2016-04-01 08:37:00

Jumapili ya huruma ya Mungu!


Padre Wojciech Adam Koscielniak kutoka katika kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anafafanua kwa kina na mapana kuhusu Jumapili ya huruma ya Mungu ambayo kwa mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inaadhimishwa kwa kishindo kikubwa, kwa kuwakusanya waamini na vyama vya kitume vyenye Ibada kwa huruma ya Mungu, kumzunguka Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha na hatimaye katika ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 3 Aprili 2016.

Padre Wojciech Adam Koscielniak anasema, maandalizi ya maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II yaanza rasmi Ijumaa kuu, Kanisa linapoadhimisha Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Kumbe, Novena yaani Siku tisa za Sala ni kipindi muhimu sana kwa waamini kuweza kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Jumapili hii.

Kwanza kabisa waamini wanapaswa kutubu dhambi zao na kujibandua kutoka kwenye nafasi na mazoea ya dhambi; kuungama, ikiwezekana kabla ya maadhimisho yenyewe; kupokea Ekaristi Takatifu kwa Ibada na uchaji, kutukuza na kuheshimu Picha Takatifu ya Yesu mwenye huruma sanjari na kuwaonesha wengine huruma katika maisha yao! Novena hii ina chimbuko lake kunako mwaka 1937, Kristo Yesu alipomwomba Sr. Faustina kufanya Novena maalum kwa nia mbali mbali.

Kumbe, hizi siku tisa za sala na tafakari anasema Padre Wojciech ni hija ya waamini wanaopita katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Yesu Mfufuka anajidhihirisha kwa wale aliopenda kujifunua kwao baada ya Ufufuko wake. Hii ni Pasaka ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo na kilele cha huruma yake ni kwenye Fumbo la Msalaba. Maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu ni kipindi cha neema na baraka; hapa waamini wanapaswa kujiaminisha na kujikabidhi kabisa kwa Yesu Kristo na kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwapyaisha katika maisha yao, tayari kuwaongoza kuelekea kwenye Lango la huruma ya Mungu!

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakutakia maandalizi mema ya Jumapili ya huruma ya Mungu wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.