2016-03-31 15:33:00

Mtakatifu Faustina na Huruma ya Mungu!


Mtakatifu Faustina Kowalska ni mtume hodari na maarufu wa huruma ya Mungu katika kipindi cha mapambazuko ya millenia ya tatu ya Ukristo. Kwa njia ya maisha, utume na maandiko yake, watu wengi wameguswa na kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kiasi cha kujiaminisha katika huruma ya Mungu ambayo imefikia kipeo chake katika maisha na utume wa Kristo Yesu.

Mtakatifu Yohane Paulo wa II alitambua dhamana na mchango wa Mtakatifu Faustina katika ustawi na maendeleo ya mamillioni ya waamini duniani, kiasi kwamba, leo hii kuna mamillioni ya watu wenye Ibada kwa huruma ya Mungu. Kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba, Kanisa linamkumbuka Mtume wa huruma ya Mungu. Ni Mtakatifu ambaye hakuwa amebobea sana katika masomo, lakini nyaraka zake zina utajiri mkubwa sana katika maisha ya kiroho, chachu ya utakatifu wa maisha, kwa wale ambao watafuata ushauri wake wa maisha ya kiroho!

Mtakatifu Faustina alipewa dhamana ya kueneza Ibada ya huruma ya Mungu, ambayo leo hii imeenea sehemu mbali mbali za dunia na kwa namna ya pekee, watu wengi wameguswa na huruma ya Mungu, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa hakika, hiki ni kipindi cha kuadhimisha huruma ya Mungu inayomwilishwa katika hija ya maisha ya binadamu: kiroho na kimwili.

Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya kuguswa na ujumbe wa huruma ya Mungu, akaanzisha Jumapili ya Huruma ya Mungu inayoadhimishwa kila mwaka Jumapili ya pili baada ya Sherehe ya Pasaka, kwa mwaka huu, Jumapili hii inaadhimishwa hapo tarehe 3 Aprili 2016. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki katika mkesha na hatimaye, maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu. Huu ni ufunuo binafsi, lakini ambao umechangia katika kulifahamu kwa kina zaidi Fumbo la Huruma ya Mungu katika historia ya ukombozi.

Hii ni tafakari ambayo imeandikwa na Padre Seraphim Michalenko, Msimamizi wa Madhabau ya Kitaifa ya Huruma ya Mungu mjini Stockbridge huko Massachusetts, Amerika katika kitabu chake kuhusu maisha ya Mtakatifu Faustina, kilichochapishwa kunako mwaka 2015. Ni kweli waamini wengi wamesoma tafakari na kumbu kumbu zake, pengine bila kufahamu mchango mkubwa ulioletwa na Mtakatifu Faustina katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Huruma ya Mungu ni mwendelezo wa Agano Jipya na milele lililoanzishwa na Kristo Yesu na kwamba, Kanisa limejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii na Kristo Yesu ndiye jiwe kuu la pembeni. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanatambua na kuthamini karama mbali mbali ambazo Roho Mtakatifu analijalia Kanisa katika maisha na utume wake. Mtakatifu Yohane Paulo II aliguswa kwa namna ya pekee na huruma ya Mungu katika maisha na utume wake; changamoto ambayo imekuzwa na kuendelezwa kwa namna ya ajabu na Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameitisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha toba, wongofu wa ndani na msamaha, tayari kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili, kama anavyosema Mtakatifu Faustina kwa ajili ya ujio wa pili wa Kristo, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watu watahukumiwa kutokana na matendo ya huruma kwa maskini na wahitaji zaidi. Mtakatifu Faustina alijitosa bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu, ili Kristo atakapokuja mara ya pili, aweze kuwahukumu watu wake kwa haki. Huruma ya Mungu iwasaidie waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma hii kwa watu wa nyakati hizi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.