2016-04-04 07:48:00

Hali ya wananchi wa Ukraine inatisha!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wa Kanisa Katoliki Barani Ulaya, tarehe 24 Aprili 2016 kumuunga mkono katika kukusanya mchango maalum kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ukraine ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe! Kuna idadi kubwa ya wananchi wa Ukraine wanaohitaji msaada wa dharura, hasa chakula na huduma ya afya!

Takwimu zinaonesha kwamba, wanawake wajawazito wako hatarini zaidi kuambukizwa magonjwa kama vile UKIMWI na Kifua Kikuu, ambayo yameongezeka kwa kasi kubwa wakati huu wa vita. Huduma ya afya imefifia kiasi cha kukatisha tamaa. Hali hii pia inachangiwa na ukosefu wa uhakika wa maji safi na salama kwa zaidi ya wananchi millioni moja na laki tatu! Nishati ya umeme na gasi inatolewa kwa mgawo! Zaidi ya watoto laki mbili wanaishi kama wakimbizi pasi na usimamizi wa wazazi wao.

Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Ukraine ni asilimia 10% ya idadi ya wananchi wote wa Ukraine. Kanisa kwa wakati huu limekuwa kweli mstari wa mbele kuiwasaidia waathirika wa vita inayoendelea huko Ukraine. Mchango utakaotolewa na waamini wa Kanisa Katoliki Barani Ulaya utadhibitiwa na Mashirika ya kitawa na utaelekezwa kwa wananchi wote pasi na ubaguzi. Hapa nia ni kuendeleza pia Uekumene wa huduma ya upendo, kumbe, viongozi wa Makanisa pia watashirikishwa katika kugawa msaada huu, utakaosimamiwa na Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.