2016-04-03 11:59:00

Tarehe 24 Aprili 2016 Majimbo Katoliki Ulaya kuchangia Ukraine!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe 3 Aprili 2016, wakati wa Sala ya Malkia wa mbingu amesema, Jumapili hii ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale watu wa mataifa wenye kiu ya upatanisho na amani. Amewakumbuka wananchi wa Ukraine; wanaoendelea kubaki katika nchi yao ambayo imegeuka kuwa uwanja wa vita na vurugu.

Baba Mtakatifu anawakumbuka wakimbizi na wahamiaji zaidi ya millioni moja kutoka Ukraine wanaokabiliana kwa sasa na hali ngumu ya maisha! Katika mazingira vita na kinzani za kijamii, waathirika wakuu ni wazee na watoto. Ili kuonesha mshikamano wa umoja na upendo, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Jumapili ya tarehe 24 Aprili 2016 kufanyike mchango maalum kutoka kwa Majimbo Katoliki Ulaya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Ukraine.

 Baba Mtakatifu anawasihi waamini kuchangia kwa moyo wa upendo na ukarimu ili kuweza kuwasaidia wananchi walau kupata mahitaji yao msingi sanjari na kuonesha mshikamano wake wa karibu na Kanisa la Ukraine. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, changamoto hii itasaidia kukoleza mchakato wa kutafuta haki na amani nchini Ukraine, ambako wananchi wamejaribiwa na kutikiswa sana!

Wakati Kanisa bado linaendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, Jumatatu tarehe 4 Aprili 2016, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya Mabomu ya kutegwa ardhini. Watu wengi wanaendelea kupoteza maisha au kupata vilema kutokana na mabomu haya ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.