2016-04-05 14:39:00

Nigeria kumekucha! Khalid Al Barnawi atiwa mbaroni!


Serikali ya Nigeria inaendelea kupata ushindi dhidi ya kikundi cha magaidi cha Boko Haram kwa kumkamata kiongozi mkuu wa Boko Haram Ansaru, Khalid Al Barnawi, katika operesheni maalum iliyofanywa vikosi vya ulinzi na usalama huko Lokoja, mkoani Kogi. Msemaji wa Jeshi la ulinzi na usalama nchini Nigeria, Siku ya Jumatatu tarehe 4 Aprili 2016 amesikika akisema kwamba, zoezi hili ni matunda ya ushirikiano wa dhati kati ya vikozi mbali mbali vya ulinzi na usalama nchini Nigeria.

Taarifa zinaonesha kwamba, Khalid Al Barnawi ni kati ya viongozi wakuu kwenye mitandao ya kigaidi Barani Afrika. Inasemekana kwamba, ana uhusiano na mawasiliano pia na vikundi vingine vya kigaidi vilivyoko Afrika ya Kaskazini na huko Mashariki ya Kati. Kuanzia mwaka 2012 amekuwa ni kati ya magaidi wanaotafutwa kwa udi na uvumba na Serikali ya Marekani. Boko Haram imekwisha sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao ndani na nje ya Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.