2016-04-08 13:24:00

Wosia wa kitume: Furaha ya Upendo ndani ya familia!


Furaha ya Upendo ndani ya familia “Amoris laetitia” “AL” ni wosia wa kitume ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Injili ya familia na kuchapishwa rasmi tarehe 19 Machi 2016, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mume wake Bikira Maria sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitatau tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wosia huu wa kitume ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na mwaka 2015.

Baba Mtakatifu Francisko amechota utajiri mkubwa kutoka katika hati elekezi ya Mababa wa Sinodi wakati wa kuandika Wosia huu wa kitume. Baba Mtakatifu anaonesha mwendelezo wa mafundisho ya watangilizi wake kuhusu Injili ya familia pamoja na kuchota mchango wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kama vile Kenya, Australia na Argentina. Kuna watu maarufu kama akina Martin King Luther wamenukuliwa katika Wosia huu wa kitume ili kufafanua kwa namna ya pekee umuhimu wa sadaka katika maisha na utume wa familia. Wosia huu unaelekezwa kwa Familia ya Mungu katika ujumla wake!

Utangulizi:

Wosia wa Furaha ya Upendo ndani ya familia umegawanyika katika sura tisa zenye utangulizi mfupi, kwa kuonesha mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya familia, mchango ambao unapaswa kutunzwa kama hazina ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, si majadiliano yote mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa, maadili au ya kichungaji yanapaswa kujadiliwa na  Khalifa wa Mtakatifu Petro, bali mambo mengine yanahitaji kupatiwa ufumbuzi makini kadiri ya mila, tamaduni na changamoto mahalia. Hii inatokana na ukweli kwamba, tamaduni zinatofautiana, kumbe, hapa kuna haja ya kutamadunisha changamoto hizi ili ziweze kuendelezwa na kutumika.

Utamadunisho ni muhimu sana hata katika mafundisho ambayo yamefafanuliwa na Mama Kanisa katika uzito wake, hapa hakuna sababu ya msingi ya kuwa na mwelekeo wa utandawazi. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kujinasua na wasi wasi wa mabadiliko na utekelezaji mkali wa sheria zinazoelea angani. Baba Mtakatifu anasema malumbano yanayojitokeza kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii na machapisho mbali mbali na hata wakati mwingine kati ya viongozi wa Kanisa yanafanyika kwa kutaka mabadiliko makubwa bila kuwa na tafakari ya kina ya kile wanachotaka kubadilisha au kwa kuwa na hitimisho kavu la masuala ya kitaalimungu. Familia ya Mungu ichukue muda kusoma na kuutafakari wosia huu kwa uvumilivu pasi na haraka na pale inapowekezana kuangalia mada maalum kadiri ya mazingira husika.

SURA YA PILI. Katika Mwanga wa Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, Neno la Mungu ni “mwandani”  wa familia hata kwa familia ambazo zinakabiliwa na “migogoro” kwa sababu linawaonesha dira na njia ya kufuata. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanaume na mwanamke wanapoungana pamoja katika kifungo chau pendo wanapendana na kuwa ni chemchemi ya uhai, mfano hai wa Mungu Mwenyezi ambaye ni Muumbaji na Mkombozi.

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja katika upendo, tunu zinazopaswa kushuhudiwa ndani ya familia. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majadiliano unanopaswa kufahamika kuwa ni mwambatano wa kimwili na maisha ya ndani, unaowawezesha wanandoa kuwa kitu kimoja sanjari na kujisadaka katika upendo. Utu wema ni tunu muhimu sana katika mang’amuzi ya maisha ya ndoa na familia ya Kikristo, ingawa tunu hii mara nyingi inasahaulika na wengi nyakati hizi za mahusiano ya haraka haraka na yasiokuwa na mizizi.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa malezi na majiundo makini ya watoto, mawe hai ndani ya familia, zawadi ya Mungu na wala si mali ya mtu binafsi. Anagusia tatizo la ukosefu wa fursa za ajira ndani ya familia; mateso na mahangaiko ya  familia za wakimbizi na wahamiaji wanaokataliwa na kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, wanaishi katika mazingira magumu na wasi wasi mkubwa!

