2016-04-01 15:50:00

Huruma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko kwa waraka wake wa kitume, “Misericordiae vultus” “Uso wa huruma” akatangaza rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, unaoongozwa na kauli mbiu “Iweni na huruma kama Baba” Anasema, Yesu Kristo ni huruma ya Baba wa milele na kwamba, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. Huruma ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu.

Tarehe 8 Desemba 2015, Baba Mtakatifu Francisko akazindua rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, Kanisa likafungua rasmi Malango ya huruma ya Mungu. Hapa Kanisa linapenda kujikita katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha na utume wake, kama walivyokaza kusema Mtakatifu Yohane wa XXIII na Mwenyeheri Paulo VI. Huruma ni jina na utambulisho wa Mungu kwa waja wake.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, wakati wa Kipindi cha Kwaresima, waamini wakaadhimisha mpango mkakati wa saa 24 kwa ajili ya Bwana. Hii ilikuwa ni nafasi kwa waamini kujipatanisha na Mungu kwa kukimbilia kwenye kiti cha toba ili kutubu, kuungama na kufanya malipizi ya dhambi. Sakramenti ya Kitubio anasema Baba Mtakatifu inamwezesha mwamini kuona ukuu wa upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Jumatano ya Majivu kwa mwaka 2016 aliwatuma Wamissionari wa huruma kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kuwatangazia na kuwapatia waamini huruma ya Mungu kwa kuwaondolea dhambi ambazo kimsingi zinaondolewa tu na Kiti cha kitume, yaani Vatican. Hii ni ishara wazi ya Baba mwenye huruma na kwamba, Wamissionari hawa wanapaswa kuonesha huruma ya Mungu katika huduma hii nyeti!

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kutoa katekesi kuhusu dhana ya huruma ya Mungu katika Maandiko Matakatifu. Baraza la Toba ya Kitume, moja ya taasisi nyeti sana katika maisha na utume wa Kanisa, kuanzia tarehe 31 hadi tarehe 1 Aprili 2016 limefanya kongamano la kimataifa kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Mauro Piacenza, mkuu wa Baraza la Toba ya Kitume anasema, Kanisa ni shuhuda na mhudumu wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu wa Mungu mintarafu Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu. Huruma ni msingi thabiti wa uhai na maisha ya Kanisa unaopaswa kujidhihirisha katika shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Kanisa linatumwa kumwilisha huruma na upendo katika maisha na vipaumbele vyake. Kanisa ni chombo na shuhuda wa: furaha, huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Katika maisha na utume wake, Kanisa kwa nyakati zote, limeendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, ili kuondokana na kishawishi cha watu kudhani kwamba, wanaweza kujiokoa wenyewe!

Yesu Kristo mwenye moyo mpole na mnyenyekevu ni sura ya huruma ya Baba wa milele na kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, analijenga na kulidumisha Kanisa, kwani Kanisa ni Sakramenti ya wokovu wa jumla. Huruma hii inasambaa na kuwafikia wengi kwa njia ya sadaka na majitoleo ya Mapadre ambao wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya Mafumbo ya Kanisa.

Kwa upande wake Professa Bruna Costacurta kutoka Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma anasema, Yesu ni uso wa huruma ya Mungu; Mkate ulioshuka kutoka mbinguni na kwamba, Yesu katika maisha na utume wake, aliwaonesha watu dira na njia kwenda mbinguni. Alionesha na kushuhudia ushindi dhidi ya dhambi, kwa kuwataka watu kujipatanisha na Mungu, ili waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao!

Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, mwamini anatubu, anaungama na kutimiza malipizi ya dhambi zake, ili kweli huruma, msamaha na upendo wa Mungu uweze tena kupata maskani moyoni mwa mwamini huyu! Sakramenti ya Upatanisho inamwezesha mwamini kuonja ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Maandiko Matakatifu yanaonesha hija ya maisha ya mwamini inayosheheni huruma na upendo wa Mungu, hata pale mwanadamu anapokengeuka na kumwasi Mungu.

Padre Francesco de Feo kutoka katika Chuo kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselm kilichoko mjini Roma anasema, Bikira Maria ni tabernakulo ya kwanza ya huruma ya Mungu iliyofanyika mwili. Mwelekeo huu unapata utajiri wake kwa njia ya sala na katika nyimbo za liturujia zinazomtaja Bikira Maria kuwa ni Mama wa huruma ya Mungu; Kimbilio la wakosefu na Lango la mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.