2016-04-01 09:58:00

Wosia wa kitume: "Furaha ya Upendo" kuzinduliwa tarehe 8 Aprili 2016


Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 31 Machi 2016 ametangaza rasmi kwamba, Waraka wa Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Injili ya familia, utazinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Aprili 2016. Waraka huu unajulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Amoris Laetitia” “Furaha ya Upendo” ndani ya familia. Waraka huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu kuhusu familia. Sinodi ya kwanza iliadhimishwa kunako mwaka 2014 na awamu ya pili kunako mwaka 2015, kuonesha jinsi ambavyo Kanisa linatoa uzito wa juu kabisa  kuhusu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo!

Uzinduzi wa Wosia wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris Laetitia” “Furaha ya upendo” ndani ya familia utafanywa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu; Kardinali Christoph Shonborn, Askofu mkuu wa Vienna pamoja na Professa Francesco Miano na mkewe Professa Giusephina De Simone.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.