SURA YA PILI: Ukweli na changamoto za familia.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mafao ya familia ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ulimwengu na Kanisa kwa siku za usoni, kumbe, unapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Hapa Baba Mtakatifu anaorodhesha litania ya matatizo yaliyobainishwa na Mababa wa Sinodi mintarafu familia katika ulimwengu mamboleo: Ubinafsi unaotishia dhana ya uhuru na haki kwa kuzing’oa kutoka katika ukweli, tunu msingi na kanuni za maisha kiasi cha kutoa mwelekeo kwamba, kila jambo linaruhusiwa. Ubinafsi, utamaduni usiojali kwa kudhalilisha upendo ambao unageuzwa na kuonekana kuwa ni jambo la mitandao ya kijami; upendo unaoweza kuunganishwa, kutatizwa au kusubilishwa kadiri ya matakwa ya mlaji! Kwa njia hii Baba Mtakatifu anasikitika kusema, watu wanageuza familia kuwa ni jambo la mpito; mahali pa kukutana pale mtu anapojisikia.

Hapa ndipo mahali muafaka ambapo mchango wa Wakristo unapaswa kujionesha kwa kuambata ndoa na kwenda kinyume cha mtazamo na mawazo ya watu wa nyakati hizi kwamba, ndoa  ni kama ”mtindo” au kwa kujisikia wanyonge katika ngazi ya ubinadamu na maadili. Mwelekeo huu wa Kikristo haupaswi kuwa tu kama kigezo cha kupambana na mwelekeo potofu wa dhana ya ndoa na familia kwa kujilinda; kwa kwenda kinyume cha ari na ugunduzi wa kimissionari au kwa kujikita katika sheria.

Baba Mtakatifu anasema, mwelekeo wa Kikristo unapaswa kuwa ni kielelezo cha uwajibikaji unaojikita katika ukarimu; kwa kushuhudia sababu msingi na malengo ya maisha ya ndoa na familia. Hapa kuna haja ya kuonesha ukomavu unaojikita katika ukweli na uhalisia wa maisha na kwamba, Wakristo wengi wamejikuta wakishuhudia maisha ya ndoa inayojikita kimsingi katika kazi ya uumbaji au katika masuala ”mafundisho tanzu ya Kanisa” maadili na kanuni maadili viumbe; mambo ambayo yamewafanya wanandoa wengi kuishi katika ombwe bila kugusa uhalisia wa mambo! Wengi wameona ndoa kuwa ni mzigo ambao wanapaswa kuubeba katika maisha yao, badala ya kuwa ni safari katika ukuaji na utimilifu wa mtu.

Baba Mtakatifu anaitaka mihimili ya Uinjilishaji kujikita kwa namna ya pekee katika majiundo makini ya dhamiri nyofu bila kujidai kwamba inataka kubadili mwelekeo. Hapa kuna haja ya kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zenye mwelekeo chanya na ukarimu; zinazoweza kutoa dira na mwelekeo barabara na sahihi wa kupata furaha ya kweli; kwa kuonesha ukaribu wa upendo kwa wanyonge. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua changamoto ambazo wanafamilia wanapaswa kukabiliana nazo katika ulimwengu mamboleo mintarafu mchango wa Mababa wa Sinodi za Maaskofu zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na mwaka 2015.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapinga kwa nguvu zote sera na mikakati inayofumbata utamaduni wa kifo kwa kuruhusu: vizuia mimba; kuwafanya watu kuwa tasa au utoaji wa mimba. Baba Mtakatifu anawaambia wanandoa kwamba, kwa kuwa na dhamiri nyofu na wanapoona kuwa kweli katika safari ya maisha yao wamekuwa wakarimu katika kuendeleza zawadi ya maisha, wanaweza kuamua kuwa na mwelekeo wa kuratibu idadi ya watoto wanaotaka kupata kutokana na sababu msingi!

Baba Mtakatifu anasema, kati ya umaskini mkubwa ambao jamii nyingi zinakabiliana nao kwa nyakati hizi ni kupungua kwa imani na matendo ya ibada, hali inayowatumbukiza watu wengi katika upweke, dalili za kutokuwepo kwa Mungu katika maisha ya watu. Familia na nyumba ni chanda na pete na kwamba, haki ya familia si haki ya mtu binafsi kwani familia ni kito cha thamani ambacho kinapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa na jamii kwa kuwa na sera makini ya familia. Baba Mtakatifu anagusia pia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinazofanywa kwenye familia, shule, jumuiya na taasisi ambazo zimepewa dhamana ya kuwalinda! Hii kashfa isiyovumilika kabisa!

