2016-04-01 16:07:00

Jengeni utamaduni wa watu kukutana!


Bara la Ulaya linaendelea kukabiliana na changamoto kubwa zinazogusa na kutikisa misingi ya maisha ya kiroho, kimaadili, kitamaduni, kisiasa na kiutu. Ili kuwa na mwelekeo makini, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu yanapaswa kupewa msukumo wa pekee katika sera na mikakati ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana huku ushuhuda wa imani ukipewa nafasi yake kwani una mvuto na mashiko kwa watu wa nyakati hizi na wala si bure hata kidogo!

Utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni mambo yenye mafao makubwa kwa binadamu, lakini utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine ni hatari kwa maisha ya binadamu kwani unatengeneza na kuunda makundi ya maskini, wale “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na wale wanaoshiba na kusaza kwa kutumia migongo ya maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Leo hii kuna hatari ya kila taifa kutaka kujifungia katika utambulisho na ustawi wake, badala ya kujenga utandawazi wa mshikamano unaoongozwa na kanuni auni! Bara la Ulaya kwa sasa linaoneka kuwa limechoka, linahitaji kujipyaisha kwa kuwa na mbinu mkakati wa tunu msingi za Injili ya familia sanjari na kuendeleza historia na mapokeo yake, vinginevyo, Bara la Ulaya litabaki kuwa ni utupu unaoshuhudiwa na watu waliokengeuka kimaadili; watu wasiothamini mwingiliano na tamaduni nyingine kama sehemu ya mchakato wa utajiri na wala si kikwazo cha maendeleo. Ni kiongozi gani Barani Ulaya anayeweza kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu?

Hizi ni kati ya changamoto ambazo Baba Mtakatifu Francisko amegusia wakati alipokutana na kufanya mazungumzo ya kisiasa na kiuchumi na kikundi cha wanasayansi jamii kutoka Ufaransa. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, amewahi kufika nchini Ufaransa mara tatu tu, katika historia ya maisha yake. Lakini ni nchi ambayo ina jeshi kubwa la watakatifu na mashuhuda wa imani.

Ni eneo ambalo majadiliano ya kidini na kiekumene yanafanyika katika uhalisia wa maisha. Katika maisha yake ya kiroho, Baba Mtakatifu anasema, amekuwa akijirutubisha kwa tafakari zilizotolewa na waandishi wengi kutoka Ufaransa. Kuna haja ya kuwa na ushirikiano kati ya Serikali na dini, kwa kukazia uhuru wa kuabudu, ukweli na uwazi. Masuala ya maisha ya kiroho si mambo binafsi kwani yanapasa kushuhudiwa na watu katika maisha ya hadhara.

Siasa inapaswa kujikita katika uwajibikaji, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya sera za kiuchumi kukumbatia faida kubwa, utajiri na mali, kiasi cha kumtelekeza binadamu ambaye anapaswa kuwa ni kiini cha siasa na sera makini za kiuchumi. Huu ndio mwanzo wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; hapa maskini wanaendelea kuwa maskini; thamani na utu wao vinawekwa rehani. Takwimu zinaonesha kwamba, matajiri wakuu ishirini duniani wanamiliki takribani asilimia 80 ya utajiri wote wa dunia! Hili si jambo la kawaida anasikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko. Fedha inapaswa kukita mizizi yake katika huduma, ustawi na maendeleo ya wengi na wala si kinyume chake. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kuinama na kuguswa na mahangaiko ya watu maskini kwa kujikita katika mchakato wa mshikamano unaosimikwa katika kanuni auni. Huruma isaidie watu kuwahudumia wale wanaokumbwa na majanga asilia; kuwajibika katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu ni dhana inayojikita katika mafundisho ya dini mbali mbali duniani. Ni changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kidini ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Anakiri kwamba, ameguswa kwa namna ya pekee na hija yake ya kitume nchini Afrika ya Kati. Hapo aliweza kutembelea na kuzungumza na waamini wa dini ya Kiislam katika msikiti wao, Akaomba ridhaa kutoka kwa Imam, ili aweze kusali kidogo, akavua viatu vyake kwa heshima na kusali.

Kila dini ina waamini wenye misimamo mikali na kwamba, kwa sasa anajiandaa kukutana na ujumbe wa viongozi dini ya Kiislam, dhehebu la Wasuni kutoka Chuo Kikuu cha Al Azhar, kilichoko mjini Cairo, Misri, ili kuendeleza majadiliano ya kidini; ili kujenga utandawazi wenye mshikamano. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anataka kuliongoza Kanisa kutoka ufichoni, ili kukutana na watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.