2016-04-07 08:20:00

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani!


Kanisa tangu mwanzo limekuwa likitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinaritishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani.

Maadhimisho ya awamu mbili za Sinodi ya familia pamoja na Mkutano wa Familia Kimataifa uliofanyika Jimbo kuu la Philadelphia Marekani kuanzia tarehe 22- 27 Septemba 2015 ni ushuhuda makini unaoonesha jinsi ambavyo Kanisa linajitahidi kuwafunda watoto wake, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya huruma na mapendo ya Mungu kwa kuanzia ndani ya familia.

Kanisa linatambua kwamba, ndoa inaundwa na mahusiano thabiti kati ya bwana na bibi na wala hakuna mkanganyiko na mifumo mingine ya maisha inayopendekezwa na baadhi ya serikali kwa kutaka kuhalalisha hata ndoa za watu wa jinsia, kielelezo cha kukengeuka na watu kutaka kumezwa na utamaduni wa kifo! Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka mzima wa 2015 ametoa katekesi kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Waraka wa kichungaji wa Mtakatifu Yohane Paulo II, Injili ya uhai “Evangelium vitae” unaendelea kuwa ni hazina muhimu sana katika kukuza na kudumisha Injili ya uhai inayofumbatwa na kushuhudiwa katika Injili ya familia.

Baraza la Kipapa la familia, tangu kuanzishwa kwake, limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo laini na ndoa za watu wa jinsia moja, ni kati ya changamoto ambazo zimefanyiwa kazi na Baraza la Kipapa la familia, ili kutangaza na kushuhudia ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Kwa namna ya pekee, Askofu Marcello Semeraro wa Jimbo Katoliki Albano, nchini Italia anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwasha moto wa Injili ya familia katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, leo hii familia ni kati ya taasisi zinazokabiliwa na matatizo pamoja na changamoto nyingi sehemu mbali mbali za dunia. Wanafamilia wasimame kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia na kamwe wasikubali kuyumbishwa na mitandao ya kijamii na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kufaidika kutokana na myumbo wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kujijenga kisiasa na kiuchumi.

Mababa wa Sinodi wanaendelea kuwahimiza wanafamilia kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku katika ukweli na uwazi; unyofu na upole wa moyo. Lengo ni kuwawezesha wanafamilia kuendeleza hija ya maisha ya ndoa na familia huku wakiwa wameshikamana, licha ya kutambua matatizo na changamoto zinazowakabili baadhi ya wanafamilia. Kuna maendeleo makubwa ya dhana ya familia kama ilivyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kukazia kanuni maadili inayofumbata sheria. Leo hii kuna hatua moja mbele, yaani kanuni maadili inayofumbata sheria na maadili ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wanandoa wanaogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha, ili kuonja upendo na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa lioneshe ukaribu na watu hawa wanaoteseka: kwa kuwafahamu; kuwapokea na kuwadindikiza kwa huruma na upendo wa Mungu, tema inayopewa kipaumbele cha pekee wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Askofu Marcello Semeraro anakaza kusema, lengo ni kuwawezesha wanandoa kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kushuhudia Injili ya familia; ili kwa kushirikiana na watu wote wa Mungu, waweze kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kanisa kwa sasa linasubiri kwa hamu Waraka wa kichungaji kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuhusu Injili ya familia baada ya tafakari ya kina kuhusu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.