Baba Mtakatifu anasema kuna familia za Kikristo zinazoteseka kwa kudhulumiwa na kunyanyaswa; kuna familia zenye walemavu, wazee na mbaya zaidi ni umaskini wa hali na kipato. Kwa familia zinaosambaratika umaskini unakuwa ni mzigo mkubwa kwani hapa wanawake ndio wanaobeba dhamana kubwa ya malezi na matunzo ya watoto wao. Watu wa jinsia moja wanaoishi pamoja, si ndoa kwani haya ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa na mpango wa Mungu kwa binadamu mintarafu kazi ya uumbaji.

Ndoa za namna hii zinahatarisha na kudhoofisha tunu msingi za Injili ya familia. Utu wema na kanuni maadili ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa na wote. Dhuluma na nyanyaso kwa wanawake ni kudhalilisha utu na heshima yao! Hakuna sababu msingi za kuwabagua wanawake, bali haki na wajibu wao vinapaswa kulindwa na kudumishwa! Lakini Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kuna misimamo mikali ya kutetea wanawake ambayo haiwezi kukubalika hata kidogo.

Suala la usawa wa kijinsia ni jambo ambalo ni hatari kwa malezi na makuzi ya watoto; tofauti za kijinsia zinaweza kubainishwa lakini haziwezi kutenganishwa; changamoto ni kuheshimu kazi ya Uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, maisha ni zawadi inayopaswa kupokelewa kwa heshima na taadhima; kwa kulindwa na kudumishwa kadiri ya mpango wa Mungu.

SURA YA TATU. Mwelekeo kwa Yesu: Wito wa Familia.

Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anatoa muhtasari wa mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia. Hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na ina mwelekeo wa kudumu ambayo ni zawadi. Ndoa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya upendo wa kweli wa wanandoa na wito mahususi wa kuishi kama bwana na bibi. Ndoa ni Sakramenti na zawadi inayowawezesha wanandoa kujikita katika mchakato wa utakatifu na wokovu wa wanandoa wenyewe. Kwa mwelekeo huu tendo la ndoa ndani ya familia, lililotakatifuzwa kwa Sakramenti ni njia ya kukua na kukomaa katika neema na Fumbo la maisha ya ndoa, mwaliko kwa wanandoa kumwomba Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuibariki Ndoa yao.

Kanisa halina budi kuwasaidia wanandoa wanaoishi “uchumba sugu” wale waliofunga ndoa ya Serikali; wanandoa wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha ya ndoa kwa baada ya kuoa au kuolewa  na kuachika na baadaye kuamua kuoa au kuolewa tena. Viongozi wanapaswa kuwashughulikia watu hawa kwa kuongozwa na ukweli wa upendo; wawafafanulie kwa kina na mapana mafundisho ya Kanisa na kwamba, hakuna majibu ya mkato, bali kila kesi inapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Viongozi wawe na hekima ya kutambua unyeti wa masuala wanayoshughulikia. Kwa wanandoa ambao hawakubahatika kupata watoto kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanahamasishwa kuridhika kwa kujikita katika utu wema na Ukristo, kwani watoto kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa mara nyingine tena tunu msingi ya maisha ya binadamu na haki ya mtu kuishi tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo cha kawaida kinaqpomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu!

Wafanyakazi katika sekta ya afya wanayo dhamana ya kimaadili kwa kukuza dhamiri nyofu ili kuendeleza zawadi ya uhai kwa kutojiingiza kwenye vitendo vya kifo laini au tiba za ghali sana. Kanisa linapinga adhabu ya kifo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, kuna mahusiano muhimu sana kati ya Familia na Kanisa, kwani ikiwa kama Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, Kanisa ni familia ya familia na kwamba, upendo unaomwilishwa kwenye familia ni nguvu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

SURA YA NNE: Upendo ndani ya ndoa.

Baba Mtakatifu Francisko anaianza sura ya nne kwa utenzi wa upendo kati ya ndugu kama anavyoutafakari Mtakatifu Paulo mtume, katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 13: 4-7 na kuuweka katika mazingira ya familia: Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; haoni uchungu, hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote. Baba Mtakatifu anasema huu ndio urafiki unaojengwa katika upendo wa dhati; unathamini na kujali  utajiri wa mwingine pamoja na kuwa na jicho pana zaidi kwani ndoa ni mchakato unaomwilisha zawadi za Mungu kwa binadamu!

