2016-04-06 07:56:00

Kumbu kumbu ya mauaji ya wanafunzi wa Chuo kikuu cha Garissa, Kenya!


Askofu Joseph Alessandro wa Jimbo Katoliki Garissa, nchini Kenya, Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe 3 Aprili 2016 ameadhimisha kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Chuo kikuu cha Garissa kiliposhambuliwa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab na hivyo kusababisha vifo vya wanafunzi 148, wengi wao wakiwa ni wanafunzi Wakristo!

Ni matumaini ya Askofu Alessandro kwamba, iko siku magaidi hawa wataweza kutubu na kumwongokea Mungu kwa kuachana na vitendo vinavyopandikiza mbegu ya kifo na badala yake kujenga jamii inayojikita katika udugu, haki, amani, huruma na heshima na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali! Askofu Alessandro anasema, Sala yao itaweza kusikilizwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, katika maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu ametolea nia na maombi yake kwa wale wote wanaoendesha vitendo vya kikatili dhidi ya Wakristo nchini Kenya na sehemu mbali mbali za dunia ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu.

Askofu Alessandro ameitia shime familia ya Mungu Jimboni Garissa kuendelea kushikamana katia imani, matumaini na mapendo! Anaishukuru na kuipongeza Serikali ya Kenya kwa kuimarisha ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Hali imekuwa shwari wakati wa maadhimisho ya Sikuu ya Pasaka na kwamba, amani na utulivu vinaendelea kutawala miongoni mwa wananchi. Hata hivyo, bado kuna wasi wasi kwamba, vitendo vya kigaidi vinaweza kufanywa tena kama tabia ya kutaka kulipiza kisasi.

Askofu Alessandro anawapongeza waamini wake kwa kuonesha imani thabiti, jambo ambalo linamtia nguvu pia katika maisha na utume wake Jimboni Garissa. Kipindi chote cha Kwaresima, Juma kuu na Pasaka ya Bwana, Makanaisa yalisheheni waamini waliofika kusali kwa ibada na uchaji pasi na woga wa mashambulizi ya kigaidi.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Martin Musonde Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa katika mahojiano maalum na Shirika la Kipapa la Kanisa hitaji anasema, familia ya Mungu nchini Kenya ilishikwa na simanzi na huzuni kubwa wakati wa kuwaombea wanafunzi waliokuwa wameuwawa kikatiliki kwenye Chuo Kikuu cha Garissa. Hivi karibuni, viongozi mbali mbali wa kidini nchini Kenya wametoa tamko la kulaani vitendo vyote vya kigaidi na kuwataka wananchi kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa!

Askofu mkuu Kivuva anakaza kusema, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika elimu kwa vijana nchini Kenya ili waweze kuwa na msimamo bora katika maisha na matumaini ya kupata fursa ya ajira: Pasi na elimu na ajira makini, vijana wengi wanaweza kutumbukia katika vitendo vya kigaidi kwa kudhani kwamba, wanaweza kupata “fedha ya chapuchapu” na hivyo kuupatia umaskini kisogo!

Viongozi wa kidini nchini Kenya wamewataka wanasiasa wanaotaka kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu unaoratajiwa kufanyika nchini Kenya kunako mwaka 2017 kujenga na kudumisha demokrasia ya kweli, umoja na mshikamano wa kitaifa badala ya kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kwa kutumia ukabila, umajimbo na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.