kutabarukiwa ni mahali patakatifu. Tunapoingia ndani yake, tunajitakasa tukijibariki kwa ishara ya msalaba na kwa kutumia maji ya baraka. Tunaingia mahali patakatifu ili utakatifu wake ututakatifuze sisi, uingie ndani ya nafsi zetu na katika maisha yetu nasi tuweze kuubeba utakatifu huo hadi nyumbani kwetu na katika maisha yetu na matendo yetu ya kila siku ili utakatifu huo utakatifuze maisha na mazingira yetu na yote tuyafanyayo.

Katika mahali patakatifu kila mmoja wetu ana mahali pake anapopapenda. Inaonekana wazi kuwa kila mmoja wetu katika kanisa lake ana sehemu yake ambayo anaipenda na kila mara anapenda kukaa pale. Sehemu unayochagua kanisani inatokana na hali yako ya kiroho ya ndani. Kadiri unavyozidi kumpenda Mungu na kujitahidi kuishi maisha ya kiinjili, ya kikristo, basi, utazidi kupenda kukaa karibu na karibu zaidi na Patakatifu kanisani, karibu na altare. Vivyo hivyo, kwa kawaida - na utafiti wa watalaam wengi unaonyesha - wale ambao mioyo yao inazidi kuwa mbali na Mungu wanapenda kukaa mbali, mlangoni, kana kwamba wanaonyesha kuwa katika maisha yao wamekuwa wamejitenga na Mungu Aliye Hai.

Turudi tena kwenye mfano wa mtoza ushuru na mfarisayo. Mtoza ushuru hakuthubutu kusogelea mbele akijisikia kuwa mwenye dhambi, mfarisayo alijiona kuwa sawa, ndiyo maana alienda mpaka mbele ya altare. Kwa vyoyote lakini, ni vema kila mmoja wetu awe anakaa pale ambapo anajisikia vizuri, ambapo ataweza kusali vizuri na kukutana na Mungu. Licha ya kusali kanisani, tunazo sehemu nyingi ambapo tunapenda kusali. Hapa mlimani zipo sehemu ambazo huwa tunachagua tukipenda kukaa na kusali na kutafakari. Watu wanapenda kupanda milima ili wasali. Wengine wanakwenda sehemu takatifu kama hija vile. Wengine wakikaa na kutazama uzuri wa uumbaji wa Mungu, wanapata fursa ya kuongea na Mungu, wanajiskia wako karibu naye.

Yesu pia alipenda kusali nje, kusali kwa kutazama uzuri wa uumbaji wa Baba yake wa mbinguni. Alikuwa anasali usiku, milimani, faraghani, alikuwa anajitenga na watu na kusali kwa muda mrefu, pengine hata usiku kucha. Alipenda hasa kupanda milima na kusali kileleni. Mfano pale alipogeuka sura. Leo ningependa tuzungumze juu ya mahali patakatifu ambapo tunaweza kupaandaa sisi wenyewe. Waislamu wanatumia zulia popote wakisafiri; muda wa sala ukifika wanatandaza zulia yao na kusali. Zulia ndiyo mahali patakatifu, mahali pa kukutania na Mungu.

Tufikiri kwa muda mfupi na tujiulize: je, majumbani mwetu tuna mahali ambapo huwa tunapenda kusali – ndani au nje? Mahali ambapo nikikaa au kupiga magoti, ninajisikia niko karibu na Mungu? Kama sina, basi, hii ni alama kuwa mji wangu hauna mpangilio mzuri, hauna utaratibu mzuri. Maana hauna nafasi kwa Mungu. Hakuna sehemu ambapo Mungu akija anaweza ‘kukaa’. Ninaweza kuwa na mpangilio mzuri katika masanduku na makabati, lakini si moyoni mwangu na maishani mwangu! Sitapata amani na utulivu katika roho yangu endapo sitakuwa na mahali pa pekee pa kukutania na Mungu.

Wakati fulani Padre fulani aliamua kumtembelea mgonjwa fulani, mwanaparokia yake, mzee fulani wa makamu. Alipiga hodi. Mgonjwa alipomfungulia mlango alifurahi, lakini pia ilionekana kuwa alishtuka sana. Akamwambia Padre: „Asante kwa kunitembelea, lakini sitathubutu kukukaribisha ndani kwa sababu sijafanya usafi, mambo yote yako shaghala bagala”. Lakini Padre alisisitiza kuwa hamna shida na bila shaka itapatikana sehemu watakapoweza kuketi na kuongea kidogo. Basi, mgonjwa alikubali shingo upande. Padre huyo baada ya kutazama jinsi kweli vitu mle ndani vi hovyo hovyo, aliamua kumsaidia mzee huyo kupanga kidogo vitu vyake na vitabu. Akatoa vitu kwenye viti viwili, akatoa matakataka kwenye sehemu ya meza na hivyo alipata kasehemu kadogo ambako waliweza kuketi na kuongea.