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kuchangamkia maisha ya ndoa na familia na wala wasione kuwa ni mzigo usioweza kubebeka bali safari ya maisha inayowaelekeza kwenye ukomavu, kwa kupokea kwa ukweli na busara mapungufu yao ya kibinadamu na changamoto zilizoko mbele yao. Vijana wanapaswa kujikita katika majadiliano ili kushuhudia, kuishi na kukomaa katika upendo. Watambue kwamba, wanatofautiana na kwamba, tofauti zao ni sehemu ya utajiri wao!

Upendo wao ni chachu muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia na huduma kwa maisha ya pamoja. Hapa kuna haja kwa vijana kupata malezi makini kuhusu vionjo vya kimwili, ili kuwa na mwelekeo sahihi na mpana zaidi. Upendo ni zawadi ya ajabu inayofumbata utakatifu na tunu msingi za maisha! Vijana wawe na mwelekeo sahihi wa tendo la ndoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Vijana waheshimu na kuthamini tendo la ndoa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata ubikira ni kielelezo cha upendo na kwamba, ndoa na ubikira ni mielekeo miwili tofauti ya upendo. Wanandoa wanaendelea kuhamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaboresha mahusiano ya upendo wao kila siku kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

SURA YA TANO: Upendo unageuka kuwa ni asili ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anajikita katika mchakato wa mwendelezo wa maisha ya binadamu na ukarimu wa kupokea zawadi ya maisha mapya ndani ya familia. Kipindi cha mwanamke kubeba mimba ni muda wa ajabu sana hata kama wakati mwingine unakuwa na shida na changamoto zake. Huu ni wakati ambapo mwanamke anashirikiana na Mwenyezi Mungu katika kazi ya Uumbaji, kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu na kwamba, mtoto ana haki ya kuwa na baba na mama yake mzazi na hivyo kupata malezi na makuzi katika mazingira ya amani na utulivu. Baba Mtakatifu anawapongeza wanawake kwa mchango wao makini katika ustawi na maendeleo ya jamii pamoja na kuona mchango wa wanaume katika maisha na utume wa kifamilia.

Upendo wa kimama unaoneshwa pia katika kuasili mtoto na kwamba ni kitendo cha upendo kutoa mtoto kwa familia ambayo haikubahatika kupata mtoto. Taratibu, sheria na kanuni maadili zinapaswa kuzingatiwa ili kuepuka tatizo la utoaji mimba na kutelekezwa kwa watoto baada ya kuasiliwa! Hapa familia zinahamasishwa kujenga utamaduni wa watu kukutana; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki, umoja, udugu; kwa kuwalinda na kuwasaidia wanajamii wanyonge sanjari na kushuhudia imani na matumaini ya kweli. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupokea Ekaristi Takatifu kwa ukamilifu zaidi baada ya kutekeleza wajibu wao hasa kwa maskini.

Baba Mtakatifu anawashauri watoto kuwapenda, kuwaheshimu na kuwasaidia wazazi wao. Amri hii inajikita katika heshima kwa watu wote. Wazee wanapaswa kutunzwa na kuhudumiwa kwa heshima, kwani wao wana mchango mkubwa katika kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii, hawa ni hazina ya historia ya jamii. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu na kwamba, shule ni eneo muhimu sana katika ujenzi wa udugu, jamii na amani.  Wakwe nao waheshimiwe na kamwe wasibezwe anasema Baba Mtakatifu!

SURA YA 6. Baadhi ya mapendekezo ya shughuli za kichungaji.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa familia za Kikristo kupewa kipaumbele cha pekee kwa kutambua kwamba, hizi ni kiini cha shughuli na mikakati ya kichungaji. Mihimili ya Uinjilishaji haina budi kufundwa barabara ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao vyema katika maisha na utume wa Kanisa. Wanandoa watarajiwa waandaliwe vyema, dhamana inayotekelezwa hatua kwa hatua kwa kuwasaidia kutambua utajiri unaofumbatwa katika Sakramenti ya Ndoa, umuhimu wa fadhila ya useja pamoja na kujifunza kupenda kwa moyo wote.

