2016-04-02 15:30:00

Wafungwa wa kisiasa nchini Uganda waachiliwe huru!


Askofu John Baptist Kaggwa wa Jimbo Katoliki Masaka, Uganda amewataka Waganda wote kuzika tofauti zao na kuanza kuchuchumilia mchakato wa umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa ili kuunganisha nguvu katika kujenga nakudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu! Askofu Kaggwa ameyasema haya wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa kuitaka Serikali kuwaachia huru wanasiasa wa upinzani, kwani uchaguzi nchini Uganda umekamilika, changamoto iliyoko mbele yao ni kuendeleza nchi huku wananchi wakiwa wameshikamana kwa dhati!

Askofu Kagwa anasema, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Uganda kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Dr. Kizza Besigye wa Chama cha FDC, “Forum for Democratic Change” amezuiliwa nyumbani kwake tangu tarehe 18 Februari 2016 wakati wa uchaguzi mkuu nchini Uganda uliofanyika mwezi Februari na hatimaye matokeo kutangazwa na kumpatia Rais Yoweri Kaguta Museveni ushindi wa asilimia 60.62 wa idadi zote za kura halali zilizopigwa katika uchaguzi huo. Dr. Besigye alijipatia asilimia 35.61 ya kura zote halali zilizopigwa.

Changamoto kwa Serikali ya Uganda kumwachia huru Dr. Besigye imetolewa pia na viongozi mbali mbali wa Kikristo nchini Uganda wakati wa Shereheza Pasaka kwa mwaka 2016. Hawa ni Askofu mkuu Stanley Ntagali; Askofu Johnson Gakumba kutoka Jimbo la Uganda ya Kaskazini aliyetaka Rais Museveni kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mpinzani wake wa jadi Dr.  Besigye na kuangalia jinsi ambavyo wanaweza kulisaidia taifa kusonga mbele badala ya mkwamo wa sasa unaohatarisha amani na mafungamano aya kijamii nchini Uganda.

Wakati huo huo vyombo vya ulinzi na usalama nchini Uganda vimenukuliwa vikisema kwamba, Dr. Besigye ataweza kuachiliwa ikiwa kama atakiri kosa la kuvuruga kampeni za uchaguzi mkuu nchini Uganda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.