2016-04-05 14:38:00

Sikukuu ya Maria Kupashwa Habari ni Siku Kuu ya kusema Ndiyo


Baba Mtakatifu Francisko, ameanza tena utaratibu wake wa kuongoza Ibada za Misa za asubuhi katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta baada ya kusitisha utaratibu huo, kwa wiki kadhaa kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki Takatifu la Pasaka. Jumatatu, katika homilia yake ya kwanza , amemtaka kila Mkristo kujihoji iwapo yu tayari kutoa jibu la ndiyo katika ujumbe wa wokovu wa Yesu, au kama yu  mtu wa kujiweka mbali na jibu. Homilia ya Papa ililenga katika Maadhimisho ya Siku Kuu ya Maria Kupaswa Habari na Malaika kwamba atamzaa Mwana wa Mungu kwa nguvu za Roho Mtakatifu.  Papa alieleza kwamba , ndiyo ya Maria, iliufungua Mlango wa wokovu ulioletwa na Yesu.

Papa aliendelea kutafakari uzito wa neno 'ndiyo' katika Maandiko Matakatifu, akiyarejea masomo  ya siku  akisema , pia Abraham alimtii Bwana, kwa kusema "ndiyo"  katika wito uliomtaka aondoke katika nchi yake bila kujua anakoplekwa, na aliendelea  kutaja  neno ndiyo  katika  mlolongo wa Maandiko Matakatifu. Kwa upande wa Sikukuu ya Maria Kupaswa habari, alikumbuka kwamba '' ubinadamu wa wanaume na wanawake  na wahenga kama ilivyokuwa kwa  Ibrahimu au Musa," walisema ndiyo  katika kumtumaini Bwana. Na pia aliwataja wale waliojiona kuwa hawana mastahili ya kupeleka ujumbe wa Bwana kwa kuwa hawako safi, walioomba kwanza kutakatifushwa kama ilivyotajwa katika somo la Isaya: ambamo  wakati Bwana anamwambia kwenda na kuwahubiri watu , anasita akisema  ana "midomo michafu".

Bwana, aliitakasa midomo ya Isaya, na ndipo Isaya akasema ”ndiyo!". Na ndivyo ilivyokuwa kwa Yeremia kwanza alionyesha udhaifu wake kwamba hana uwezo wa kuongea, lakini kisha akasema 'ndiyo' kwa Bwana:

Homilia ya Papa baada ya kutazama Maandiko Matakatifu mengi katika Agano la Kale, alirejea tena katika Injili ya Siku akisema ni mwanzo mwingine  wa 'ndiyo', iliyoanzishwa na Maria. Na kwamba, Mungu hupokea "ndiyo"  ya mtu si katika mtazamo wa kibiandamu na wala si kwa wateule wake tu , lakini kwa kila anayekubali kuwa mfuasi wa Kristo, aliyeuchukua mwili wetu.  'Ndiyo' ya  Bikira Maria , inayofungua Mlango wa kusema ndiyo kwa Yesu: 'Nimekuja kufanya mapenzi yako. Na alifafanua maana ya kusema ' ndiyo hiyo' kwamba ni kukubali kutembea na Yesu wakati wote wa maisha hata katika vipindi vigumu vya maisha.  

Baba Mtakatifu Francisko pia aliitafakari pia ndiyo ya Yesu wakati akiomba kwa Baba yake,amwondolee kikombe cha mateso,  lakini aliongeza  "Utakalo lifanyike".  Kumbe kwa  Yesu Kristo, tunajifunza kusema pia 'ndiyo'  kwa  Mungu, kwa kuwa Yeye ndiye  'ndiyo'".

Baba Mtakifu ameeleza na kuyataja maadhimisho ya Skukuu hii ya Maria Kupaswa habari  kuwa ni  Siku nzuri  ya kumshukuru Mungu,  kwa kuwa inatufundisha kutembea katika 'barabara ya Ndiyo. Ni siku nzuri ambamo tunapaswa kufikiri vyema  juu ya maisha yetu. 

Papa kwa  namna ya kipekee aliwakumbuka Mapadre waliokuwa katika Ibada hiyo ambao baadhi yao walikuwa wanaadhimisha miaka 50 ya Upadre . Kwao wote alimtaka kila mmoja wao kila siku kufikiri vyema na kutoa jibu lake la kweli , au ndiyo au hapana. Ni kusema 'ndiyo' au hapana kwa  mara nyingine bila ya kujificha ficha kama alivyofanya Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni. Aliogopa kutoa jibu bayana  kwa Bwana alipomwita. Papa alisema na ndivyo wengi tunavyofanya tunataka kumsubirisha kwa muda jibu letu kwa kisingizio bado sijaelewa kile Mungu anachotaka nifanye.  Papa alieleza na kuitaja Sikukuu ya hii kuwa ni  Sikukuu ya ”Ndiyo”, inayohimiza kutoa jibu mara kama ilivyokuwa kwa Maria. Na kwamba  katika 'ndiyo' ya Maria   mna 'ndiyo' ya historia nzima ya wokovu, na mna mwanzo na mwisho wa 'ndiyo' ya binadamu na ya Mungu.

Papa alikamilisha homilia yake kwa kuomba majaliwa ya Bwana,  yawawezeshe wote wake kwa waume kupata neema ya kuingia katika njia hii ya “ndiyo “ kutembea pamoja na wanawake na wanaume wanaosema “ndiyo kwa Bwana. Kisha aliwakumbuka  Masista wa Mtakatifu Vincent wanaotoa huduma katika Jengo la Mtakatifu Marta waliokuwa wanarudia  upya kukiri nadhiri zao, kusema tena ndiyo katika kumtumikia Bwana , kama wanavyotakiwa kurudia ahadi hiyo kila mwaka. 








All the contents on this site are copyrighted ©.