2016-04-02 16:10:00

Sakramenti za huruma ya Mungu!


Padre Wojciech Adam Koscielniak kutoka Kituo cha Hija ya huruma ya Mungu Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Mapadre ni wahudumu na mashuhuda wa Sakramenti za huruma ya Mungu kwa waja wake.

Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho mwamini anaonja na kusikia huruma ya Mungu katika maisha yake, kwani Mungu ni mwingi wa rehema na kwa mapenzi yake makuu anampenda mwanadamu, hata pale anapokuwa mfu kutokana na dhambi zake, bado Mungu anaendelea kumpenda na kumpatia nafasi ya kutubu, kuongoka na kuanza upya hija ya maisha yake ya kiroho. Mdhambi aliyetubu na kuungama dhambi zake vyema, anarudisha mahusiano na Kristo Mfufuka na hivyo kuendeleza ile neema ya Utakaso aliyoipokea wakati wa Sakramenti ya Ubatizo.

Mapadre ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho, ambayo wanapaswa kuiadhimisha kwa kuvaa sura ya Baba mwenye huruma! Ikiwa kama Padre anajisikia kuwa na hasira, ni afadhali asiende kwenye kiti cha huruma ya Mungu kwani anaweza kuwakwaza waamini, aliwahi kusema Baba Mtakatifu Francisko wakati akizungumza na Wamissionari wa huruma ya Mungu alipokutana nao mjini Vatican.

Waamini wajibidishe kuitafuta na kuambata huruma ya Mungu kwa kutumia kiti cha huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni sakramenti inayomponya mwamini kutokana na dhambi zake na kwa njia ya kitubio mwamini anaelimishwa mambo msingi ya kuzingatia katika hija ya maisha yake ya kiroho! Waamini waendelee kuwaombea Mapadre wao ili kweli wawe ni watu wenye moyo wa huruma kwa waamini wao; wawe ni waungamishaji bora wanaogawa Mafumbo ya Kanisa kwa moyo radhi, sadaka na majitoleo. Wadhambi watubu na kumwongokea Mungu!

Padre Wojciech Adam Koscielniak anaendelea kufafanua kwamba, sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake, chemchemi ya huruma na mapendo! Hapa Wakristo wanahamasishwa kuwa ni Ekaristi, yaani mkate uliomegwa kwa ajili ya jirani zao kwa njia ya huduma makini. Kumbe, Mapadre wawasaidie waamini katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi, ili waweze kujichotea huruma na mapendo ya Kristo kutoka katika Sakramenti hii kuu na ya ajabu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.