2016-04-03 12:23:00

Kimbilieni kwenye Madonda Matakatifu ya huruma ya Mungu!


Ilikuwa ni tarehe 2 Aprili 2005 katika mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alipofariki dunia, muasisi wa Jumapili ya huruma ya Mungu aliyoianzisha kunako mwaka 2000 kwa kufuata ushuhuda uliotolewa na Mtakatifu Faustina Kowalska. Maadhimisho ya Mwaka huu yamewakusanya waamini na vyama vya kitume vyenye Ibada kwa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni, tarehe 2 Aprili 2016 ameadhimisha mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu na katika tafakari yake, amewashukuru waamini na vyama vyenye Ibada kwa huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini kuendelea kujibidisha kumtafuta, kumpokea na kuonesha hamu ya kukutana naye! Hili ni jambo linalowashangaza wengi kwa kumwona Mungu akiwaendea waja wake ili kuwashirikisha upendo mkuu. Jina la Mungu ni huruma ambayo haina kifani.

Huruma ya Mungu inajionesha kwa namna ya pekee kutokana na ukaribu wa Mungu kwa watu wake unaojidhihirisha kama msaada na ulinzi unaofumbatwa katika vifungo vya upendo kama wafanyavyo wazazi kwa watoto wao. Mwenyezi Mungu anamwinua kila mtu na kumpandisha ili kumwonjesha upendo wake usiokuwa na mipaka! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, neno upendo, leo hii linalonekana kupitwa na wakati.

Nembo ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu inamwonesha Yesu akiwa amewabeba watu mabegani mwake, huku shavu lake likiwa linakaribiana kabisa na lile la Adamu  kiasi kwamba nyuso hizi mbili zinaonekana kana kwamba, zimekuwa ni kitu kimoja! Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na kwa nguvu ya huruma yake, Neno wa Mungu amefanyika mwili katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa kutenda dhambi.

Kwa njia ya Kristo Yesu, binadamu anaweza kugusa kwa namna ya pekee huruma ya Mungu ambayo inamhamasisha kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni rahisi sana kuzungumzia kuhusu huruma ya Mungu, lakini ni vigumu kuimwilisha katika matendo! Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu mchakato ambao ni endelevu katika maisha yao yote hapa duniani; iweni na huruma kama Baba wa mbinguni! Hii ni kauli inayojikita katika maisha yote ya mwamini!

Uso wa huruma ya Mungu unajionesha kwa namna ya pekee kabisa katika: upendo na ushirikiano; faraja na msamaha; mambo ambayo waamini wanapaswa kuwashirikisha jirani zao katika hija ya maisha yao ya kiroho. Waamini wawe na ujasiri wa kuutambua Uso wa Kristo miongoni mwa wageni, wanyonge, wapweke, waliochanganyikiwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Huruma ya Mungu ni mchakato unaowatafuta wale waliopotea na kumezwa na malimwengu na kwamba, kila mtu ana thamani kubwa mbele ya Mungu!

Inasikitisha kuona watu wakiwatelekeza maskini barabarani kwani kufanya hivi ni kinyume kabisa cha huruma ya Yesu inayoendelea kuwawajibisha waja wake, ili kuwapatanisha wengine na Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kuwa tayari kutambua uso wa huruma ya Mungu kwa jirani zao. Mtakatifu Tomaso alikuwa na imani haba! Hakuamini kwamba Kristo amefufuka kwa wafu hadi pale alipotia mkono wake kwenye makovu ya misumari mikononi mwa Yesu na ubavu wake uliotobolewa kwa mkuki! Na kwa mikono yake, Tomaso akagusa huruma ya Mungu ambayo ni kiini cha imani ya Kanisa, huyu ni Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake.

Ni Mungu aliyeonesha mshikamano na wadhambi, akainama na kumhudumia mwanadamu katika udhaifu na mapungufu yake. Imani ya kweli iwawahamasishe waamini kukimbilia kwenye madonda ya huruma ya Mungu kwa binadamu ili kuonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kuumwilisha kwa wale wanaouhitaji. Roho Mtakatifu awasaidie waamini kutembea katika njia ya upendo na huruma inayokita mizizi yake katika mioyo ya watu! Waamini wawe na ujasiri wa kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu kwa unyenyekevu na kwa njia hii, Roho Mtakatifu atawajalia wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho! Kwa kuingia katika madonda yake matakatifu, waamini wawe kweli ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka anayeendelea kuishi kati yao!

Mwishoni mwa Ibada ya Mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini pamoja na Maaskofu wao mahalia kujadili kwa kina na mapana jinsi ambavyo wataweza kuwa na kumbu kumbu endelevu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kujikita katika ujenzi wa nyumba ya watoto yatima, wazee, maskini; watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hospitali au zahanati. Kwa njia hii, mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu utaendelea kuwa hai katika akili na nyoyo za watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.