2016-04-05 09:04:00

Iweni na huruma kama Baba!


Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha wema, upendo na ukarimu kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Familia ya Mungu inapaswa pia kuwa na ujasiri wa kukemea uvunjwaji wa haki msingi za binadamu dhidi ya  Zingari, ambao wanabaguliwa na kutengwa na wengi. Hili ni kundi la jamii linalopaswa kuonjeshwa upendo na mshikamano.

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Antonio Maria Vegliò kwa wajumbe wa Kamati ya Kanisa Katoliki Kimataifa kwa ajili ya Zingari katika mkutano wake unaotarajiwa kufunguliwa rasmi hapo tarehe 8 – 10 Aprili 2016 huko mjini Esztergom nchini Hungaria. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Makutano: Ulaya, Kanisa na tamaduni mbele ya huruma ya Mungu”.

Wakristo wanahamasishwa kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma. Wajitahidi kuwa kweli ni chemchemi ya huruma na mapendo katika familia, parokia na kwenye jumuiya na vyama vya kitume! Kwa njia hii Wakristo watakuwa wanashiriki katika mchakato wa kuendelea kuandika Injili ya huruma ya Mungu, kielelezo makini cha Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha! Shughuli mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa kwa wakati huu zinapaswa kuratabiwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; Iweni na huruma kama Baba! “misericordes sicut Pater”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.