2016-04-01 09:07:00

Huruma ya Mungu inaadhimishwa zaidi katika Fumbo la Pasaka!


Huruma ya Mungu inaadhimishwa katika maisha ya ufufuko. Hili ndilo linaonekana katika Jumuiya za mwanzo kabisa za kikristo baada ufufuko wa Kristo na kwa hakika huu ndiyo utume wa Kanisa zima kama tunavyokumbushwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kitabu kiitwacho “Jina la Mungu ni Huruma” wakati tukiadhimisha Jubilei ya Huruma ya Mungu akisema: “Ninaamini kwamba hizi ni nyakati za huruma. Kanisa linaonesha haiba yake ya kimama, uso wake wa kimama kwa ubinadamu uliojeruhiwa. Halingoji hadi majeruhi huyu aje kugonga mlango, linawatafuta katika mitaa, linawakusanya, linawakumbatia, linawatunza, linawafanya wajisikie kuwa wanapendwa”.

Somo la kwanza linatudhihirishia utendaji huo wa jumuiya ya mwanzo ya kikristo, yaani Kanisa la mwanzo baada ya ufufuko wa Kristo. Ilikuwa ni jumuiya ilioyojaa upendo na uwezo wa Mungu ulionekana ndani ya jumuiya hii. “Kwa mikono ya mitume zilifanyika ishara na maajabu mengi katika watu”. Neno la Mungu linaendelea kutufafanulia jumuiya hii ya mwanzo kwamba “walizidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume kwa wanawake”. Kwa hakika ni jumuiya iliyouonja upendo wa Kristo mfufuka kwa nguvu na maajabu ya Mungu yalikuwa yakitendeka ndani mwake. Wenye matatizo mbalimbali waliletwa na kuponywa na mitume kwa sababu tu ya imani yao kwa Kristo mfufuka alitenda kazi pamoja nao.

Jumuiya hii ya mwanzo inadhihirisha uwepo wa Kristo mfufuka ndani mwao na ndiyo maana neema ya Mungu inafuguliwa ndani mwao. Neema hii inawaonjesha huruma ya Mungu ambalo kimsingi ndilo jukumu la Kanisa kwa nyakati zote. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutufundisha kwamba: “Kimsingi, huruma ndiyo kiini cha ujumbe wa Injili, ni jina la Mungu mwenyewe, uso wake aliojifunua katika Agano la Kale na katika ukamilifu kabisa kwa Yesu Kristo, umwilisho wa upendo wa uumbaji na ukombozi. Upendo huu wa huruma huung’arisha uso wa Kanisa na unadhihirishwa kupitia masakramenti, kwa namna ya pekee sakramenti ya upatanisho, ikiwa pamoja na matendo ya huruma ya jumuiya nzima au mtu mmoja mmoja. Kila linalofanywa au kutamkwa na Kanisa linaonesha kwamba Mungu ana huruma kwa watu”.

Jumuiya inayoonja maisha ya ufufuko inaendelea kualikwa kuishi katika hali ya furaha na kujiamini bila kuwa na mashaka yoyote. Katika somo la pili Kristo mfufuka anasisitiza hilo: “usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu”. Uwepo wa Kristo mfufuka ni sababu tosha ya jumuiya hii kuwa na nguvu na kutembea pasi hofu wala mashaka. Ni wazi kwamba katika hali ya kibinadamu tukio la kukamatwa, kuteswa na kuuwawa kwa Mwalimu wao liliwavunja nguvu. Yote waliyoyatumaini yalionekana kuishia gizani. Lakini sasa yu mzima, uthibitisho wa nguvu ya kimungu iliyokuwa inatenda kazi pamoja naye. Kumbe hatupaswi tena kuendelea kumtafakari kana kwamba amepotea, kana kwamba mafundisho yake yalikuwa utupu, la hasha, tunapaswa kumwendea kwa imani kubwa na kumsikiliza Yeye aliye mwalimu mwetu wa uzima.

