2016-04-02 15:18:00

Jengeni na kudumisha umoja wa Kitaifa Rwanda!


Viongozi wa Makanisa mbali mbali nchini Rwanda wametumia maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kuwataka wananchi wote kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani, haki, amani na upatanisho; mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kwa njia hii waamini wataweza kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kilele cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu! Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Thaddèè Ntihinyurwa wa Jimbo kuu la Kigali, Rwanda anasema, Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti na amefufuka kwa wafu, changamoto na mwaliko kwa waamini kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, huku wakijitahidi kutenda mema, Yesu alionesha uso wa huruma ya Baba wa milele kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake yaliyogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili.

Yesu aliwasamehe wadhambi, aliwaponya wagonjwa, akawafufua watu na kuwalisha wenye njaa! Yesu alikuwa ni mtu wa sala na tafakari, alifunga Jangwani kwa kipindi cha Siku 40, kwa kusali na kutafakari juu ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kwa njia hii, aliweza kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Baba yake wa mbinguni.Kipindi cha Pasaka uwe ni muda muafaka wa kusali  na kutafakari Neno la Mungu ambalo linapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kielelezo cha imani tendaji!

Wakristo wanakumbushwa kwamba, Kristo Mfufuka ni kiini cha imani, matumaini na mapendo ambayo yanapaswa kushuhudiwa katika maisha ya watu! Hili linawezekana kwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu! Waamini wajenge utamaduni wa kuthubutu kusamehe na kusahau, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia hii, Rwanda inaweza kupeta katika mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.