2016-04-02 13:34:00

Kardinali Cottier alikuwa ni shuhuda wa imani!


Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumamosi tarehe 2 Aprili 2016 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Kardinali Georges Marie Martin Cottier, mwanataalimungu mstaafu wa nyumba ya kipapa, aliyefariki dunia hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 93. Baada ya Misa takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya mazishi ya Kardinali Cottier iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kardinali  Sodano katika mahubiri yake, kwa namna ya pekee amefanya kumbu kumbu ya maisha na utume wa Kardinali Cottier, aliyejitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kueneza Ufalme wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Marehemu Kardinali Cottier alitangaza na kushuhudia imani ya Kikristo! Katika maisha na utume wake, alijitahidi kuwasaidia watu ili waweze kumfahamu Kristo kwa kuona kile ambacho kimefichika machoni pa wengi!

Marehemu Kardinali Cottier ni mwanataalimungu nguri, aliyebobea katika maandiko ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, akabahatika kuona matukio mbali mbali katika maisha na historia ya mwanadamu kwa jicho la imani. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambi rambi, alimshukuru Mungu kwa kumwezesha Kardinali Cottier kuwahudumia kwa umakini mkubwa Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI kama mwanataalimungu wa nyumba ya kipapa.

Kwa kifo cha Kardinali Cottier, idadi ya Makardinali inakuwa ni 215 kati yao 116 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wengine 99 hawana haki ya kupiga wala kupigiwa kura kutokana na Sheria za Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.