2016-04-09 15:28:00

Baba Mtakatifu Francisko kukutana na Rais Touadèra kutoka Afrika ya Kati!


Professa Faustin Archange Touadèra, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati Jumatatu tarehe 18 Aprili 2016 anatarajiwa kukutana na kuzungumza ana kwa ana na Baba Mtakatifu Francisko ili kumshukuru kwa changamoto ya ujenzi wa msingi wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Haya ni mambo msingi yaliyofanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwa amani na usalama, baada ya kinzani, vurugu na mipasuko ya kisiasa, kijamii na kidini!

Rais Touadèra anakuja mjini Vatican akiwa amebeba ndani ya moyo wake shukrani za dhati kabisa kutoka kwa wananchi wa Afrika ya Kati, walionja upendo na mshikamano wake wa kibaba na imani thabiti pasi na woga! Akawa ni chombo cha huruma ya Mungu inayomwilishwa katika mateso na mahangaiko ya watu waliokata tamaa kutokana na vita na machafuko ya kidini, kisiasa na kijamii. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Afrika ya Kati, imekuwa ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa watu waliokuwa wanateseka kutokana na vita kiasi hata cha kutengwa na Jumuiya ya Kimataifa!

Baba Mtakatifu akaonesha ujasiri wa imani, akathubutu kwenda Bangui, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga na kudumisha upendo, haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hii itakuwa ni safari ya kwanza ya kimataifa kufanywa na Rais Touadèra tangu alipoingia madarakani, Mwezi Februari 2016. Taarifa ya safari hii ya kikazi mjini Vatican imetolewa na Ubalozi wa Vatican nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuridhiwa kwa mikono miwili na Baba Mtakatifu Francisko aliyethubutu kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, Jamhiri ya Watu wa Afrika ya Kati!

Baada ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Afrika ya Kati iliyomwezesha kujionea shida na mahangaiko ya watoto na wanawake, Hospitali ya Bambino Gesù, inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican ikaamua kusaidia huduma katika Hospitali ya Watoto Bangui, ili kweli hospitali hii iweze kuwa ni kituo kinachomwilisha huruma ya Mungu kwa watoto kwa njia ya tiba muafaka.

Rais Mariella Enoc wa Hospitali ya Bambino Gesù anasema, Hospitali yake imekwisha kusaidia kununua Jenerata kwa ajili ya kuzalisha umeme walau kwa muda wa saa 4 kwa siku. Lakini lengo kubwa zaidi ni kusaidia majiundo makini ya wahudumu wa afya ya mama na mtoto kwa siku za usoni; ukarabati mkubwa wa majengo ya hospitali pamoja na kugharimia mishahara ya madaktari kumi na sita watakaojisadaka kutoa huduma ya upendo kwa watoto wagonjwa huko Bangui!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.