Viongozi wa Kanisa wawe wepesi kung’amua kinzani zinazoanza kujitokeza kwa wanandoa wapya na kwamba, ndoa tata na zenye mashaka zisiruhusiwe kufungwa kamwe! Wanandoa wakati wa arusi yao wawe ni watu wa kiasi kwani jambo la msingi ni upendo na wala si mambo ya nje yanayoweza kunyauka na kupotea kama ndoto ya mchana! Kanisa liwaongozwe wanandoa wapya katika miaka yao ya kwanza kwanza ya ndoa; wasaidiwe kuonesha ukarimu kwa kupokea, kuitunza na kudumisha zawadi ya maisha; familia zisaidiwe kukua na kukomaa katika imani kwa kujenga na kuimarisha ari na mwako wa kimissionari.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna changamoto ambazo ni nyeti na daima kinzani zinalenga kuigawa familia, hapa ni kuangalia kila jambo kwani hata katika mazingira kama haya, kunaweza kuibuka jambo jema! Kanisa liwasaidie wanandoa kuvuka vipindi hivi kwa amani na utulivu. Talaka ni hatari ambayo inaendelea kukua na kuongezeka maradufu kwa nyakati hizi. Kanisa linapaswa kusaidia kuganga na kuponya madonda yanayoweza kusababisha talaka. Talaka liwe ni jambo la mwisho kabisa kufikiriwa na hasa pale linapoonekana kimaadili kuwa sahihi kabisa. Baba Mtakatifu anakemea tabia ya kutaka kuwabagua watu ndani ya Kanisa kutokana na hali zao. Wanandoa waliotengana na bila kuamua kuoa au kuolewa tena wahamasishwe kushiriki Ekaristi Takatifu na wale ambao wameoa au kuolewa tena wasijisikie kana kwamba, wametengwa na Kanisa, waoneshwe na kuonjeshwa upendo kama njia ya kuimarisha imani na udumifu wa ndoa.

Ndoa kati ya Wakatoliki na Wakristo wengine pamoja na Ndoa za mseto zinapaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; ingawa wakati mwingine kuna matatizo na changamoto kubwa hususan kuhusu malezi na makuzi ya watoto. Wakristo wanahamasishwa kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika maisha yao. Kwa watu wenye mwelekeo wa ushoga, waheshimiwe utu wao, wasibaguliwe lakini wakumbuke kwamba, ndani ya Kanisa hakuna ndoa ya watu wa jinsia moja na kwamba, hili ni jambo ambalo haliwezi kukubalika na Kanisa. Ndoa za jinsia moja lisiwe ni shinikizo la kisiasa kwa nchi maskini duniani kama sharti la kupokea misaada ya kiuchumi. Kifo kinapoingia ndani ya familia kinapaswa kupokelewa kwa mwanga wa imani na matumaini ya maisha ya uzima wa milele.

SURA YA 7. Kuimarisha elimu kwa watoto.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, elimu na malezi kwa watoto ni wajibu msingi kwa wazazi, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa hekima, busara na uhuru. Wazazi na walezi wawe na dhamiri nyofu na haki ya kuchagua aina ya elimu kwa watoto wao, ili waweze kufanya maamuzi makini wakati wanapokabiliwa na hali tete; wawasaidie kuwa na dira na mwelekeo chanya wa maisha. Malezi yawasaidie watoto kuwajibika katika kufanya maamuzi yao.

Elimu inapaswa kujikita pia katika subirá, jambo ambalo si rahisi sana katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambamo kuna mchaka mchaka wa maisha. Watoto wajengewe utamaduni wa kuomba msamaha pale wanapowakosea wengine, ili waweze kuwa na uhuru unaowajibisha. Elimu ya jinsia inalenga pamoja na mambo mengine, kumsaidia kijana kukua na kukomaa katika fadhila ya upendo badala ya kuwageuza watu wengine kuwa ni vyombo vya kuridhisha tamaa ya mwili.

Ngono salama inawajengea watu dhana dhana dhidi ya zawadi ya maisha! Watu wakubali na kujipokea jinsi walivyoumbwa na Mwenyezi Mungu; waheshimu na kuthamini tofauti zinazojitokeza, kwani yote haya ni kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha sura ya saba kwa kujikita katika umuhimu wa kurithisha imani, kwani familia inapaswa kuwa ni mahali pa kufundishia jinsi ya kupokea tunu na uzuri wa imani; mahali pa sala na huduma. Wazazi na walezi wawe ni vyombo na mashuhuda wa katekesi makini wanayoishuhudia na kuwafundisha watoto wao kuipokea katika uhuru kamili!

SURA YA NANE. Kuwasindikiza, kung’amua na kushirikisha familia dhaifu!

Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anapenda kujikita katika mambo makuu mawili: kwanza kabisa ni juu ya Mafundisho tanzu ya Sakramenti ya Ndoa na Nidhamu ya Sakramenti ya Ndoa. Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Ndoa ni kielelezo cha umoja na upendo wa Kristo kwa Kanisa lake, mwaliko wa kuwapokea, kuwasaidia na kuwasindikiza waamini wanaokabiliwa na matatizo na changamoto katika maisha ya ndoa na familia. Hapa kazi ya Kanisa inafananishwa na hospitali iliyoko kwenye uwanja wa vita.

