2016-04-02 15:03:00

Ugonjwa wa mtindio wa ubongo unahitaji sera makini!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wafanyakazi katika sekta ya afya, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Watu wenye Mtindio wa Ubongo, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Aprili, amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni wajenzi na mashuhuda wa matumaini kwa watu wanaoteseka kutokana na ugonjwa huu. Wadau mbali mbali waoneshe sera na mbinu mkakati ya kuwasaidia wagonjwa hawa kwa vitendo!

Lengo la kuanzishwa kwa siku hii ni kuwawezesha watu kuwa na ufahamu kuhusu ugonjwa huu ili kuweza kuwahudumia wagonja kwa upendo na matumaini pasi na kuogopa kwani Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kwa wafu! Kumbe, Kristo mfufuka awe ni chemchemi ya faraja na matumaini kwa wagonjwa wenye mtindio wa ubongo.

Matumaini haya yajengwe na kudumishwa kwenye familia, wafanyakazi wa sekta ya afya, vyama vya sayansi ya tiba ya mwanadamu, taasisi pamoja na watu wa kujitolea. Jambo la msingi ni kuendelea kuboresha huduma za afya pamoja na kuendeleza tafiti mbali mbali ili kuwaza kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa mtindio wa ubongo pamoja na familia zao, ili kuwajengea matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, matumaini ya Kikristo yanapata chimbuko lake katika Fumbo la upendo wa Mungu kwa mwanadamu ambalo limedhihirishwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu, changamoto kwa waamini kukimbilia uso wa huruma ya Mungu.

Askofu mkuu Zimowski anawashauri waathirika wa ugonjwa huu kuendelea kuwa na matumaini katika huruma ya Mungu inayomwilishwa katika huduma makini kwa wagonjwa na familia zao. Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Baraza la Kipapa la wafanyakazi katika sekta ya afya liliandaa kongamano la kimataifa kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali ili kuwajengea watu matumaini, ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati.

Kuna haja ya taasisi za elimu kushirikiana na sekta ya afya ili kuwajengea wagonjwa wa mtindio wa ubongo uwezo wa kujitegemea wenyewe pale inapowezekana. Hii ni dhamana nyeti na inayowezekana kutekelezwa na wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anapenda kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kukuza moyo wa upendo na mshikamano; umoja na udugu; kwa kuwapokea na kuwasaidia maskini na wale wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha. Lengo kuu ni kuwawezesha watu kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.