2016-04-06 10:38:00

Yaani tumeambulia patupu! Lakini kwa Neno lako tutashusha nyavu zetu!


Tunaadhimisha Dominika ya tatu ya Pasaka, ambapo Kanisa zima linaendelea kuufurahia ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi. Mwanadamu huyu ambaye alijeruhiwa kwa kiasi kikubwa na dhambi sasa amerudishiwa tena hadhi yake ya awali na zaidi amefanywa kuwa ni mwana mrithi wa Mungu. Tunaiadhimisha huruma ya Mungu. Hakika ni kwa huruma yake kuu ambayo ni jina lake ndipo Mwenyezi Mungu alipomtafuta tena mwanadamu, huyu kiumbe wake aliyemuacha na kumuasi na kumrudisha tena katika hadhi yake. Upendo wa Mungu unatamalaki dhidi ya hila za shetani. Mungu anaonesha ni nini maana ya upendo, yaani anaonesha jinsi ya kuwa tayari kutoka nje na kunuia mema kwa mwingine kinyume na husuda ya ibilisi shetani ambaye huanza kwa kulaghai kana kwamba anapenda lakini katika ukweli anajifikiria yeye zaidi kukua na kupanuka katika udhalimu wake.

Lakini uwepo wa Mungu baada ya Ufufuko wa Kristo ni wa kututia moyo na kutugutusha kwamba “imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”. Ni wazi kwamba tendo hili la ushindi wa uhai dhidi ya mauti ni pigo kwa shetani na ni lazima atatumia njia zozote za upinzani dhidi yake ili kuutokomeza. Jamii ya kiyahudi inataka kuuzima huu ukweli kwamba kweli amefufuka. Ni juhudi zao za kuipoteza kabisa habari ya Kristo mfufuka kusudi waendelee kulowea katika dimbwi la maisha maisha yao ya kale ambamo wanadhania wanamtumikia Mungu kumbe wanamtumikia shetani. “Mungu wa Baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi”. Ukuu wa upendo wa Mungu dhidi ya dhambi ya mwanadamu unadhihirishwa na hili. Mwanadamu katika hali ya dhambi anadhani kwamba anaweza kuzuia upendo wa Mungu usipenye katika jamii inayomzunguka.

 Jamii yetu inayotuzunguka leo imezingirwa sana na umambo sasa ambao daima unamtoa mwadamu katika kutenda kama anavyotaka Mungu bali kutenda kama anavyotaka mwanadamu. Hii ndiyo tabia ya mfumo wa kijamii inayoitwa usekulari, yaani ile juhudi ya kumwondoa Mwenyezi Mungu katika masuala yote yanayomuhusu mwanadamu. Kwa picha iliyofichika ndani kabisa ni upinzani juu ya uwepo wa Mungu na juhudi ya kumrudisha mwanadamu katika dhambi ya asili pale ambapo mwanadamu alitafuta “kuwa kama Mungu” ili aweze kuwa huru kuamua lililo jema na lililo baya katika maisha ya kila siku. Maandiko matakatifu yanatufunulia kwamba pale mwanadamu alimuondoa Mwenyezi Mungu katika maisha yake ya kila siku ndipo mwanzo wa anguko la mwanadamu na dhambi ikaingia katika ulimwengu. Mwanadamu huyu ambaye alitafuta kuwa huru akaangukia kuwa mtumwa wa shetani na kufuata maelekezo yake. Ndipo hapo ndugu kwa ndugu wakaanza kuchukiana na hata kuuana, uasherati na uzinzi ukaliangamiza taifa la Mungu, vita na mapigano baina ya mataifa yakaendelea kushamiri. Hakika uhuru huu alioutaka mwanadamu uligeuka kuwa uhuru bandia na hivyo kuwa ni utumwa.

“Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka ... Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo hata milele na milele”. Mwana-Kondoo huyu aliyechinjwa ndiye Kristo Mfufuka aliye kiongozi wetu na kichwa cha mwili wetu yaani Kanisa. Uweza wake unadhihirika kwa matendo makuu na huduma ya Kanisa kwa wanadamu. Kwa namna ya pekee katika mwaka huu anatualika kuitafakari hii huruma yake kuu na kuistawisha katika jamii yetu. Ni mwaliko tunaopata wa kuimbilia huruma hiyo, kuionja na sisi kuwa vyombo vya kuisambaza kwa watu wengine.

Matendo yetu kwa wenzetu na uwajibikaji wetu katika nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku unapaswa kuifunua huruma hiyo kwa wengine. Wakati wa Dominika ya Pasaka tulipewa mwaliko wa kumshuhudia Kristo Mfufuka. Tuuitikie mwaliko huo kwa kuiambia dunia kuwa kweli amefufuka na nguvu zake, adhama yake na enzi yake Yeye aliyechinjwa zinaonekana katika upendo wetu kwa wengine, msamaha wetu kwa wengine, huruma yetu kwa wengine na zaidi kwa utayari wetu wa kufunguka na kuwa vyombo vya kuieneza huruma ya Mungu.

Mtume Petro anapewa jukumu ya kulilinda na kulilisha kundi la Kristo. Jukumu hilo anakabidhiwa huku likiambatana na takwa la muhimu ambalo linaturudisha katika tafakari ya hapo juu: “Je, wanipenda kuliko hawa?” Hii inamaanisha kwamba juhudi za Kanisa katika kulinda na kulisha kundi zinapaswa kuongozwa na upendo thabiti kwake kuliko vitu vingine. Ni ufafanuzi kwetu kwamba pale tunapotaka kufanya chochote nje ya upendo huo wa kimungu mara zote tunaishia kuanguka. Injili inatuambia kwamba: “Wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu”. Hii ni ishara ya Kanisa linalotaka kutenda peke yake na kuusahau upendo wa Kristo. Giza pia linawakilisha jamii ambayo inakosa uwepo wa kimungu. Lakini pale Kristo anapokuwa katikati yao na wao kuisikiliza sauti yake wanapata samaki wengi, wakubwa na wa kutosha: “Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki”.

“Je, wanipenda kuliko hawa?” Ni mwaliko wa kumtamalakisha Mwenyezi Mungu katika kila jambo. Yeye ambaye asili yake ni upendo anapenda kuishi katika nafsi ya kila mmoja kusudi mwisho Yeye awe yote katika yote. Katika ukomavu wetu wa kikristo tunapaswa kuelekea katika hali hiyo ambayo inatutoa katika vilema vyetu vya kimwili, ambayo inatuondoa katika tamaa zetu za kibinadamu na ambayo inatunasua kutoka katika kongwa la utumwa wa shetani. Ukristo unapaswa kuwa ni mshangao katika jamii ya mwanadamu. Pale tunapojikuta tumesawazishwa na maisha ya kawaida ya kijamii ni udhihirisho kwamba bado tunadaiwa kufanya zaidi, tunagutushwa kwamba tumeisahau njia yetu na upendo wetu kwa Kristo umepotea. Lakini Yeye katika huruma yake kuu anaendelea kutuuliza, “Je, wanipenda kuliko hawa?” Je, unampenda kuliko raha na starehe za kidunia?, je, unampenda kuliko vyeo na umaarufu? Je, unampenda kuliko mali za ulimwengu huu?

Tutafakari Dominika hii jukumu letu la kuwa mashahidi wa maisha ya Ufufuko. Hii ndiyo bendera ya kuutambulisha ukristo ili Mwana-Kondoo aliyechinjwa apokee uweza na utajiri na hekima na nguvu na na heshima na utukufu na baraka. Katika ujasiri mkubwa tuuambie ulimwengu kwamba tunapaswa kumtii zaidi Mungu kuliko mwanadamu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.