Baada ya kumaliza mazungumzo yao, mgonjwa huyo alimshukuru sana Padre akisema kuwa hamshukuru kwa ajili ya kufika tu, bali hasa anamshukuru kwa ajili ya kumwonyesha kuwa nyumbani kwake kuna sehemu ambapo binadamu anaweza kujisikia vizuri, anaweza kukutana na mwingine. Hakuamini. Padre baada ya kurudi kwa mzee huyo baada ya miezi miwili alikuta kuwa mzee alikuwa ameshapanga vitu katika karibu nyumba nzima. Mzee mwenyewe alikuwa na furaha. Ilionekana alikuwa ameridhika na nyumba yake na mpangilio mzuri wa vitu na kuona ile sehemu ya kuweza kukaa na wengine na kuongea nao kulimridhisha sana na kumfanya awe mzima kuliko awali.

Mimi mwenyewe ninaweza kushuhudia jinsi wazazi wangu walivyojitengezea visehemu vyao kwa ajili ya sala. Kwetu tulikoishi ni nyumba ya ghorofa kumi ambapo familia 44 zinaishi. Sisi tuliishi kwenye ghorofa ya 8. Tulikuwa na vyumba vitatu vidogo, kajiko na kabafu. Sehemu yote hiyo inaweza kulingana na kanisa letu dogo au kuwa ndogo zaidi. Walimoishi ni baba, mama na bibi mzaa mama. Kila mmoja alikuwa na chumba chake. Kila mmoja alikuwa na sehemu yake ya kusali asubuhi na jioni. Baba karibu na kitanda chake ameweka vitabu mbalimbali vya sala, rozari, picha takatifu, juu ya kitanda alitundika picha ya Mama Bikira Maria na Msalaba. Kila asubuhi saa 10.30 alfajiri aliamka na kutandaza kitandani picha zake takataifu na vitabu na kuanza kusali akipiga magoti. Baada ya nusu saa hivi alikuwa amemaliza sala zake. Ndipo alipoenda kujiandalia chai na kwenda kazini (kabla hajastaafu). Saa 12.00 alfajiri alikuwa ameshafika kwenye kanisa la wafransiskani lililopo njiani kwenda kazini (kazini ni kilometa 15 kutoka nyumbani). Alishiriki Misa ya saa 12.30 asubuhi parokiani ingawa alikuwa mzee.

Mama yangu mzazi naye alikuwa na sehemu yake ya kusali dirishani. Ameweka kameza kadogo kamviringo, akapanga pembeni mwake vitabu vya sala, rozari, juu ya kitandaaliweka msalaba na picha za Bikira Maria na Yesu wa Huruma pamoja na picha zetu watoto wake na wajukuu ili atukumbuke katika sala. Ameweka pia karedio kadogo, maana alipenda sana kusikiliza vipindi vya dini redioni hasa akikamata stesheni ya redio katoliki ya taifa.

Bibi naye vivyo hivyo. Alikuwa na kakabati kafupi hivi chumbani mwake, napo alipanga picha za watoto na wajukuu na vitukuu, akaweka vitabu vyake vya sala, akaweka sanamu ya Bikira Maria wa Fatima, akaweka na rozari. Halafu alikuwa anakaa kwenye kakochi kadogo nilikokuwa nikitumia nilipokuwa bado ninafanya kazi Jimboni mwetu. Hako kakochi kalimkumbushia mjukuu wake aliyeko Tanzania.

Sisi je? Sehemu yetu ya sala ikoje? Iko wapi? Tunayo? Mahali pangu pa kukutania na Mungu Aliye Hai pako wapi? Endapo ninajua saa ngapi ninakutana na Mungu – kwa dakika tano au kumi asubuhi na jioni au saa nyingine; endapo ninajua kuwa ninahitaji kuwa makini katika sala na ninahitaji kujiweka mbele ya Mungu, lazima pia nijue nitakutana naye wapi? Ninahitaji mahali tutakapoweza kukutana kama marafiki. Tunahitaji kuwa na mahali binafsi pa kukutania na Mungu.

Endapo nina bahati ya kugundua hitaji hilo, endapo nina mahali pangu pa kukutania na Mungu – nyumbani – basi, nitagundua mapema kuwa inaniwia rahisi zaidi na zaidi kukutana na Mungu na kumwona na kujisikia niko karibu naye – njiani, hospitalini, ninaposafiri. Kipaji hiki cha kukutana na Mungu mahali pote kinatokana na ujuzi wa kujiandalia na kuitumia vema sehemu binafsi, mahali pa kukutania na Mungu hai nyumbani kwetu.

Maswali. Je, tunamshukuru Mungu kwa ajili ya Hekalu hili takatifu tunapokutana naye? Tumeshamshukuru kwa mahali patakatifu hapa? Hapa ni mahali patakatifu sana, mahali pa pekee pa neema. Hapa tunapata nguvu na neema, hapa tunatakatifuzwa kiasi cha kutosha kutakatifuza shughuli zetu na siku zote za juma zima na maisha yetu yote kwa ujumla! Tumshukuru Mungu pia kwa ajili ya sehemu zetu takatifu za sala nyumbani kwetu – kama ni chumbani mwako unapolala, au sebuleni au sehemu nyingine maalum. Mshukuru Mungu kwa hilo. 

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak

Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.