2016-04-05 12:00:00

Ni kipindi cha kuandika Injili ya huruma ya Mungu!


Huruma ndilo jina la Mungu wetu ni changamoto inayoendelea kufanyiwa kazi na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ndio ule muda uliokubaliwa wa kumwilishwa ujumbe wa huruma kwa watu wa nyakati hizi kama walivyofanya Mtakatifu Yohane XXIII, aliyelitaka Kanisa kutibu na kuwaganga walimwengu kwa kutumia dawa ya huruma.

Baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wazo hili likavaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyeonja machungu ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, akashuhudia mateso ya Auschwitz na utawala wa Kikomunisti nchini Poland. Leo, hii walimwengu wanakabiliwa na wasi wasi na hofu ya vita; mashambulizi ya kigaidi, maafa na majanga asilia, lakini mbaya zaidi ni utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu, Kanisa linaalikwa kuwa ni Hospitali katika uwanja wa mapambano, ili kujibu kilio cha watu wa nyakati hizi! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Kardinali Walter Kaspar wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Huruma ya Mungu Barani Ulaya.

Kardinali Kasper amepembua kwa kina na mapana dhana ya huruma ya Mungu katika Maandiko Matakatifu kwa kumwonesha  kuwa ni Mungu anayeona mateso na mahangaiko ya watu wake, kama alivyojifunua kwa Musa; Ni Mungu anayesikiliza kwa makini na ni Mungu anayeongoza hatima ya maisha ya binadamu! Ni Mungu anayefanya hija na mwanadamu katika historia ya maisha yake: Ni mwingi wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira na kwamba, huruma ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha haki ya Mungu anayethubutu kusamehe na kusahau. Hii ndiyo changamoto kubwa ambayo waamini wanahamasishwa kuimwilisha katika maisha yao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Kardinali Kasper anaendelea kufafanua kwamba, katika Agano Jipya, kwa namna ya pekee, Mungu amejifunua kama upendo ambao umeshuhudiwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Upendo na huruma ya Mungu inawahamasisha waamini kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma!

Hii ni huruma inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwani Mungu ni upendo, “Deus Caritas est”. Kwa njia ya huruma, Mwenyezi Mungu analifunua Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kuonesha: Ukuu na Utakatifu; Wema na Ukarimu wa Mungu katika mateso na mahangaiko ya binadamu. Ieleweke wazi kwamba huruma inamwilishwa katika uhalisia wa historia na maisha ya watu! Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu aliyamimina kabisa maisha yake, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu! Ni huruma inayosamehe na kutoa dira na mwelekeo mpya ya matumaini! Huruma inaokoa, inaganga na kuponya madonda ya binadamu na hivyo kumkirimia matumaini mapya. Hapa huruma na ukweli vinakumbatiana na kubusiana. Huruma haiondoi kweli za imani, bali inapyaisha mchakato wa Uinjilishaji mpya. Haki na huruma ni mambo muhimu sana katika maisha ya watu!

Kardinali Kasper anakaza kusema, tasaufi ya huruma ya Mungu inapaswa kuwasaidia viongozi wa Kanisa kuwa na mbinu mkakati makini katika shughuli zao za kichungaji ili kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu; kuadhimisha Sakramenti za huruma ya Mungu yaani: Ekaristi takatifu na Upatanisho kwa uchaji na ibada; ushuhuda katika kuongoza kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma.

Matendo ya huruma kiroho na kimwili yawasaidie waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mama Theresa wa Calcutta na mashuhuda wengine wengi wa Injili ya huruma ya Mungu. Huruma ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linapaswa kujikita katika mchakato wa Umissionari! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni chachu ya upyaisho wa maisha ya Kanisa mintarafu maelekezo yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa liendelee kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kushikamana na kuwasaidia maskini wa kiroho na kimwili; haki, amani na upatanisho wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.