Mitume wenyewe wanapata nguvu na matumaini baada ya kuwatokea wakati wakiwa wamejifungia “kwa hofu ya Wayahudi” kama tunavyoelezwa na Injili ya leo. Ndiyo hao hao, wakiongozwa na Mtume Petro, wanaokuwa mashuhuda kwa Jumuiya ya kwanza ambayo tumeisikia katika somo la kwanza. Zawadi ya kwanza wanayopatiwa na Kristo mfufuka ni amani: “Amani iwe kwenu”. Kisha anawavuvia Roho Mtakatifu: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”. Huu ni ufafanuzi wa jinsi ambavyo dhambi inavyotoa amani ndani ya maisha ya mtu binafsi na ndani ya jumuiya nzima. Hivyo mwanzoni kabisa Kristo mfufuka anatoa tangazo hili la huruma ya Mungu kama utume wa kwanza kwa wafuasi wake na huku wakiwezeshwa na Roho Mtakatifu kusudi amani itawale ndani mwao. Bila amani hofu utawala, kutokuaminiana kati ya wanadamu kunaongezeka na upendo kati yetu hupotea.

Ushuhuda wa ulimwengu wetu wa leo ambao unaelekea kupoteza amani kuanzia kwa mtu binafsi, familia na hata kwa jumuiya nzima ya wanadamu ni udhihirisho kuwa Kristo mfufuka anakosa nafasi ndani mwetu. Ni udhihirisho kwamba bado tunalo jukumu kubwa la kuidhihirisha huruma ya Mungu, utume wa kwanza kabisa na zawadi tunayoipokea kutoka juu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hapa ndipo tunaweza kuona maana na uzito wa mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu tunaouadhimisha kipindi hiki. Ni tendo ambalo linahitajika zaidi kwa wanadamu pengine kuliko vipindi vingine vyote kusudi kanisa liweze kutumika kama njia ya kuufunua upendo wa Mungu, Baba yetu mwenye huruma, upendo ambao unajifunua katika Kristo Mfufuka kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Jambo la mwisho ambalo ingefaa pia kulitafakari leo hii ni juu ya umuhimu wa maisha ya jumuiya. Kristo mfufuka anajidhihisha katika maisha ya jumuiya kwani tunapokuwa wawili au watatu ndipo tunapoweza kupendana, kusameheana, kusaidiana, kupongezana na kupenana misaada ya kila aina. Kristo mwenyewe anatuhakikishia katika Injili kwamba “walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Mt 18:20). Mtume Tomaso anakuwa na mashaka juu ya ufufuko wa Kristo, anashindwa kuuonja upendo na huruma yake kwa sababu tu hakuwepo pamoja na wenzake wakati  Kristo Mfufuka alipowatokea. “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo”. Kristo anapowatokea tena mara pili na kumtaka Mtakatifu Tomaso kutenda kama alivyonuia yeye anaishia tu kukiri “Bwana wangu na Mungu wangu”.

Namna hii ya imani ndiyo tunayoishuhudia kwa kiasi katika ulimwengu wa leo: imani ya uthibitisho. Ni athari za sayansi na falsafa za wakati huu zinatupeleka huko na mara nyingi hututenga na jamii ya waamini. Tunashindwa kuonja wema wa Mungu kupia maisha na huduma za Kanisa na wanakanisa, mathalani Sakramenti kama vile Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Kitubio, matendo ya upendo kutoka kwa wenzetu na mengineyo mengi yanayomshuhudia Kristo Mfufuka. Tunabaki tumejifungia katika mioyo yetu tukitaka kutia mikono katika kovu za mishumari ndipo tuamini. Mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu unaendelea kutualika kujifunua na kujumuika na wenzetu na humo ndimo tunaweza kuchota huruma na upendo wa Mungu, humo ndimo pekee tunapoweza kukiri “Bwana wangu na Mungu wangu”.

Nakualika katika Dominika hii tunapoendelea kusherehekea Sherehe hii kubwa ya wokovu wetu tuendelee kuifurahia huruma ya Mungu. Huruma yake ndiyo inatupatia amani na furaha. Huruma yake ndiyo inaufunua ukuu wa Mungu kwetu. Tuwe tayari kujifunua na kuipokea huruma hiyo kupitia maisha ya wenzetu ndani ya Kanisa jumuiya inayoalikwa kuadhimisha daima huruma ya Mungu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.