Viongozi wa Kanisa waendelee kukazia mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa; wawe na mang’amuzi ya kichungaji kwa kesi maalum, ili kuamriwa kadiri ya tamaduni na mazingira ya watu husika. Lengo ni kufikia utimilifu wa maisha ya ndoa na familia mintarafu mwanga wa Injili! Njia ya Kanisa ni ile ambayo imeoneshwa kwa njia ya huruma, kwa kuwashirikisha waamini wote katika maisha na utume wa Kanisa bila ubaguzi wala kuwatenga. Hapa jambo la msingi ni kuwa na maamuzi makini kwa mtu mmoja mmoja na katika shughuli za kichungaji kwa ujumla wake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hakuna sheria au kanuni maalum inayotarajiwa kutolewa na Mababa wa Sinodi wala katika Wosia huu wa kitume kama sheria ya Kanisa inayoweza kutumika kwa watu wote. Waamini waliotalakiana wanapaswa kuchunguza dhamiri zao, ili kudumisha imani na matumaini yao kwa huruma ya Mungu. Mapadre kwenye kiti cha huruma ya Mungu wawasaidie waamini kuunda dhamiri nyofu, jambo linalohitaji unyenyekevu, usiri na upendo kwa Kristo, Kanisa na Sheria zake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kumekuwepo na giza nene la kufahamu sheria za Kanisa hali ambayo kimsingi inagumisha maamuzi: nyanyaso, hofu, ukosefu wa ukomavu katika upendo.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti inayopania kuwaimarisha wanyonge na wala si nishani kwa waamini wema na watakatifu! Baba Mtakatifu anawahimiza viongozi wa Kanisa kujikita katika sheria ya upendo na kukazia mafundisho yake sanjari na kuwa na sera na mikakati makini ya kuimarisha ndoa ili kuepuka mipasuko isiyokuwa na tija. Hakuna sababu ya kuhukumu, kushutumu wala kumtenga mtu, bali wote wanahamasishwa kuishi katika huruma ya Mungu inayomwambata kila mtu, bila kubeza Injili. Mikakati ya shughuli za kichungaji iwe na upendo wenye huruma, tayari kusaidia, kuelewa, kusamehe, kusindikiza, kuamini na kujumuishwa. Waamini wanaoishi katika mazingira tete wawe na ujasiri wa kuwaendea Mapadre au waamini walei ili hatimaye, waweze kupata mwanga utakaowasaidia kuelewa hali ya maisha yao. Mapadre wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini, upendo na utulivu, ili kuwasaidia kugundua nafasi yao katika maisha na utume wa Kanisa.

SURA YA TISA. Tasaufi ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu Francisko anakamilisha Wosia wake wa kitume, Furaha ya Upendo ndani ya familia kwa kuwaalika wanandoa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali kama njia muhimu sana ya kuimarisha maisha ya kifamilia, hususan nyakati za giza, kwani Fumbo la Msalaba linageuza mateso na machungu ya maisha kwa kutoa upendo. Familia zijikite katika tasaufi ya upendo huru unaobubujika kutoka katika sakafu ya moyo, ili kupyaisha kila siku uaminifu wa maisha ya ndoa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Familia iwe ni hospitali iliyo karibu zaidi inayowasaidia wanafamilia kuhudumiana na kuhurumiana; kwa kusaidiana ili kuandika kurasa safi zaidi za maisha ya kifamilia. Familia zijenge na kudumisha upendo na ukarimu; kwa kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujikita katika upendo wa kijamii, unaoshuhudiwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, chachu muhimu ya kuleta mabadiliko duniani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hakuna familia ambayo imekamilika, bali ukamilifu na utakatifu wa maisha ya familia ni mchakato endelevu unaojikita katika nia njema na udumifu. Familia kamili itaweza kupatikana mbinguni, kwani hapa duniani, familia inafanya hija ya kukuza na kuendeleza uwezo wake wa kupenda. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Wosia wake wa kitume Furaha ya Upendo ndani ya familia kwa kuwataka wanafamilia kusonga mbele bila kupoteza matumaini na mwishoni kabisa, anawapatia wanafamilia Sala ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu!

Wosia huu umehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.